Alhamisi, 21 Desemba 2017

KIBUYU CHIRIZI KINAVYOTUMIKA KUKABILI MAGONJWA YATOKANAYO NA HALI YA UCHAFU

Mmoja wa Wanafunzi wa Shule ya Msingi Humekwa iliyopo kijiji cha Humekwa Wilaya ya Chamwino akinawa mikono kwa kutumia sabuni na maji ya kibuyu chirizi (Picha kwa hisani ya Blogu rasmi ya serikali

Na Veronica Romwald, Aliyekuwa Dodoma

NI mwendo wa zaidi ya saa mbili kwa kutumia usafiri wa gari kutoka katikati ya mji wa Dodoma hadi kufika katika Kijiji cha Humekwa.

Kijiji cha Humekwa ni miongoni mwa vijiji vilivyopo katika Tarafa ya Itiso, Kata ya Haneti, Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma.

Kina jumla ya vitongoji vitano ambavyo ni Visimani chenye Kaya 77, Miembeni Kaya 108, Chibefu Kaya 69, Robaito Kaya 58 na Mkola chenye Kaya 39.

Desemba 6, mwaka huu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu akiwa ameambatana na waandishi wa habari alikitembelea kijiji hicho kuwapongeza kwa hatua waliyofikia.

Hatua ipi?

Kijiji hicho kimekuwa cha mfano katika utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mradi wa Kampeni ya Taifa ya Usafi wa Mazingira.

Kampeni hiyo inatekelezwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, awamu hiyo ya kwanza ilizinduliwa 2012 na kuhitimika 2016.

Katika awamu hiyo ya kwanza ya kampeni hiyo, Wizara ililenga kuhamasisha jamii kuzingatia ujenzi wa vyoo bora na kunawa mikono baada ya kutoka chooni.

Kabla ya kuanza utekelezaji wa mradi huo katika kijiji hicho hali ya usafi wa mazingira haikuwa nzuri kiasi cha wananchi kuugua magonjwa ya matumbo mara kwa mara.

Akisoma risala kwa niaba ya Ofisa Mtendaji wa Kijiji hicho Ashery Myogoya, mbele ya Waziri huyo, Eveline Gidole mbele ya Waziri Ummy Mwalimu, anasema kijiji hicho kina jumla ya kaya 349 zenye jumla ya watu 1,657 kati yao wanaume ni 746 na wanawake 911.

“Tuna zahanati moja ya serikali, Shule moja ya serikali, makanisa saba ya madhehebu mbalimbali, mashine tatu za kusaga, mashine moja inayosukuma maji kuleta kijijini, maduka sita, migahawa minne ya kuuza Chakula na glossary moja,” anabainisha.

Anasema kabla ya utekelezaji wa mradi wa usafi wa mazingira kupitia kampeni hiyo ya Taifa, hali ya usafi wa mazingira katika kijiji hicho ilikuwa mbaya.
 
WAZIRI wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na watoto Mhe. Ummy Mwalimu pamoja na Mwakilishi wa shirika la DFID nchini Tanzania Elizabeth Arthur wakiangalia  namna Kibuyu Chilizi kinavyosaidia kuepukana na magonjwa ya matumbo,kuhara pamoja na kipindupindu.

Hali halisi

Anasema kutokana na wakazi wa kijiji hicho kutokuwa na vyoo bora walikuwa wakiugua magonjwa yatokanayo na hali ya uchafu wa mazingira ikiwamo typhoid na minyoo kila mara.
Eveline anasema Machi, 2016 kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo walianza kutekeleza Kampeni ya Usafi wa Mazingira Tanzania katika kijiji hicho.

“Tulishirikiana na wenzetu wa Shirika la Plan International kupitia mradi wake wa Usafi wa Mazingira Tanzania (UMATA) kuielimisha jamii juu ya umuhimu wa ujenzi na matumizi ya vyoo bora pamoja na kuzingatia kunawa mikono baada ya kutoka chooni,” anasema.

Anasema katika utekelezaji huo walibaini uwepo wa Kaya 189 ambazo hazikuwa na vyoo kabisa, sawa na asilimia 54, Kaya 158 walikuwa wakitumia vyoo vya asili na Kaya mbili zilikuwa na vyoo vya bomba.

Anasema walibaini nyumba moja ya mwalimu wa Shule ya Msingi Humekwa haikuwa na choo kabisa na kwamba katika kaya zote 349, kaya mbili pekee ndizo ambazo zilikuwa na sehemu ya kunawa mikono (kibuyu chirizi).

“Kaya 347 hazikuwa zinanawa mikono kabisa…sambamba na kutokuwa na vyoo, hali ya Usafi katika kijiji ilikuwa mbaya kwani Kaya nyingi kutokuwa na vyoo kabisa,” anasema.
 
Baadhi ya wanakijiji cha Humekwa wilayani Chamwino,wakifuatilia yaliyokuwa yakijiri kwenye mkutano huo wa hadhara,ambapo mgeni rasmi alikuwa WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto Mhe. Ummy Mwalimu ambaye amefika katika kijiji hicho kukagua Usafi wa Mazingira na Vyoo bora kuelekea uzinduzi wa awamu ya pili ya kampeni ya Taifa ya usafi wa Mazingira. 

Kibuyu chirizi ni nini?

Mussa Masumbuko ni mkazi wa kijiji hicho anasema ni mbinu ya asili ambayo wanaitumia katika kunawa mikono pindi wanapotoka chooni.

“Unaweza kusema ni ‘teknolojia’ ya asili, ukiangalia vizuri utaona katika kila choo eneo la nje kumejengwa kichanja maalum ambacho kimening’inizwa kidumu cha maji cha lita tatu au tano kilichozibwa na gunzi na pembeni yake kuna kikopo cha maji ya sabuni,” anasema.

Anasema pindi mtu anapotoka chooni huenda kwenye kichanja hicho na kunawa mikono yake vema kabla ya kwenda kuendelea na shughuli zingine.

“Kwanza utachukua sabuni kidogo kutoka kwenye kile kikopo, ili uweze kunawa nay ale maji yaliyopo kwenye kidumu utalazimika kukanyaga mti ambao umewekwa chini ukiwa umeunganishwa na kamba.

“Pindi unapokanyaga fimbo hiyo, ile kamba iliyounganishwa kwenye kidumu itavutia na hivyo kuwezesha kidumu kuinama na maji kutiririka, utanawa hadi unapohakikisha mikono yako imekuwa safi,” anasema.

Mafanikio

Eveline (Pichani) anasema ujenzi wa vyoo bora na matumizi ya kibuyu chirizi yamesaidia kwa kiasi kikubwa kijiji hicho kukabilina na maambukizi ya magonjwa yatokanayo na hali ya uchafu.

“Tumeweza kupunguza idadi ya wagonjwa wanaotokana na athari za hali ya uchafu wa mazingira, kutoka wagonjwa 138 Desemba, 2015 hadi kufikia 26 Novemba, 2017 sawa na asilimia 82,” anasema.

Anasema takwimu hizi ni kwa mujibu wa taarifa ya kila robo mwaka inazotolewa na Kitengo Cha Afya katika Zahanati ya Humekwa katika kitabu cha mtuha namba tano cha wagonjwa wanaohudhuria kila siku.

Ilichukua muda

Emmanuel Mzungu ni Mwenyekiti wa serikali ya kijiji hicho anasema haikuwa rahisi kufikia mafanikio hayo na kwamba walipitia changamoto mbalimbali.

“Kijiji chetu kulikuwa kichafu kabla ya kutekelezwa kwa mradi huu, changamoto kubwa tuliyokabiliana nayo ni jinsi ya kubadili mtizamo wa jamii ambao walikuwa nao awali juu ya matumizi ya vyoo.

“Tulishirikiana na wadau wa maendeleo kupeleka elimu hiyo kwa kila namna na mwisho tulifanikiwa, jamii ikapokea elimu ile na kutekeleza,” anasema.

Anawashukuru wadau wa maendeleo waliojitolea kila kukicha kuwaelimisha wakazi wa kijiji hicho juu ya umuhimu wa matumizi ya vyoo na kunawa mikono baada ya kutoka chooni.

“Uamuzi tuliochukua na utekelezaji wa elimu tuliyopewa leo hii imefanya kijiji chetu kuwa safi, wadau wa maendeleo na watumishi wa afya wamefanya kazi kubwa kufikisha elimu hii ya usafi wa mazingira, leo tunaona matunda yake,” anasema.

Kuhusu tuzo

Anaongeza “Nashukuru Waziri Ummy amesema katika awamu nyingine watakapotoa tuzo kwa vijiji vilivyofanya vizuri na chetu kitakuwepo, nimefurahi mno kusikia hivyo.

“Ikiwa tutapewa tuzo hiyo, itasaidia wananchi wangu kuendelea kujituma zaidi katika utunzaji wa mazingira kwa ujumla na itahamasisha wenzetu waliopo katika vijiji vingine ambao bado hawajachukua hatua kuiga mfano bora kutoka kwetu,” anasema.
Hali ilivyo duniani

Shirika la Afya Duniani (WHO) linaeleza hali ya uchafu wa mazingira ni chanzo kikuu cha magonjwa mengi ya kuambukiza hasa ya kuhara na kipindupindu.

WHO linakadiria kila mwaka watu bilioni 1.7 huugua magonjwa ya kuhara duniani na watu milioni 1.8 hufariki kila mwaka duniani kutokana na magonjwa hayo.

Idadi hiyo ni sawa na wastani wa vifo vinne kila dakika, kwamba hali hiyo huchangiwa zaidi na  ukosefu wa vyoo bora.

Kwa mujibu wa Shirika hilo watu bilioni 2.3 sawa na theluthi ya watu wote duniani hawatumii vyoo bora na watu milioni 892 hawana kabisa vyoo bora.
Mwakilishi wa shirika la DFID nchini Tanzania Elizabeth Arthur,ambaopia ni baadhi ya Wafadhiri wa Mazingira na Usafi katika sehemu mbalimbali hapa nchini,akiwasalimia baadhi wa wanakijiji cha Humekwa wilayani Chamwino

Hali ilivyo nchini

WHO linaeleza asilimia 70 ya wakazi waishio katika Bara la Afrika hasa Kusini mwa Jangwa la Sahara, Tanzania ikiwamo hawana kabisa vyoo bora.

Takwimu zinaeleza asilimia 40.5 ya kaya zote Tanzania ndizo zenye vyoo bora huku Kaya 600,000 zenyewe hazina vyoo bora.

Inakadiriwa pia, kila mwaka watu 30,000 huugua magonjwa ya kuhara nchini hiyo ikiwa ni sawa na asilimia 83 ya wagonjwa wote wanaolazwa kila siku hospitalini.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu anafafanua kwamba katika kila wagonjwa 100 wanaofika katika vitengo vya wagonjwa wa nje hospitalini (OPD) kwa siku, wagonjwa 60 huwa ni wale wanaougua magonjwa yatokanayo na hali ya uchafu.

“Takwimu zinaonesha ugonjwa wa kipindupindu ambao upo katika kundi la magonjwa yatokanayo na uchafu umeendelea kuitesa jamii tangu uliporipotiwa kuwapo nchini mwaka 2015,” anasema.

Anaongeza “Tangu kipindi hicho hadi kufikia Novemba 12, 2017 watu 27,554 wameripotiwa kuugua ugonjwa huo na 432 wakiripotiwa kupoteza maisha.

“Lakini magonjwa haya tunaweza kuyakabili kwa kuzingatia usafi wa mazingira hasa matumizi ya vyoo bora na kunawa mikono pindi tunapotoka chooni,” anasema.

Anasema takwimu zinaonesha hali ya unawaji mikono nchini si nzuri nchini hasa baada ya kutoka chooni ambapo asilimia 12 pekee ya watanzania ndiyo ambao huzingatia suala hilo.

“Wengi hawanawi ni tabia iliyojengeka, tunahitaji kuielimisha jamii iendelee kutambua umuhimu wa suala hilo na ndiyo maana tumezindua awamu ya pili ya Kampeni ya Taifa ya Usafi wa Mazingira,” anasema.
Nguvu zaidi

Waziri Ummy (anayezungumza pichani) anasema serikali itahakikisha wananchi hasa wa vijiji wanapata huduma bora za afya na kuendelea kupatiwa elimu ya umuhimu wa matumizi ya vyoo bora na unawaji mikono baada ya kutoka chooni.

“Kwa mfano, Wilaya ya Chamwino kabla ya serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais John Magufuli bajeti ya afya ilikuwa ni Sh milioni 113, mwaka jana imepatiwa Sh milioni 436 na imetengewa tena kiasi cha Sh milioni 505,” anabainisha.

Anaongeza “Kwa mazingira ya kijijini kwa mfano hapa Dodoma mwananchi hahitaji kuwa na fedha nyingi kujenga choo bora, nimezungumza na mmoja wao amenieleza ametumia kiasi cha Sh 50,500 na amejenga choo bora.

“Tafiti zinaonesha kila mwaka binadamu asiye na choo bora hutumia saa 58 kutafuta mahala pa kujisitiri, sasa tunazungumzia Tanzania ya viwanda basi ni pamoja na kuwa na choo bora.

“Ukiwa na choo bora maana yake ni kwamba utaokoa muda huo ambao unaweza kuupoteza ambao utautumia katika kufanya shughuli za maendeleo yako kiuchumi, kijamii na Taifa kwa ujumla na utakuwa umejiepusha na uwezekano wa kupata magonjwa yatokanayo na hali ya uchafu,” anasema.

Makala haya kwa mara ya kwanza yametoka Desemba 21, 2017 katika gazeti la MTANZANIA ambalo nalitumikia (Picha kwa hisani ya Blogu rasmi ya serikali)