Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement

https://www.womenshealth.gov/files/styles/masthead/public/images/mh_woman-crossing-legs.jpg?itok=2mDGfY9_&c=fb0bb35101799fc7b9ace6dcd4defc95Na Veronica Romwald – Dar es Salaam

KUNA mtu leo hii akiambiwa asimame, azungumze mbele ya umati wa watu, anashindwa kabisa na iwapo atajitahidi kusimama anaweza kutokwa jasho jingi au kutetemeka kabisa na hata kusahau baadhi ya maneno aliyokusudia kuyazungumza.

Lakini wapo watu ambao wanao uwezo wa kusimama na kuzungumza kwa ufasaha pasipo kuwa na shaka yoyote ile.
Kuna mtu mwingine akiona kwa mfano mdudu mdogo kama mende ameingia ndani ya chumba chake basi yupo radhi kuhama kwa muda chumba hicho na kutafuta watu wa kumsaidia kumtoa mende huyo.

Simulizi ya John

John Simon mkazi wa Tegeta, Dar es Salaam anasema hawezi kabisa kusimama mbele ya umati wa watu na kuzungumza.

“Natamani mno kusimama na kuzungumza mbele za watu, lakini sijui kwanini huwa nakosa kabisa ule ujasiri, hofu kuu huwa inaniingia ndani ya moyo wangu,” anasema.

Simon anasema hata alipofanikiwa kuendelea na masomo yake ya sekondari alikuwa anachelewa kufika shuleni ili asichaguliwe kuzungumza kwenye gwaride.

“Shule niliyosoma, viranja waliweka utaratibu wa kuita wanafunzi mbele kuzungumza jambo, hasa siku ya jumatatu, basi nilikuwa nachelewa makusudi ili nisichaguliwe,” anasema.

Anasema hali hiyo anayo hadi leo na hajui kama anaweza kuondokana nayo.

“Jambo ninaloshukuru mimi sina nafasi yoyote ya uongozi kazini, nadhani wanajua nina udhaifu huu maana hawajawahi kunichagua kuzungumza, sijui lini nitaweza kupata ule ujasiri walio nao watu wengine,” anasema.
http://i1.wp.com/millardayo.com/wp-content/uploads/2016/07/cockroach.jpg?resize=720%2C302
Wapo watu wakimuona mende 'hutimua' mbio

Mariam

Mariam Eliud, Mkazi wa Magomeni anasema yeye akimuona mende ameingia ndani ya nyumba yake anakosa amani kabisa.

“Yaani bora nimuone nyoka simuogopi hata kidogo, nitampiga mwenyewe hadi nimuue lakini si mende, nikiona yupo ndani nakosa amani kabisa.

“Nyumba yangu ina vyumba viwili vya kulala, nipo radhi nihame chumba changu kwenda kingine, nitatafuta na mtu aje kunisaidia kumuua mende huyo kwa kutumia dawa maalumu ya kuua wadudu,” anasema.

Wazazi wanavyochangia

Msaikolojia Tiba wa Chuo Kikuu cha Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas), Isack Lema anasema wengi wanakumbwa na hali hiyo ukubwani lakini msingi wake ulianzia walipokuwa utotoni.

“Wazazi wengi hawajui, ni kosa kubwa kumtamkia maneno yanayomvunja moyo mtoto au kumshusha thamani.

“Unakuta mtoto anajitahidi kuonesha kipaji chake lakini mzazi anamvunja moyo na kumwambia hawezi kufika popote, au kwa mfano mwanafunzi ananyoosha mkono darasani kujibu swali akakosea, wenzake wakamcheka.

“Mwalimu anatakiwa amsaidie mwanafunzi husika, kumjenga, ili asiogope tena wakati mwingine kujibu, amsaidie kujenga ule ujasiri, wengi wanaoshindwa hata kusimama mbele ya watu ukubwani, walichekwa au kukatishwa tama walipokuwa utotoni,” anasema.
Nini hutokea

Lema (pichani) ambaye pia ni Daktari Bingwa wa Afya na Magonjwa ya Akili wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) anasema wasiwasi uliopitiliza ni tatizo la akili lakini wengi hudhani ni hali ya kawaida.

“Kila mmoja anaugua ugonjwa wa wasiwasi lakini si rahisi kuona watu wakija hospitalini kupata matibabu kwa sababu wengi hudhani ni hali ya kawaida, kwa sababu mara nyingi huwa si rahisi kusababisha athari za moja kwa moja, na utaona wengi huendelea kufanya shughuli zao za kila siku kama kawaida,” anasema.

Dk. Lema anasema kawaida magonjwa ya akili huanza na vitu ambavyo ni vya kawaida kabisa.

“Kwa mfano mtu alikuwa analala kwa saa nane inafika hatua hawezi tena kulala analala kwa saa mbili, hali hiyo ikiendelea kwa zaidi ya miezi mitatu tayari ni tatizo, inakuwa si hali ya kawaida tena bali ugonjwa,” anasema.

Kila mwanadamu ameumbwa na hofu

Daktari huyo anasema jinsi Mwenyezi Mungu alivyoumba mwili amemuwekea kila mtu hofu ndani yake.

“Ni hali tuliyoumbwa nayo katika mfumo wa akili, hofu ni sawa sawa na ‘alarm’ ya gari, kwa mfano  nikiigusa gari yangu vibaya ‘alarm’ itatoa mlio, kuashiria gari haikuguswa vizuri.

“Hofu katika maisha ya binadamu ni hali ambayo ipo na inatusaidia kuishi maisha yetu ya kila siku hasa tunapokabiliwa na hali za hatari,” anasema.
https://i.ytimg.com/vi/DVXtnWQ1LVw/hqdefault.jpg
Mwanamume akipambana na simba porini

Anaongeza “Kwa mfano tunajua kwamba simba ni mnyama hatari, ikitokea mtu akakutana naye porini, macho yake humsaidia kuona, hofu iliyopo ndani yake hutoa ishara na ubongo hupokea taarifa na kwamba kilichopo mbele yake ni kitu cha hatari.

Anasema kwa sababu hiyo, mwili nao ambao umeumbwa ukiwa na mfumo wa kumsaidia mtu kupambana nao huanza kujiandaa kukabiliana na hatari hiyo.

“Mwili utaachilia homoni na mhusika ataanza kukabiliana na ile hatari, kuna njia mbili ambazo muhusika ataweza kuzitumia ama kupambana na simba huyo au kukimbia, hofu ya namna hii ni ya kawaida kabisa,” anasema.

Kwa nini ni kawaida

Dk. Lema anasema kwa kuwa ni hali ya hatari na macho yamepeleka taarifa kwenye ubongo, nao utatuma taarifa kwa mwili ujiandae kupambana, ni hali ya kawaida.

“Cha kwanza mwili utahitaji muhusika avute pumzi ya kutosha ili kuweza kujiandaa, kisayansi mwili huvuta hewa ya oksijeni na kutoa nje hewa ya kabonidioksaidi,” anasema.

Anasema hewa hiyo huenda hadi kwenye mapafu na ikifika huko kuna mabadiliko ambayo hutokea katika pumzi iliyoingia ndani.
https://img.planespotters.net/photo/083000/original/5h-mwh-air-tanzania-airbus-a320-214_PlanespottersNet_083238.jpg
Kuna watu wanaogopa hata kupanda ndege

“Sasa mtu aliyekutana na simba, huanza kuvuta pumzi nyingi kwa nguvu, kwa kuwa anavuta kwa nguvu ile oksijeni inafika pale kwenye mapafu ambapo hata hivyo si kituo chake cha mwisho.

“Pumzi hiyo inatakiwa isafirishwe kwenda katika sehemu mbalimbali za mwili. Kwa kuwa anavuta pumzi kwa nguvu, matokeo yake ni kwamba mapigo ya moyo huanza kuongezeka, kuwezesha pumzi yenye oksijeni ifike sehemu zote za mwili,” anasema.

Hofu inavyogeuka kuwa ugonjwa

Dk. Lema anasema hofu hugeuka kuwa ugonjwa iwapo inatokea pasipo kuwa na kisababishi chochote cha hali ya hatari.

“Yaani, inakuja katika hali ya ghafla na inakuwa nje ya uwezo wa mtu husika kuweza kuitawala hiyo hofu na katika mazingira ambayo hakuna sababu ya muhusika kupata hofu,” anasema.

Anatoa mfano “Ni sawa na alarm ya gari inapopiga wakati hakuna kitu kilichoigusa gari husika. Hii inamaanisha alarm husika ina tatizo. Hofu inapompata mtu bila kuwapo kwa kisababishi cha hatari inakuwa si hofu ya kawaida tena (tuliyoumbwa nayo) bali ugonjwa wa wasiwasi.

Aina za magonjwa ya wasiwasi

Daktari huyo anasema wapo watu ambao hupata wasiwasi wa kuhamaki kitaalamu hali hiyo huitwa Panic- disorder.

“Unakuta mtu yupo mahali ghafla anapatwa na hofu, anahamaki, anakuwa kwenye tafrani kweli kweli na hata akafikia hatua ya kukung’ang’ania wewe uliyekaribu naye. 

"Lakini ukiangalia mazingira unaona kabisa hakuna kitu ambacho kinaweza kumfanya mtu kuingiwa na hofu namna hiyo,” anasema.
https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEiV1m-Y9YiG6Sjwh7_XmsqONGfOscHq4E03c88QIxuzNKLNoAqgUZl5oismq6bdYAF-Yng08rgEnPemshENontskYKIvjKHIlCW7HTFxz0N23iHGCth9inrVd7AVJIJZ0WcEdyylEbcIN4/s1600/MMGM1143.jpg
Wapo wanaoogopa kupanda au kupita kando kando ya majengo marefu au kusafiri baharini

Anasema wengine hupata wasiwasi ambao huendana na wao kuona vitu fulani fulani kwa mfano wadudu, wanyama, mabonde na vingine vingi.

“Kwa mfano kuna mtu akipanda lifti anapatwa na wasiwasi, anahisi akiingia kwenye lifti atakosa pumzi, joto litakuwa kali na matokeo yake atapoteza uhai wake, hivyo anashindwa kabisa kupanda lifti. Au mwingine anaogopa kupanda kabisa ndege,” anasema.

Anasema mwingine akikaa juu ya ghorofa au akienda sehemu ambapo pana mwinuko mrefu huhisi hali ya kizunguzungu .

“Wapo wengine wakiona damu wanapatwa na hali ya wasiwasi, kuna kundi la tatu la wasiwasi wa kijamii, unakuta kuna watu wanahisi kukaa katika kundi la watu wengi kuna kitu kinaweza kutokea.

“Hawa ndio wale ambao wakipewa nafasi ya kuzungumza mbele za watu wanahisi huenda kuna jambo baya linaweza kutokea au watamfikiria vibaya au atatokewa na vitu vya ajabu ajabu,” anasema.

Anasema wengine hupata wasiwasi wa kila kitu kilichopo mbele yake.

“Yaani wanakuwa si watu wa kuwa na uhakika wa kila jambo wanalofanya, wanahisi lazima watakosea, kwa sababu ni mambo ambayo huanza katika hali ya kawaida ili tuseme ni tatizo lazima dalili zisiwe za siku mbili tatu,” anasema.

Anasema lazima muhusika afanyiwe uchunguzi na wataalamu na dalili hizo awe ameziona kwa kipindi cha zaidi ya miezi mitatu.
http://a57.foxnews.com/images.foxnews.com/content/fox-news/us/2014/05/30/man-sentenced-to-life-for-shooting-that-claimed-life-seton-hall-student-from/_jcr_content/par/featured-media/media-0.img.jpg/876/493/1422712432124.jpg?ve=1&tl=1
Mara nyingi mtu hutumia mikono yake kuficha uso pindi anaposhikwa na uwoga

Dalili za ugonjwa

Anasema wakati ni hali ya kawaida kwa mtu anayekabiliana na hali ya hatari kuvuta na kutoa pumzi haraka haraka kwa mtu ambaye anapatwa na hali hiyo bila kuwa na kisababishi cha hatari hali huwa tofauti.

“Yule anayekabiliana na hatari ataona anavuta hewa katika hali ya kawaida lakini huyu ambaye hakabiliani na hatari yoyote atapata shida mno, ataanza kujiuliza kwanini mapigo yake ya moyo yamebadilika na kwenda kasi na anaanza kuhisi kifua kinakuwa kizito, hilo ni tatizo,” anabainisha.

Zimegawanyika

Daktari huyo anasema dalili za ugonjwa huo zimegawanyika katika makundi makuu matatu, ya kwanza ikiwa ni dalili ya mwili ambayo wengi huanza kuipata.

Mara nyingi muhusika huona ile pumzi anayoivuta ni ndogo, haimtoshi, kwa hiyo anaijitahidi kuivuta kwa nguvu na ndiyo maana anakuwa anahisi kama vile kifua kinabana na wakati huo huo mapigo ya moyo huanza kwenda kwa kasi,” anasema.

Anasema kwa kuwa wakati hali hiyo inatokea huwa kunakuwa na nguvu ambayo imeachiliwa ndani yake anaanza kutetemeka mwili.

“Wengine huanza kutokwa jasho jingi kiasi cha kulowanisha nguo zao, wapo wengine huhisi kabisa kama vile kuna kipepeo kinaruka ruka ndani ya tumbo,” anasema.

Huathiri kibofu.

Dk. Lema anasema mara nyingi inapotokea mtu akapatwa na ugonjwa wa wasiwasi humsababishia athari katika kibofu chake cha mkojo.

“Kibofu hulegea na ndiyo maana mtu hujihisi kwenda haja ndogo, kila anapopatwa na hali ya wasiwasi, wapo ambao huhisi kizunguzungu, wengine tumbo huunguruma na wapo ambao huishiwa kabisa nguvu mwilini na hata kupoteza fahamu kabisa,” anasema.
http://topnews.ae/images/mental-workspace-in-human-brain.jpg
Dalili za kiakili

Anasema hili ni kundi la pili la dalili, kwamba mtu huwa na hofu kuu, huhisi huenda kuna kitu kibaya ambacho kitatokea katika maisha yake.

“Unakuta anatafakari mno juu ya hayo anayodhani huenda yatamtokea matokeo yake mapigo ya moyo yanabadilika, yaanza kwenda kasi kwa hofu anayokuwa ameijenga ndani yake juu ya hayo anayohisi yatamtokea,” anasema.

Dalili za kitabia

Anasema watu wanaougua ugonjwa wa wasiwasi huanza kuepuka kukaa katika maeneo au vitu vyote ambavyo huwasababishia kukumbwa na hali hiyo.

“Kwa mfano utakuta mtu anakwepa kukaa au kusimama mbele ya kundi la watu, kupanda lifti, kupanda gari, ndege na vitu vingine vingi vinavyomsababishia hali ya wasiwasi,” anasema.

Anaongeza “Kuna tabia fulani tunaziita za kiusalama, kwamba mtu anaona ili awe salama ni vema aepuke mazingira yote yanayoweza kumsababishia kupata wasiwasi.

Si rahisi kugundua tatizo

Anasema kwa sababu suala hilo linalohusisha mwitikio au mabadiliko ya kimwili wengi hudhani wanakabiliwa na tatizo la pumu (athima).

“Wengine hudhani wanasumbuliwa na shinikizo la damu, wanakwenda hospitalini lakini wakitibiwa hawaponi kwa sababu si ‘pressure’ ya kawaida,” anasema.
http://pic.pimg.tw/mulicia/1342404351-3402839975.jpg
Kundi linaloathirika zaidi

Anasema ni vijana, ambao kawaida huwa wamefunzwa mambo mengi kipindi cha utotoni na uishi kwa kuamini katika kile walichofundishwa.

“Tatizo lina vyanzo vingi, jinsi tunavyokuwa tumelelewa, kwa mfano walizoea kukutishia tishia, unajikuta unakuwa mtu mwenye wasiwasi kila wakati tangu ukiwa mtoto.

“Lakini wakati mwingine kuna malezi ambayo yanatuweka katika mazingira ambayo ni ya kuogopa kila wakati, kwa mfano mtu anayeogopa mende ukimuuliza kwanini anamuogopa mende wengi huwa hawana majibu ya kujitosheleza,” anasema.https://www.ohsu.edu/xd/education/schools/school-of-medicine/departments/clinical-departments/surgery/residency-and-fellowships/general-surgery-programs/images/20141029_092850-small-main-hospital-entrance.jpg

Tiba

Anasema wagonjwa wa wasiwasi hupewa matibabu ya kibaiolojia ambapo hupewa dawa zinazowasaidia kurejea katika hali yao ya kawaida wanapopatwa na wasiwasi.

“Kuna tiba za kisaikolojia pia, kwa mfano mtu alipata tukio fulani likamjengea hali ya wasiwasi, tiba hizi huwa zinatusaidia kumfanya mtu arejee katika hali yake ya kawaida,” anasema.

*Makala haya kwa mara ya kwanza imechapishwa katika gazeti la MTANZANIA Mei 4, mwaka huu

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement