CHUO cha Taifa cha Usafirishaji (NIT)
kinatarajia kuanza kutoa mafunzo ya kozi ya Uhandisi wa kutengeneza ndege (Air
craft maintenance enginearing) kwa ngazi ya cheti na Astashahada ifikapo
Novemba, mwaka huu chuoni hapo.
Akizungumza na MTANZANIA jijini Dar es
Salaam kwenye maadhimisho ya 13 ya siku ya wahandisi nchini, Ofisa Uhusiano wa
NIT, Juma Manday alisema tayari idadi kubwa ya vijana imejitokeza kutaka kusoma
kozi hiyo.
“Kwa mara ya kwanza NIT tunatarajia kutoa
mafunzo hayo nchini ili watanzania wengi wapate fursa ya kusoma kwani awali
iliwalazimu kwenda nje ya nchi ambapo walilipia gharama kubwa,” alisema.
Alisema wanaamini kwamba mafunzo hayo
pindi yatakapoanza yatasaidia kuzalisha wataalamu vijana wa kitanzania ambao
watakakuja kutengeneza ndege kwa ajili ya nchi yao.
“Tunataka kusaidia Taifa letu, vijana hawa
wasome hapa hapa badala ya kwenda nje ya nchi ili tuzalishe wataalamu wazalendo
ambao wataweza kuja kututengenezea na sisi ndege yetu,” alisema.
Alisema hatua hiyo itasaidia pia kupunguza
tatizo la ajira na hatimaye kuinua uchumi wao na Taifa kwa ujumla.
Source Mtanzania newspaper
Chapisha Maoni