Mara nyingi watoto wenye tatizo hili, huwa waharibifu na hawapendi kujifunza, Picha na Mtandano
NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM
TANGU mimba inapotungwa tumboni mwa mama hadi mtoto
anazaliwa baada ya miezi tisa kipindi chote hicho mtoto huwa katika hali ya
uchangamfu.
Hiyo ni kwa sababu binadamu ameumbwa kuchangamka,
wakati wa ujauzito, mama huhisi hali hiyo ya uchangamfu wa mtoto tumboni mwake.
Mtoto akiwa tumboni mwa mama yake, mama huweza kuhisi
vema namna ambavyo mtoto husogea au kugeuka kutoka upande mmoja hadi mwingine
na hata kuzunguka zunguka.
Mtaalamu wa Tiba ya Mazoezi katika Hospitali ya Taifa
Muhimbili (MNH), Rosemary Kauzeni anasema Hiyo ni hali ya kawaida ambayo hudumu
kwa kipindi chote cha ujauzito.
“Wakina mama ambao tayari wamepitia hali ya ujauzito na
kubahatika kujifungua wanaelewa vema jinsi hali hii inavyokuwa, kuna wakati
huweza kuhisi kabisa mtoto akiwa amelala upande mmoja baadae anahamia upande wa
pili au anacheza cheza tumboni,” anabainisha.
Baada
ya kuzaliwa
Mtaalamu huyo anasema kisayansi kuna uchangamfu ambao
umeainishwa unaoashiria uchangamfu wa mtoto baada ya kuzaliwa.
“Mtoto anapozaliwa anaanza kujifunza kazi mbalimbali,
kazi yake ya kwanza ambayo anajifunza ni kunyonya… hakuna mtu anayemfundisha
mtoto kunyonya hata siku moja,” anasema.
Anataja kazi zingine ambazo mtoto hujifunza mwenyewe
kuzifanya pasipo kufundishwa na mtu ni kurusha mikono na miguu yake.
“Hii ni hatua ya kwanza ya uchangamfu wa mtoto ambao
tunaouona mara tu anapozaliwa, hatua ya pili tunaouona ni uchangamfu wa lugha,”
anasema.
Anafafanua “Lugha ya mtoto mchanga ni kulia, akizaliwa
tu iwe kwa njia ya kawaida au ya upasuaji tunahitaji kuuona uchangamfu huu,
mara nyingi mtoto huwa anawasiliana kwa njia ya kilio.
Wakati
wa ukuaji
Anasema baada ya
kuzaliwa mtoto huendelea kuonesha uchangamfu wa aina mbalimbali hadi kipindi
cha miezi mitatu.
“Katika kipindi hicho mtoto huonesha uchangamfu mwingi
ambao mama huuona kadri siku zinavyozidi kusonga mbele, kwa mfano mtoto
huonesha uchangamfu wa kuzungusha macho, usikivu wake, hisia za kugusa,”
anasema.
Dk. Kauzeni (pichani) anasema jinsi mtoto anavyozidi kukua mama huona
uchangamfu wake katika kusogea hasa anapokuwa akijirusha rusha au kusogeza
miguu yake.
“Uchangamfu zaidi huonekana hasa anapofikisha wiki nne
tangu alipozaliwa, hapo mama anaweza kuona mtoto wake akianza kucheka, akisikia
sauti mbalimbali anaweza hata kutoa hisia ya kufurahi,” anasema.
Anaongeza “Anapofikisha umri wa miezi mitatu shingo ya
mtoto hukaza vizuri zaidi, uchangamfu huendelea kubadilika badilika kadiri
anavyokua.
“Kimsingi tangu mwaka sifuri hadi miezi mitatu mtoto
huwa anacheza mwili mzima, lakini anapofikisha miezi mitatu shingo yake hukaza.
“Hapo utaona uchangamfu wake ukiwa umebakia kwenye
kiwili wili, sehemu ya tumbo na mgongo huonekana ikicheza zaidi, au utaona
mikono na miguu ikiwa haijakaza vizuri,” anasema.
Anasema hali hiyo huendelea hadi anapofikia umri wa
miezi minne na kwamba katika kipindi hicho mama huona uchangamfu wa mtoto kukaa
na au kuanza kutumia zaidi mikono yake.
“Huanza kushika vitu mbalimbali anavyoviona mbele yake,
husikilizana na watu wanaomzunguka na sauti anazozisikia, huu ni uchangamfu wa
kawaida ambao hutegemea makuzi salama,” anasema.
Anaongeza “Mtoto atakua katika hali hiyo hadi kipindi
cha miezi mitano hadi sita ambapo huanza kujivuta kusogea kutoka eneo moja hadi
jingine.
Tatizo
huanzia wapi?
Mtaalamu huyo ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Utengamao
na Tiba hospitalini hapo, anasema iwapo mtoto anakabiliwa na tatizo la haraka
nyingi huonesha uchangamfu usio wa kawaida.
“Dalili huanza kuonekana hasa katika kipindi ambacho
huanza kukaa chini au kutembea, huwa anakuwa na kasi isiyokuwa ya kawaida,”
anabainisha.
Anasema mara nyingi mtoto mwenye tatizo hilo anapowekwa
chini huanza kuvamia vitu mbalimbali anavyoviona mbele yake.
“Kutokana na hali hiyo wengi huwa ni lazima washikiliwe
na mtu, au unakuta ameanza kutembea na kasi yake huwa kubwa kuliko kawaida ya
umri wake, hapo utasikia wazazi wengi wakisema mtoto ni mtundu mno,” anasema.
Anasema huwa hawataki
kushika kitu chochote kwenye mikono yao, wakishika wanatupa hata wakipewa
maagizo hawatekelezi (hawafuati oda ya mzazi).
Anaongeza “Hata akiwa anacheza na wenzake hawezi
kufuata zile taratibu za mchezo na wenzake ili kucheza pamoja, ni vigumu
kushirikiana na wenzao ingawa wanaongea, wanatembea kama watoto wengine.
Anasema ingawa kwa hali ya kawaida tatizo hilo si
ugonjwa lakini huweza kumsababisha mtoto kupata magonjwa mbalimbali yatakayoathiri afya yake baadae
katika maisha yake.
Magonjwa
yenyewe
Mtaalamu huyo anasema mtoto mwenye tatizo hilo huwa
kwenye hatari kubwa ya kuathirika afya ya ubongo na baadae kupata magonjwa ya
akili (mood dis-order).
“Yaani anakuwa hisia zake zinabadilika badilika, mara
mwenye hasira nyingi, mara furaha, hali hiyo huweza kumpelekea ubongo wake
kuathirika na kumsababishia magonjwa ya akili,” anabainisha.
Anasema hali huweza kuwa mbaya zaidi na hata kupeleka
mtoto kupata ugonjwa wa kifafa baadae.
Anasema kutokana na hali hiyo hulazimu wazazi, ndugu au
familia kutumia muda na akili yao yote kumwangalia mtoto kwa umakini mkubwa.
Daktari huyo akionesha baadhi ya vifaa wanavyotumia kuwatibu watoto wenye tatizo la haraka nyingi
Matendo
yasiyo ya kibinadamu
Anasema kwa kawaida mtoto anapokuwa hutakiwa kuonesha
matendo ya kibinadamu lakini yule mwenye tatizo huonesha matendo yasiyo ya
kibinadamu.
“Mtoto anapokuwa na umri wa mwaka mmoja huwa anachezea
au kuunganisha vitu mbalimbali unavyompatia lakini mtoto mwenye tatizo hili
kamwe hawezi kutulia na kuchezea vitu unavyompatia.
“Utaona chochote unachompatia anakitupa ovyo, maana
yake ni kwamba anakuwa haoneshi ufundi hata kidogo ambao tunautarajia. Kwa
kawaida mtoto tunarajia ajifunze kwa mfano mara nyingi mtoto wa kiume akiona
gari achukue chochote kilichopo mbele yake na kuanza kukisogeza kama gari
linavyokwenda.
“Akiwa mtoto wa kike akikaa karibu na mama au dada yake
wakati wa kupika chakula jikoni, utaona na yeye anachukua vikopo na kukaa chini
akiigiza anapika,” anasema.
Anaongeza “Mtoto mwenye haraka nyingi hana huo muda wa
kujifunza, yeye hufanya matendo ya vurugu tu, wengi wanawaita watundu ingawa si
neno zuri kulitumia.
Anasisitiza kwamba mtoto ambaye hana tatizo huonesha
ufundi wake kwani hutulia na kunuia kutazama
kile anachotaka kukitazama.
Namna
linavyotokea
Mtaalamu huyo anasema kila binadamu ana milango ya
fahamu ambapo mtoto mwenye tatizo la haraka nyingi, mara nyingi huwa anakuwa na
milango ya fahamu isiyo wiana.
“Yaani… tunatumia macho kutazama kitu na kupeleka
taarifa kwenye ubongo ambao hutafsiri kitu tunachokiangalia, ukigusa kitu
taarifa hupelekwa kwenye ubongo na wenyewe hutafsiri umegusa nini.
“Ukinusa harufu yoyote nayo ni hivyo hivyo, na mwili
nao hupeleka taarifa kwenye ubongo kwa mfano ukiwa ukitaka kupanda ngazi
unapeleka taarifa kwenye ubongo na ndipo pale unajikuta unainua mguu wako,”
anasema.
Anaongeza “Mtoto mwenye tatizo upo uwezekano mkubwa
kwamba kuna shida ya mawasiliano katika mwili wake, lakini kwa bahati mbaya hakuna
kipimo tunaweza kukitumia kubaini tatizo hili mapema, tutakachokiona ni ule
uharaka wa kupindukia kutokana na haraka ya kupindukia.
Athari
zaidi
Anasema kutokana na tatizo hilo kumekuwa na ajali
nyingi za moto kwa watoto.
“Unakuta mama ameinjika maji jikoni au ameweka chupa ya
chai mezani ghafla anakuta mtoto ameshafika, ameshavunja na tayari ameungua,”
anasema.
Anafafanua “Yaani ukimuweka chini haraka anakuwa
amevamia kitu, ni lazima ashikiliwe, katika hilo lazima uanze kuwa na wasiwasi
wa uchangamfu wa mtoto huyo.
Anasema kutokana na hali hiyo hulazimu wazazi, ndugu au
familia kutumia muda na akili yao yote kumwangalia mtoto kwa umakini mkubwa.
Hali
ipoje
Anasema ingawa bado hakuna utafiti uliofanywa kubaini
ukubwa wa tatizo hilo nchini lakini katika Idara hiyo wamekuwa wakipokea watoto
wenye tatizo hilo.
“Kwa mfano mwaka 2012 tulipokea watoto 32 katika
kipindi cha miezi mitatu ambao walikuwa wameungua moto na tulipozungumza na
wazazi wao wengi walidai watoto wao ni watundu sawa na asilimia 10 (si taarifa
rasmi),” anasema.
Anasema watoto wengi hufariki dunia kwa kutumbukia
kwenye maji, wapo ambao hushindwa kumudu masomo darasani.
“Tunapokea watoto wengi ambao wanakataliwa shuleni kwa
sababu wana tatizo hili la haraka nyingi. Hawa si ‘slow learners’… hawa ingawa wana
akili nyingi mno lakini wanashindwa kujifunza kwa sababu ubongo wao upo
haraka,” anasema.
Anasema kutokana na hali hiyo anakusudia kufanya
utafiti wa kina kuhusu tatizo hilo kwamba lipo kwa kiasi gani nchini.
Sehemu ambayo madaktari hutumia pia kuwatibu watoto wenye tatizo la haraka nyingi
Matibabu
Anasema kwa kuwa si ugonjwa ambao huonekana wazazi
wengi hubaki na watoto wao nyumbani wakidhani ni hali ya kawaida.
“Si rahisi kubaini kwa sababu saa zote mtoto huwa
‘active’ ingawa wanaweza kuonesha dalili kwa mfano kukosa usingizi, kukosa hamu
ya kula au kula chakula kingi, muda wote wenyewe hupenda kucheza,” anasema.
Anasema iwapo mtoto anakuwa tayari amepata magonjwa ya
akili na kifafa wataalamu humuanzishia dawa maalumu.
“Lakini tiba nyingine ambayo huwa wanapatiwa ni tiba
kwa njia ya vitendo. Tiba hii inatolewa na mtaalamu na mwanasayansi aliyesomea
jinsi ya kutoa matibabu hayo.
Anasema zipo tafiti nyingi ambazo zimefanywa na kueleza
jinsi gani mtaalamu anaweza kubaini milango ya fahamu ya mtoto na jinsi gani
inavyopokea taarifa na kuzituma kwenye ubongo wake kutafsiriwa.
“Kwa hiyo anaangalia je ubongo wa mtoto unapokea
taarifa sahihi na zinafika kwa kiasi gani. Hapa tunatumia vifaa mbalimbali kwa
kumgusisha kwenye mikono yake,” anasema.
Anaongeza “Tunatumia njia hiyo kwa sababu, viganja vina
mishipa midogo midogo mingi mno ambayo hupeleka taarifa na kuiwasilisha kwenye
ubongo wake.
Anasisitiza kitendo hicho hufanywa kwa kurudia rudia
pale tu tatizo linapogundulika.
“Huwa pia tunaangalia mpangilio wake wa mwili, jinsi
Mungu alivyoumba mwili umepangiliwa kama kuna tatizo mtaalamu anao uwezo wa
kubaini na kumsaidia mtoto tunaita kitaalamu (handling technique),” anasema .
Ushauri
Mtaalamu huyo anashauri wazazi kuwa karibu na watoto
wao kufuatilia mwenendo wao wa ukuaji kwani itasaidia kubaini mapema iwapo
mtoto ana tatizo hili au la.
“Ni rahisi zaidi mama kubaini, kwa sababu anao uwezo wa
kujua kilio cha mtoto kina maana gani, lakini tatizo siku hizi watoto
wanalelewa na ‘house girls’.
“Suala la malezi ni muhimu mno kwa mtotio, zamani wazee
walikuwa wanakaa na mama aliyejifungua hata siku saba kwa mfano wakimfundisha
jinsi ya kulea mtoto walijua umuhimu wake, lakini leo hii hakuna, ni tatizo”
anasema.
Makala haya kwa mara ya kwanza yamechapishwa Agosti 31, mwaka huu kwenye gazeti la MTANZANIA
Chapisha Maoni