Picha na mtandao
Na Veronica Romwald – Dar es Salaam
MSIMAMO wa serikali ya awamu ya tano wa kupiga marufuku
wasichana wanaobeba ujauzito wakiwa shule ya msingi na sekondari kurejea
shuleni baada ya kujifungua.
Rais John Magufuli alitangaza marufuku hiyo hivi
karibuni akiwa Chalinze mkoani Pwani.
Alinukuliwa “katika utawala wake wasichana watakaobeba
mimba wakiwa shuleni hawataruhusiwa kurudi katika mfumo rasmi hata baada ya
kujifungua.
“Labda waende kwenye mfumo usio rasmi kwa mfano huko
kwenye vyuo vya ufundi stadi ikiwamo VETA na kwingineko,” alinukuliwa akisema.
Alisisitiza mwanamume ambaye
atapatikana na hatia ya kumpachika mimba mtoto wa shule, atafungwa jela miaka
30 na kutumia nguvu alizotumia kumpachika mimba msichana huyo, kufanya kilimo
akiwa gerezani.
"Mashirika
haya yasiyo ya serikali yanastahili kuenda kufungua shule kwa wazazi, lakini
hayastahili kuilazimisha serikali kuwarejesha shuleni. Ninatoa elimu ya bure
kwa wanafunzi ambao wameamua kusoma, na sasa mnataka niwaelimishe
wazazi," alihoji.
Msimamo huo wa serikali ulipokelewa kwa mitizamo miwili
tofauti kwenye jamii, wapo ambao wanaunga mkono suala hilo na wapo ambao
wanapinga hasa mashirika yasiyo ya kiserikali.
Wasemavyo wazazi
Maimuna Ally mkazi wa Mbezi Luis jijini Dar es Salaam
anasema anaunga mkono msimamo huo uliotolewa na serikali kwamba wasichana
walijiachia mno na kuendekeza mapenzi badala ya masomo.
“Wengi waliona hakuna umuhimu wa masomo, binafsi
nimeshaongea mno na wanangu lakini hawasikii na wala walikuwa hawataki
kubadilika, kwa amri hiyo ya Rais Magufuli naamini watabadilika na kurejea
kwenye mstari,” anasema.
Wakati Maimuna akikubaliana na msimamo huo, Juma Karim
mkazi wa Sinza Kijiweni anaupinga huku akisema kwamba una mkandamiza mtoto wa
kike.
“Unajua si wote wanaobeba ujauzito wanakuwa wamependa,
kuna ambao wanabakwa au wanashawishiwa na wanaume ‘wakware’ mwisho wa siku kwa
kuwa jamii nayo ipo kimya na haipendi kueleza watoto ukweli wanajikuta wamepata
ujauzito,” anasema.
Anaongeza “Nakubali wapo ambao wanajihusisha na
mahusiano ya kimapenzi wakiwa shuleni kwa kupenda wenyewe, lakini naona wengi
huwa ni kwa kushawishiwa na wengine kwa kubakwa.
Anasema kutokana na hali hiyo serikali ilipaswa
kuangalia upya msimamo wake. Hata hivyo bado serikali imesisitiza juu ya
msimamo wake huo.
Hawa ni wazazi hao ambao wanawakilisha mawazo ya wazazi
walio wengi katika jamii, lakini pamoja na yote hayo lazima kila mmoja wetu
ajiulize swali la msingi kwamba je, hatima ya mtoto wa kike ipo mikononi mwa
nani.
Wahenga
na malezi
Upo msemo wa wahenga usemao, kuzaa si kazi, kazi kule
mwana. Kwamba ni rahisi kulea mtoto akiwa tumboni mwa mama lakini ni kazi
kumlea akiwa tayari amezaliwa.
Mzee Mussa Faustine (78) Mkazi wa Manzese, jijini hapa
anasema kwa kawaida mtoto akiwa tumboni hitaji lake kuwa huwa ni chakula cha
kutosha kutoka kwa mama yake ili aumbike vema.
“Mtoto akizaliwa katika mwaka sifuri hadi miaka 18
mbali na chakula bora mahitaji yake huongezeka, huhitaji kupata haki zake za
msingi kuanzia kula, malazi, elimu, afya bora, ulinzi wa kutosha na malezi bora
kutoka kwa wazazi na jamii nzima iliyomzunguka,” anasema.
Changamoto
Hata hivyo, ingawa inasisitizwa kwamba watoto wote wana
haki sawa bado kuna changamoto nyingi zinazomkabili mtoto wa kiume.
Kwa muda mrefu kumekuwapo mila na desturi ambazo
zinamkandamiza mtoto wa kike hali ambayo imekuwa ikimfanya akose haki zake
nyingi za msingi hasa ya kusoma.
Mtoto wa kiume anapozaliwa kwenye jamii anaonekana bora
zaidi kuliko wa kike.
Kwa mfano yapo baadhi ya makabila ambayo yanaona mtoto
wa kike hastahili kabisa kwenda shule badala yake yeye ni wa kusubiri kuolewa
kwenda kuitunza familia yake.
Ofisa wa Mradi wa Shirika lisilo la Kiserikali la African
Youth and Adolesence Network on Population and Development (Afriyan), Jennifer
Kayombo akizungumza na mwandishi wa makala haya hivi karibuni
Mtizamo
wa kijana
Ofisa wa Mradi huyo anasema bado jamii inahitaji kupatiwa elimu ya kutosha ili kuondokana
na mila na desturi zinazoendelea kumkandamiza mtoto wa kike.
“Serikali imetangaza msimamo wake, lakini binafsi naona
nguvu kubwa sasa inapaswa kuwekezwa kwenye kupeleka elimu kwa jamii kuachana na
mila na desturi zinazomkandamiza mtoto wa kike,” anasema.
Anasema mtoto wa kike anastahili kupata haki ya elimu
kama ilivyo kwa mtoto wa kiume na kwamba ili kumkomboa kutokana na changamoto
ya ndoa na mimba za utotoni anapaswa kuopatiwa elimu sahihi ya afya ya uzazi.
“Elimu hiyo itolewe kwa vijana wote bila kuwabagua,
vijana wakijitambua naamini kabisa ndoa na mimba za utotoni zitapungua kama si
kuisha kabisa na hivyo wasichana watapata nafasi ya kusoma na kumaliza masomo
yao wakiwa kwenye mfumo rasmi,” anasema.
Anaongeza “Vijana lazima wapatiwe elimu ya afya ya
uzazi, wajitambue, ni muhimu mno kwani kundi hili takwimu zinaonesha ni zaidi
ya asilimia 60 ya watanzania wote waliopo nchini, na elimu pekee ndiyo ambayo
itawakomboa.
“Tumegundua jamii bado inaishi kwa kuamini mila na
desturi ambazo kimsingi zinamkandamiza kijana hasa msichana. Familia nyingi
hazimpi msichana fursa ya kutoa maamuzi (hana sauti kwenye familia),” anasema.
Mfano
wa Singida
Ofisa Mradi huyo wa Afriyan anasema shirika hilo
limewahi kwenda kutembelea kijiji kimoja huko mkoani Singida ambapo walikutana
na dada mwenye umri wa miaka 17 ambaye alikuwa tayari amezalishwa watoto
wawili.
“Dada huyo alilazimika kuacha shule kutokana na kubeba
ujauzito, tulimuuliza maswali mbalimbali jambo lililotusikitisha alitueleza
hakupata elimu kabla juu ya madhara yatokanayo na kujamiiana.
“Dada huyo alitueleza kwamba alianza kujamiiana akiwa
darasa la tatu, alitueleza hakuwa amepata kujifunza elimu ya afya ya uzazi hapo
kwanza, hivyo hakuwa anajua kuna kupata mimba, alijikuta tayari ni mjamzito na
hakuweza tena kuendelea na shule hadi leo yupo nyumbani akilea watoto wake
hao,” anasema.
Kauli ya Waziri
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto, Ummy Mwalimu (pichani) anasema Wizara imejipanga kuendelea kuelimisha wazazi
kuzingatia malezi ya watoto wao.
“Rais Magufuli ametoa msimamo wa serikali, mimi amenipa
dhamana ya kusimamia sera ya maendeleo ya mtoto na ninamsaidia kusimamia katika
masuala ya afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto.
“Si kwamba wasichana wanaopata ujauzito hawatasoma,
watasoma lakini si kwenye mfumo rasmi bali mfumo usio rasmi labda Veta na
ufugaji,” anasema.
Anaongeza “Hivyo kwa sababu tuna dhamana hii ya kusimamia maendeleo ya watoto wakike na wakiume
nguvu kubwa sasa ni kuendelea kuwahimiza na kuwashawishi wazazi kutimiza wajibu
wao kikamilifu katika malezi ya watoto.
“Wazazi wengi wapo ‘bize’ kutafuta fedha… kwa hiyo Idara
yake ya Maendeleo ya Jamii, tutaendelea kuwahimiza wakumbuke wajibu wao, aidha
tutaendelea kuwahamasisha vijana (wasichana) kuzingatia masomo,” anasema.
Kampeni
maalumu
“Tunataka mtoto wa kike azingatie elimu badala ya mambo
mengine, rai yangu kwa mashirika yasiyo ya serikali, twendeni kwenye kila
kijiji na kila mtaa tumwambie mtoto wa kike, tunataka kila mmoja aseme sishabii
mapenzi, elimu ndiyo mpango mzima,” anasema.
Anaongeza “Tutawajengea uwezo watoto wa kike,
tutaimarisha elimu ya afya ya uzazi katika shule za msingi na sekondari.
Anasema lengo ni kupunguza idadi ya wasichana ambao
wanapata ujauzito wakiwa katika umri mdogo kabla ya miaka 18.
“Takwimu zinaonesha katika kila wasichana 100, wenye
umri wa chini ya miaka 18 nchini wasicaha 27 wanapata ujauzito, tunataka
kumfikia kila msichana katika kila mtaa na kila kijiji ajitambue ili aweze
kuzingatia masomo badala ya mambo mengine,” anasema.
Anaongeza “Endapo mtoto anabakwa kazi yetu (Wizara) ni
kuhakikisha wabakaji wanafikishwa kwenye vyombo vya dola, ni vema jamii, wazazi
na walezi watoe ushirikiano tafiti zinaonesha watoto wanabakwa na watu wa
karibu yetu.
Chapisha Maoni