Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement
https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEgwY3_CaPZRoyyTTJZpd7SHs8V993rpCnbnSJHhJlHKztkRPljSX15CWGgXdU7VaB_glyFZZkagtZGhjcjTOmaD4SZzttuOiBEnRCWaFym7ezpjPH9RoYeyJIUPAT6WHpibHBgYdFFG8HD6/s1600/23.JPGNA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

WAPO ndugu, jamaa na rafiki zetu ambao hudai kuwa huwa wanakosa kabisa usingizi wakati watu wengine wakiwa wamelala hasa nyakati za usiku.

Kuna ambao hudai hali hiyo huwatokea mara nyingi na sasa wameizoea kabisa hali hiyo na kuiona ni ya kawaida kabisa kwao.

Ingawa wapo ambao hutafuta msaada lakini wengi hukosea kwani huishia kwenda katika maduka ya dawa na kununua dawa za kuwasaidia na wao waweze kupata usingizi.

Hatua hiyo huwaweka katika hatari ya kupata matatizo mengi zaidi pasipo kujua kwamba kukosa usingizi pekee ni tatizo linalohitaji ufumbuzi tena wa haraka.

Daktari Bingwa wa Afya na Magonjwa ya Akili wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Said Bakari anasema kukosa usingizi ni tatizo ambalo baadae huathiri afya ya akili.

“Wengi hawajui jambo hili, kuna watu wenyewe hupenda ama kuonanekana wanajua sana kufanya kazi ofisini, hawana muda wa kupumzika kila wakati wanafanya kazi hawana muda wa kupumzika kabisa, wanapaswa kujua kwamba kufanya hivyo kunawaweka kwenye hatari ya kuathirika afya ya akili,” anasema.

Daktari huyo anasema watu wanapaswa kujua kwamba ubongo na akili navyo huhitaji kupumzika kama ilivyo kwa viungo vingine vya mwili wa binadamu.

“Mtu akifanya kazi nyingi pasipo kupumzika na akakosa usingizi baadae hali hiyo humsababishia kushindwa kufanya kazi kwa ufanisi na hivyo kujikuta akiharibu kazi ofisini kwake,” anasema.

Anaongeza “Aliyekosa usingizi hataonesha dalili sawa na yule aliyeanza kutembea barabarani, kwamba ataanza kuleta vurugu, watu wataona kiwango chake cha kufanya kazi kinashuka,” anasema.

Anasema wapo pia ambao hupata maumivu makali ya kichwa, hushindwa kuona vema na hata kupooza mwili.

“Unakuta mtu analalamika anasumbuliwa na maumivu ya kichwa mwaka wa pili kwa mfano akipimwa hakuna ugonjwa anaokutwa nao au haoni na akipimwa macho hayana tatizo, wengine walalamika tumbo linauma lakini wakipimwa pia hakuna matatizo. Akili ikipata mshtuko husababisha matatizo makubwa,” anasema.

Anasema wengine hupata matatizo ya akili kutokana na matatizo ya kifamilia.

“Unakuta mama na baba hawaelewani kwa kipindi cha muda mrefu baadae hali hiyo huweza kusababisha matatizo ya akili hata kwa watoto wao,” anasema.

Dalili

Anasema mtu mwenye matatizo ya akili mara nyingi huonekana kuwa na mawazo ambayo huwa hayapo katika hali ya uhalisia.

“Yaani ile ‘thinking capacity’ yake au na imani yake inakuwa imetoka kabisa nje ya uhalisia, kwa mfano unasikia wote tunajua sisi ni binadamu na si Mungu na tunaamini kwamba Mungu yupo lakini anakuja mtu na kuanza kusema yeye ni Mungu na anasimama na msimamo wake huo.

“Unakuta anaanza kufanya vitu anavyodhani ni vya kimungu anapoulizwa ametoa wapi anatoa utetezi ambao mkiutazama mnaona kabisa anakabiliwa na tatizo la akili,” anasema.

Anaongeza “Wakati mwingine hutokea mtu na kudai wanadamu wote ni wake, yupo mmoja ambaye alitueleza karibu watoto wote wa Tanzania ni wa kwake na anao wengine wengi Marekani, alisema amezaa na rais mmoja mkubwa duniani na kwamba hakuna mtu atakayemuambia amuelewe lolote, sisi tulijua moja kwa moja hilo ni tatizo la akili.

Anasema wapo pia ambao hujikuta wakisema magari yote yaliyopo jijini Dar es Salaam ni ya kwao na iwapo ikatokea akaingia katika gari la mtu huishia kuambulia kipigo.

“Wanapigwa mno wapo wengine wanakamatwa hadi ikulu na wengine wanazuka tu huko barabarani na kuanza kuwafanyia maombezi watu wanaopita barabarani,” anasema.

Anasema watu waliopata tatizo la akili huhisi vitu ambavyo havipo katika hali ya uhalisia.

“Tunajua kuna njia tano za utambui, kugusa, kunusa, kuonja, kuona na kusikia lakini watu walio katika hali ya kuchanganyikiwa huwa wanahisi, vitu ambavyo havipo.

“Kwa mfano anaweza kuona watu wameshika silaha na mkimuuliza wapo wapi hao watu, mtamuona anawashangaa ninyi kwanini hamuwaoni, wakati mwingine wanaweza kusikia sauti ambazo nyie mliomzunguka hamzisikii kabisa,” anasema.

Anaongeza “Wengine hudai wamerogwa, ni imani ambayo ipo kwenye jamii zetu, wakati mwingine mtu mwenye tatizo la akili anaweza kudai amerogwa na kuwataja hao waliomroga, sasa ikiwa ni watu wa karibu yake, matokeo yake huishia kuzua ugomvo kwenye jamii na familia husika.

“Ndugu wanaposhtuka na kumleta hospitalini hugundulika kuwa hakurogwa bali alikuwa anasumbuliwa na tatizo la akili, basi hapo amani na furaha hurejea katika familia,” anasema.

Anaongeza “Wapo wengine huletwa wanadai kuwa wanasikia vitu au nyoka wanatembea ndani, tumboni. Yaani huwa wanakuwa na hisia potofu ambazo wakati mwingine humsababishia hofu kubwa na kuhisi kuwa hawapo salama.

“Ndipo pale unakuta mtu anashinda amejifungia ndani tu, anashindwa kwenda kazini au hata sokoni na wapo ambao hufikia hatua ya kuacha kazi kabisa.

“Unakuta kwanza anahama ofisi moja anakwenda nyingine ambako hadumu, anahama tena, yaani anaweza kuhama ofisi hata 10 na baadae anaamua kukaa nyumbani, kwa sababu, kwa mfano anakuwa analalamika kila akitoka anakuwa analalamika kuona watu wanaomfuata wakiwa wameshika silaha lakini nyie mkiangalia watu hao hamuwaoni,” anasema.

Anasema kukosa usingizi ni sababu kubwa ya maradhi ya akili kwani husababisha kutetereka afya ya akili kwa haraka.

Madhara

Anasema iwapo mtu hatawahi hospitalini kupata tiba tatizo hilo huanza kumuathiri yeye mwenyewe.

“Kwa sababu hushusha kiwango chake cha kufanya kazi kama awali hivyo uchumi wake utatetereka na jamii yake nayo huathirika maana hulazimu watu kuwa karibu naye wakimuhudumia.

“Afya ya mwili wake nayo hutetereka kwani kinga zake hushuka kwa kiwango kikubwa, magonjwa haya huleta matatizo pia kwenye ndoa nyingi na mwisho husababisha vifo,” anasema.

Yanatibika

Daktari huyo anasema magonjwa hayo yanatibika kama maradhi mengine ingawa yapo machache ambayo hayatibiki.

“Huwa tunatumia dawa kutibu maradhi haya lakini kama yametokana na hitilafu za kemikali (ya kurithi) huwa hayatibiki ingawa zipo dawa zinazosaidia kurekebisha kemikali hizo,” anasema.

Anasema huwa pia watumia njia ya ushauri wa kisaikolojia na matibabu ya jamii.

“Tunaposema matibabu ya kijamii tunamaanisha kwamba huwa tunaipa elimu jamii inayomzunguka mgonjwa, kwamba wasimtenge kwa hali aliyonayo maana hiyo itamfanya kuwa mpweke kama wanaandaa kikao kwa mfano basi na yeye ashirikishwe na akitoa maoni yapokelewe na ikiwezekana wampongeze.

“Ile inamsaidia kuona kwamba naye anathaminiwa lakini si kumkejeli na kumtamkia maneno ambayo ni ya kuudhi mfano kumuita kichaa au chizi si sahihi, huku ni kumnyanyapaa, huwa pia tunawapa matibabu ya kazi,” anasema.

Makala haya kwa mara ya kwanza yalitoka Februari, mwaka huu katika gazeti la MTANZANIA

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement