Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement
https://image.shutterstock.com/z/stock-vector-an-image-of-a-menstrual-cycle-chart-74110774.jpg 
NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

HEDHI ni mzunguko wa kila mwezi ambao huleta kutokwa na damu ukeni, hali hiyo hutokea pale ambapo yai la mwanamke linakuwa halijakutana na mbegu ya kiume ili kulirubutisha kutengeneza mtoto.

Kila mwanamke ana mzunguko wake wa hedhi, ingawa kwa kawaida hedhi ya kwanza hutokea katika umri wa miaka 12 na 13 hata hivyo wapo ambao huanza kupata hedhi katika umri mdogo wa kati ya miaka tisa hata 10.

Mzunguko wa hedhi hudhibitiwa na homoni zinazozalishwa na mwili wenyewe, hedhi hutokea pale ambapo tishu za ukuta wa mji wa mimba hubomoka na kutoka kama damu ukeni.

Hedhi ni kipindi maalumu katika maisha ya mwanamke aliyefikia umri wa kuzaa.

Kwa kawaida mzunguko wa hedhi hutokea kila mwezi na kila mwanamke anao mzunguko wake ni hapo ambapo mwili hujiandaa kwa hali ya kupata ujauzito.

Jinsi inavyotokea

Mwanamke ana ovary mbili (vifuko vya mayai) katika mwili wake, moja upande wa kushoto na nyingine kulia ambazo hutengeneza mayai ya uzazi.

Kila mwezi, ovary moja huachilia yai kitendo hicho kitaalamu huitwa ‘ovulation’ yai husafirishwa hadi katika mji wa mimba kupitia mirija ya uzazi.

Wakati huo mabadiliko ya homoni huuandaa mji wa mimba (uterusi) kutengeneza ukuta mpya uitwao ‘endometrium’ kwa ajili ya kujiweka tayari kwa mapokezi ya mimba inayoweza kutungwa.

Yai linalofika katika mji wa mimba (uterasi) iwapo halitarutubishwa na mbegu ya mwanamume, ukuta huo humeguka na kutoka nje ya mji wa mimba kupitia ukeni ukiwa pamoja na damu.

Kitendo hicho ndicho huitwa hedhi (menstruation) au mzunguko wa hedhi (menstruation cycle). Mara nyingi mwanamke hukoma hedhi anapotimiza umri wa kuanzia miaka 45 hadi 50.

Ingawa ni kipindi muhimu katika maisha ya mwanamke lakini huwa kimejaa changamoto ambazo huzipitia, changamoto hizo hutofautina kati ya mwanamke mmoja na mwingine.

Wapo ambao hupata hedhi kwa siku tatu na wengine huenda hadi saba na miongoni mwao wapo pia ambao hupata hedhi nyepesi na wengine nzito.

Wapo pia ambao hupata hedhi pasipo kukabiliana na matatizo yoyote lakini wengine hupata hedhi kwa uchungu na masumbufu mengi, kama kuumwa tumbo, mgongo, kichwa, kiuno na mengineyo.
https://www.wellandgood.com/wp-content/uploads/2016/12/lola-pad.jpgUsafi muhimu

Pamoja na yote hayo, suala la usafi ni jambo la muhimu mwanamke anapaswa kuzingatia kipindi chote maishani mwake, hasa kipindi cha mzunguko wa hedhi.

Ili kujiitiri katika kipindi hicho muhimu, mwanamke hulazimika kutumia kifaa maalumu ambacho hukinga damu ya hedhi ili asichafuke.

Inawezekana ikawa ni kitambaa kilichotengenezwa kwa ajili ya kazi hiyo iwe kwa njia ya asili au kisasa, hujulikana kama pedi au taulo za kike.

Enzi za mabibi zetu njia iliyokuwa ikitumika zaidi ni ile ya asili, walitengeneza vipande vya kanga au kitenge kujisitiri.

Lakini kukua kwa teknolojia kukapelekea kutengenezwa taulo za kisasa za kutumia na kutupa ambazo huuzwa kwa bei tofauti tofauti madukani.

Daktari

Akizungumza hivi karibuni na MTANZANIA, Daktari Bingwa wa magonjwa ya kinamama na uzazi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Belinda Balandya anasema kipindi cha hedhi ni cha muhimu kwa afya ya mwanamke.

“Mwanamke anapokuwa katika siku zake hulazimika kutumia taulo hizo ambazo kazi yake kuu ni kupokea ile damu inayotoka, kama hatavaa maana yake ni kwamba itapitiliza kuchafua nguo zake.

“Taulo za kutumia na kutupa jinsi zilivyotengenezwa zina ‘layer’ maalumu kwa ndani ambayo hufyonza damu ya hedhi, hulazimu kubadili mara nyingi (kiasi cha kila baada ya saa nne) hasa inapokuwa inatoka kwa wingi,” anasema.

Madhara ya kuvaa taulo muda mrefu

Daktari huyo ambaye pia ni muhadhiri wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi (Muhas) anasema kuna athari kubwa iwapo mwanamke hatazingatia usafi akiwa katika kipindi hicho katika via vyake vya uzazi.

“Kwa kuwa inanyonya damu maana yake ni kwamba hufika wakati unakuwa kama vile umevaa kitu kibichi, hivyo ngozi huanza kupata michubuko. Kwa wale ambao ngozi yao ni ngumu kidogo huwa si rahisi kuona michubuko hiyo lakini wanapojisafisha kwa maji na sabuni huhisi maumivu,” anasema.

Bakteria huzaliana

Anaongeza “Damu ni sehemu ambayo bacteria huota kwa urahisi kwa sababu wanakuwa wanapata chakula wanachohitaji kwa urahisi, mtu anaweza kuendelea kuvaa kwa sababu hajui jambo hili lakini ni hatari.

“Kwa sababu bakteria wanakua kwa urahisi husababisha pia muhusika kupata maambukizi katika sehemu zake za siri,” anasema.

Wanaotumia vitambaa

Anasema iwapo mtu anatumia vitambaa alivyovitengeneza kujisitiri navyo vinapaswa kukauka ili bakteria wasipate nafasi ya kuzaliana.

“Kumbuka kwamba nimesema bakteria huzaliana kwa urahisi kwenye damu, kitambaa kisipokauka na kubaki na unyevunyevu maana yake ni kwamba bakteria waliozaliwa watabaki hawajafa kwa hiyo wataendelea kukua hivyo muhusika atakuwa amejiweka kwenye ‘risk’ ya kupata ‘infections,” anasema.

Anaongeza “Kuna pedi  fulani...zimetengenezwa mfano wa unene wa  kidole na imewekwa kamba kidogo. Wapo wanawake wanazitumia, zinauzwa huko madukani, huingizwa ndani ya uke ili kufyonza damu na huitoa kwa kuvuta kamba hiyo inayokuwa imebaki nje ya uke.

“Sasa hizi ni taulo mbaya zaidi, wengine wanapoweka wakati wa hedhi chache, hujisahau kuzitoa na hivyo kujiweka kwenye hatari ya kupata madhara,” anasema.
http://www.news-medical.net/image.axd?picture=2012%2F11%2Futerus-1.jpg
Mfumo wa uzazi wa mwanamke

Athari yenyewe

Anasema bakteria hao huenda kutengeneza kovu katika mirija ya uzazi na mwisho huziba kabisa na kwamba huweza kupenya na kuingia hadi katika mfumo wa damu na kuleta athari zaidi.

“Kama mwanamke huyu hatawahi hospitalini anakuwa yupo kwenye hatari hata ya kushindwa kushika ujauzito kwa sababu bakteria hao huendelea kushambulia mfumo wake,” anasema.

Kauli za wanawake

Julieth Masinga Mkazi wa Mbezi Luis anasema awali hakuwa anajua iwapo taulo ya kike inaweza kusabisha madhara makubwa namna hiyo.

“Najua suala la usafi ni la msingi lakini sikuwahi kujua nini madhara ambayo yanaweza kujitokeza iwapo mwanamke atakaa muda mrefu akiwa amevaa taulo moja kwa muda mrefu,” anasema.

Anaongeza “Binafsi huwa sipendelei kukaa na taulo moja muda mrefu lakini kuna wakati unashindwa jinsi ya kufanya kwa mfano ukiwa safarini unatumia muda mrefu barabarani, ni changamoto kwa kweli.

“Kuna siku nilikuwa kwenye mizunguko yangu ya kibiashara nilitumia muda mrefu mno, nilikuwa kwenye siku zangu, kusema ukweli nilijihisi vibaya kukaa muda mrefu bila kujisafisha, nililazimika kutafuta bafu la kulipia nikaoga na kubadili pedi nyingine.

“Lakini itabidi tuzingatie ushauri wa daktari ili tuweze kujilinda afya zetu tusipate maambukizi,” anasema.

Mkazi wa Sinza Kijiweni, Pelina Yesaya anasema bado elimu kuhusu hedhi inahitajika hasa kwa kundi la wasichana wadogo.

“Kwa mfano huko vijijini bado kuna maeneo ambayo wasichana wanahitaji kuelimishwa zaidi kuhusu hedhi, jinsi inavyotokea na namna ya kujisitiri na hata kuepukana na mimba za utotoni,” anasema.

Anaongeza “Kule wengi hawajafikiwa angalau huku mjini watu wanao uwezo wa kutumia taulo ya kutumia na kutupa, kule wengi wanatumia taulo za asili, kwa hiyo kuna ulazima mkubwa wa kuwapelekea elimu kama hii ili wawe salama,” anasema.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement