Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement


http://www.mwananchi.co.tz/image/view/-/3456506/lowRes/1492490/-/p6yhku/-/mrefu+pic.jpg 
NA VERONICA ROMWALD, DAR ES SALAAM

KIJANA, Baraka Elias (35) mwenye urefu wa futi 7.4 anayesubiri kufanyiwa matibabu ya kubadilisha nyonga yake ambayo imevunjika, hatapewa tena rufaa ya kwenda nje ya nchi kufuata matibabu hayo.

Badala yake atafanyiwa upasuaji pale pale katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI) ambako anapatiwa matibabu ya kutuliza maumivu yanayomkabili hivi sasa.

Mkurugenzi wa MOI, Dk. Othuman Kiloloma alisema hayo jana alipozungumza na MTANZANIA lililotaka kujua hatma ya matibabu ya kijana huyo kwani awali MOI ilishindwa kumfanyia upasuaji huo kutokana na umbile lake.

Ilielezwa kwamba madaktari walishindwa kumtibu kwa sababu mashine za MOI hazikuwa zinalingana na urefu wake.

Mkurugenzi huyo alisema baada ya changamoto hiyo kujitokeza, walilazimika kuunda jopo la madaktari ambalo lilifanya tathmini ya matibabu ya kijana huyo.

“Kwa kuwa umbo lake ni kubwa ikilinganishwa na watu wengine, tulipokwama awali ilitulazimu kuunda jopo la madaktari kufanya tathmini na maamuzi ya hatma ya matibabu ya Elias.

“Jopo hilo lilikuwa chini ya Daktari wetu, Lupondo, tayari limefanya tathmini na imeonekana kwamba kifaa anachohitaji kinaweza kupatikana, hivyo badala ya kumpa rufaa kwenda nje tumewasiliana na nchi tatu ili tupate kifaa hicho,” alisema.

Dk. Kiloloma alitaja nchi ambazo wamewasiliana nazo ili kupata kifaa kinachohitajika kufanikisha upasuaji huo kuwa ni Ujerumani, Marekani na India.

“Hawa wana viwanda vinavyotengeneza kifaa hicho kwa ubora, hatujajua hadi kitakapofikishwa hapa kitagharimu kiasi gani itategemeana na bei ya manunuzi.

“Na kwa sababu ya umbile lake watalazimika pia kubadilisha kidogo mfumo wa mashine zao ili kupata kile kitakachomtosheleza mgonjwa wetu kwa hiyo bado hatujajua pia kitawasili lini nchini,” alisema.

Mkurugenzi huyo alisema upasuaji wa kijana huyo utafanyika katika chumba cha upasuaji wa taasisi hiyo na kwamba atatumia kitanda kama wanachotumia watu wengine.

“Changamoto kubwa ilikuwa ni kupata kifaa cha kumtosha, hatuagizi na kitanda, tutatumia tu hivi vilivyopo maana amezidi kiasi cha kama futi moja tu,” alisema.

Awali akizungumza na MTANZANIA, Elias alisema bado anasubiri majibu kutoka kwa uongozi wa hospitali hiyo.

“Bado nipo nyumbani naugulia maumivu… wamenipa dawa za kutuliza, sijui lini hasa nitapata matibabu,” alisema.

Elias aliliambia gazeti hili kuwa chanzo cha tatizo lake, alipata hitilafu ya nyonga baada ya kuanguka kwenye ngazi za nyumbani kwake mkoani Ruvuma na tangu wakati huo hakuweza kuendelea kufanya shughuli zake za kiuchumi.

Alisema baada ya muda kidogo alipelekwa Hospitali ya Peramiho ambako alifanyiwa kipimo cha X-ray na kuonekana nyonga yake ilikuwa imevunjika.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement