Na Veronica Romwald, Dar es Salaam
WATOTO 15 kati 100 wanaofariki dunia nchini vifo vyao huwa
vimetokana na ugonjwa wa nimonia, imeelezwa
Nimonia unatajwa kushika nafasi ya pili kusababisha vifo
vya watoto wachanga nchini na kwamba ni miongoni mwa magonjwa yanayochangia
vifo vya watoto wachanga duniani.
Kaimu Meneja Program ya Afya ya Mtoto wa Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Felix Bundara amesema hayo hivi
karibuni katika mahojiano mahojiano maalumu na mtandao huu.
Dk Bundara amesema hiyo ni kwa mujibu wa utafiti wa Utafiti
wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Malaria Tanzania wa mwaka 2015/16 (TDS).
“Utafiti huo ulionesha wazazi na walezi hawapeleki watoto
kutibiwa pindi wanapopata kikohozi hali ambayo inawaweka kwenye hatari, kati ya
watoto 100 waliopata kikohozi 55 pekee ndiyo walifikishwa hospitalini,” amebainisha.
Amesema jamii inapaswa kuamka na kuhakikisha mtoto
anapopata tatizo la kikohozi anafikishwa mapema hospitalini kwa uchunguzi.
“Watoto 45 hawakufikishwa hospitalini, wapo ambao wamejenga
mazoezi ya kwenda kununua dawa za ‘antibiotics’ madukani na kuwapatia watoto
wanapopata kikohozi,” amesema.
Ameongeza “Si jambo sahihi, wajue kwamba si kila kikohozi
ni nimonia kitendo cha kuwapatia dawa bila ushauri wa daktari kunaweza
kusababisha kutengeneza usugu wa dawa mwilini.
Dk. Bundara amesema ingawa ugonjwa huo huwapata pia watu
wazima hata hivyo watoto wapo hatarini zaidi kupoteza maisha kwa sababu kinga
yao haipo ya kutosha.
“Ni ugonjwa ambao unaathiri mapafu unaweza kuupata kwa
kupata maambukizi ya bacteria, virusi au fangasi,” amesema.
Amesema dalili kuu ya kwanza huwa ni kukohoa na kupata
shida ya kupumua.
Amesema watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi kwa
mfano yenye moshi wa kuni, mkaa, sigara, nyumba isiyo na hewa ya kutosha wapo
hatarini zaidi kupata ugonjwa huo.
“Mtoto anapaswa kunyonya maziwa ya mama miezi sita bila
kupewa kitu chochote ile humsaidia kupata lishe, akikosa lishe anakuwa kwenye
hatari pia ya kupata ugonjwa huo,” amesema.
Amesema wazazi wanapaswa kuwawahisha hospitalini watoto ili
wapate matibabu sahihi na si kwenda kuwakata kimeo.
“Huko wanapoteza damu nyingi na hivyo kufariki dunia,
serikali inafanya jitihada nyingi na tunatoa chanjo katika kila kituo chenye
huduma ya afya ya mama na mtoto, wawalete wafanyiwe uchunguzi,” ametoa rai.
Chapisha Maoni