Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Azim Dewji akizungumza na baadhi ya wafanyakazi wa MOI na waandishi wa habari (hawapo pichani) mapema leo, (mwenye koti jeupe) ni Mkurugenzi wa Tiba wa taasisi hiyo, Dk. Samwel Swai.
Na Veronica Romwald, Dar es Salaam
WAUMINI wa dhehebu la Shia nchini wamejitolea kuwezesha
matibabu ya watoto 40 waliozaliwa na tatizo la kichwa kikubwa ambao wamelazwa
katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI).
Akizungumza na waandishi wa habari mapema leo, Mwenyekiti wa
jumuiya hiyo, Azim Dewji amesema matibabu hayo yatagharimu kiasi cha Sh.
milioni sita.
Mkurugenzi wa Tiba wa MOI, Dk. Swai akiwafafanulia jambo wageni hao.
“Wiki mbili zilizopita tulikuja MOI na tukajitolea uniti 140
za damu lengo ni kufanikisha upasuaji wa watoto hawa na tulikusanya fedha kwa
ajili ya kuwezesha matibabu yao.
“Leo tumekuja tena, tumeahidi kuendelea kuchangia damu
kupitia shule ya Al-Muntazil. Wananchi wajue kwamba madaktari hawa wanafanya
kazi kwa moyo na kwa kujitolea ili kuokoa maisha ya ndugu zetu hawa, ombi langu
kwao waje wajitolee damu.
Hapa wakiwa wodini
“Wamenidokeza kila wiki zinahitajika uniti 100 kufanikisha
upasuaji, sasa Mungu ametujalia afya nzuri hivyo ni vema nasi tujitolee
kusaidia wengine,” ametoa rai.
Amesisitiza “Ukitoa damu hutakufa, jinsi tulivyoumbwa na Mungu
ndani ya miezi mitatu hadi minne damu yote uliyotoa inakuwa imerudi, ukitoa
damu unapata faida kuu tatu, kwanza unakuwa mtu mwenye huruma, unapata thawabu
kwa Mungu na unakuwa umeokoa maisha ya mtu.
Amesema jumuiya hiyo imejiwekea utamaduni wa muda mrefu
kuchangia damu katika Mpango wa Taifa wa Damu Salama kila mwaka angalau mara
moja lakini sasa wanakusudia kuchangia mara nne hadi tano.
“Tulikuwa tunafanya hivyo kila inapofika mwezi wa Ramadhani sasa
tutajitolea si mara moja tu kwa mwaka bali nne hadi tano hivyo nawaalika na
waumini wa wananchi wengine tuungane kuchangia damu,” amesema.
Chapisha Maoni