Ijumaa, 24 Februari 2017

MOI: YAMRUHUSU MATUMLA KUREJEA NYUMBANIMatumla akizungumza na mmoja wa madaktari waliomtibu katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI) kabla ya kuruhusiwa kurudi nyumbani mapema wiki hii.
 
NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

BONDIA Mohamed Matumla (30) aliyekuwa amelazwa katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI), ameruhusiwa kurudi nyumbani.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Ofisa Uhusiano wa MOI, Patrick Mvungi alisema Matumla aliruhusiwa jana na madaktari wake ambao walijiridhisha maendeleo ya afya yake kuwa ni mazuri.

“Tunapenda kuwaarifu wanamichezo wote hususani wapenzi wa Mchezo wa Ngumi Tanzania kwamba tumemruhusu Matumla kwenda nyumbani. Tumejiridhisha kwamba afya yake imetengamaa vizuri,” alisema.

Mvungi alisema wataendelea kumfuatilia kama mgonjwa wa nje (Out patient) kwenye kliniki zao.

“Hivyo tuendelee kumuombea ili Afya yake iendelee kuimarika zaidi,” aliongeza.

Bondia huyo hivi karibuni alifanyiwa upasuaji mkubwa wa ubongo kuondoa damu iliyokuwa imevilia ndani ya kichwa chake.

Alipatwa na hali hiyo baada ya kupigwa ngumi kichwani na bondia mwenzake, Mfaume Mfaume katika raundi ya saba katika pambano lisilo la ubingwa lililofanyika hivi karibuni, jijni Dar es Salaam.


Kaimu Mkurugenzi wa MOI, Dk. Othuman Kiloloma alisema, Matumla atalazimika kukaa nje ya ulingo kwa kipindi cha miezi minane hadi 12 baada ya kufanyiwa matibabu.

Alisema atarejea ulingoni baada ya kuisha kwa muda huo hata hivyo atalazimika pia kupta kibali cha daktari.
 http://3.bp.blogspot.com/-2XpGKYZYUDA/TwGP59Yuq2I/AAAAAAABObM/jplMoErRV_I/s1600/DSC_0555.JPG
“Matumla atalazimika pia kuvaa kofia ngumu maalumu (helment) kichwani ili kuzuia eneo ambalo tulifumua ili kuondoa damu iliyoingia ndani ya ubongo lisije likapata madhara akiwa ulingoni,” alisema.