Mbu aina zote hueneza ugonjwa wa matende na mabusha.
Na Veronica Romwald, Dar es Salaam
WENGI wetu tunajua kwamba busha ni hali inayowapata
wanaume pekee ambayo husababisha kuvimba
kwa maumbile yao katika sehemu za siri.
Miaka ya nyuma, jamii nyingi hasa zile zinazoishi katika
maeneo ya Pwani ziliwapa heshima kubwa watu waliokuwa na hali hiyo.
Huwaita Mamwinyi mara nyingi huwa wakivaa vazi maalumu liitwalo msuli na kila
walipotembea hushika fimbo maaalum mkononi mwao iliyowawezesha kutembea kutoka
eneo moja hadi jingine.
Jamii iliwaogopa pia watu waliokuwa na hali hiyo kwani
wengi wakihusishwa na imani za kishirikina kwamba wana nguvu za kipekee
zinazoweza kumdhuru au kumwadhibu mtu yeyote anayekwenda kinyume na matakwa
yao.
Hatukujua kuwa hali ile ni ugonjwa ambao huweza
kumsabishia mwanaume kukosa nguvu za kushiriki tendo la ndoa kikamilifu na hata
kumsababishia ugumba au utasa kabisa.
Hali huwa mbaya zaidi pindi anapochelewa kwenda
hospitalini kufanyiwa uchunguzi kisha upasuaji kutibu tatizo, wengi walikuwa
wakijificha majumbani.
“Hiyo ni changamoto kubwa ambayo tumekabiliana nayo
kwa muda mrefu katika mapambano dhidi ya ugonjwa huu, wengi wanaogopa
kujitokeza hasa wanawake,” anasema Kaimu Meneja Mpango wa Taifa Magonjwa
yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele, Oscar Kaitaba (pichani chini).
MTANZANIA / matukionamaisha limezungumza kwa kina na Kaitaba juu ya
ugonjwa huo, namna unavyoambukizwa na nini hasa husababisha mtu kupata hali
hiyo.
Anasema ugonjwa huo hutokana na minyoo iitwayo
kitaalamu….. ambayo huenezwa na mbu kutoka kwa mtu mwenye ugonjwa hadi kwa mtu
ambaye hana ugonjwa huo.
“Mbu hunyonya damu kwa mtu ili kurutubisha mayai
yake sasa inapotokea amemng’ata mtu mwenye minyoo hiyo huibeba na ikiwa
atamng’ata yule ambaye hana minyoo hiyo basi humwambukiza,” anasema.
Anasema ikiwa minyoo hiyo inapoingia kwenye mwili
wa binadamu itakwenda kuziba mirija ya mfumo wa damu iliyopo katika maeneo
mengine ya mwili kwa mfano miguuni basi hapo huitwa tende.
“Lakini minyoo ile ile ikiwa itakwenda kuziba
mirija ya mfumo wa damu iliyopo katika sehemu za siri basi hapo huitwa busha,
hivyo huu ni ugonjwa aina moja ambao unatokana na minyoo ambayo husambazwa na
mbu,” anabainisha.
Anasema maeneo ya Pwani yanaonekana kuathirika
zaidi na ugonjwa huo kuliko mengine kwani huko mbu huzaliana kwa wingi zaidi.
“Na kadiri mtu anavyoumwa na mbu wengi ndivyo
anavyokuwa kweneye uwezekano mkubwa zaidi wa kupata ugonjwa huu kuliko
wengine,” anasema.
Maji
ya dafu
Kaitaba anasema si kweli kwamba maji ya dafu huweza
kumsababishia mtu kupata ugonjwa huo kama ambavyo wengi wamekuwa wakidai.
“Maji ya dafu yanahusianishwa tu na tatizo hili
lakini ukweli ni kwamba maeneo ya Pwani nazi ni zao lao la kibiashara.
“Sasa unakuta watu wanakula madafu kisha wanatupa
ovyo vile vifuu, kumbuka awali nimesema kwamba minyoo inayosababisha tatizo hili.
“Kwa hiyo wanapotupa vile vifuu ikitokea mvua ikanyesha
vile vifuu vikajaa maji basi mbu huzaliana kwa wingi na hivyo kuongeza ule
uwezekano wa watu kupata maambukizi,” anasema.
Anaongeza “Kwa hiyo si kweli kwamba ile ni ishara
ya ukuu (umwinyi), wanajifariji tu na wala wasihusianishe na nguvu za
kishirikiana watu wanapaswa kuelewa kwamba ule ni ugonjwa unaosababishwa na
minyoo.
“Wajue ni tatizo la kiafya na linalohitaji matibabu
ya haraka ili kukabiliana nalo ikiwa tayari mtu amepata zile athari za kuvimba
(maji na manyanyama) katika sehemu zake za siri.
Dalili
Kaimu Meneja huyo anasema kwa kawaida dalili za
ugonjwa huo huanza kujitokeza miaka mitatu baadae tangu mtu alipoambukizwa.
“Dalili hizo ni pamoja na kupata homa za mara kwa
mara, maumivu na kuvimba mitoki, miguu kuwaka moto, maumivu ya kichwa na
mengine mengi,” anabainisha.
Wanawake
Anasema miaka ya nyuma wengi walijua tatizo hilo
huwapata wanaume pekee lakini si kweli.
“Linawapata pia wanawake lakini wengi huwa
hawajitokezi na nadhani kwa sababu zamani kwa mfano walikuwa wakijifungua kwa
wakunga wa jadi ilikuwa rahisi kwao kujificha.
“Lakini leo hii wanakuja hospitalini na wakunga
wanapowagundua huwapatia ushauri nasaha na kuwahimiza waanze matibabu mara
moja,” anabainisha.
Inakuwaje
Kaitaba anasema wakati wanaume huwa wanavimba
sehemu wanawake hupata pia uvimbe katika sehemu zao za siri hasa eneo la
mashavu ya uke.
“Huwa yanavimba kiasi cha kuziba kabisa eneo lote
la uke na wakati mwingine uvimbe unapozidi huweza kuziba ile njia ya mkojo na
hivyo kusababisha kupata mkojo kwa kiwango kidogo mno,” anabainisha.
Anaongeza “Ikiwa mwanamke hupata maumivu kutokana
na hali hiyo na kwamba ikiwa hatakwenda mapema hospitalini kutibiwa huweza
kujikuta mwili wake hukitoa harufu mbaya.
“Lakini kama nilivyosema awali wanawake si wengi
wanaojitokeza kama ambavyo wanaume wanagundulika na kujitokeza, hadi sasa
nafahamu wanawake watatu ambao wamejitokeza na kutibiwa.
“Mmoja makazi yake ni huko Mkuranga mkoani Pwani,
kuna ambaye anaishi Mororogo na mwingine yupo Muheza mkoani Tanga,” anasema.
Hofu
Anasema watu wengi wenye tatizo hilo huogopa
kujitokeza kufanyiwa upasuaji kwa hofu ya kufariki dunia wakati wakipatiwa
matibabu hayo.
“Hofu hiyo imejenga tangu zamani, unajua wakati ule
teknolojia ilikuwa haijakuwa kama ilivyo sasa, mtu aliyehitaji upasuaji
alilazimika kuchomwa sindano ya ganzi mwili mzima.
“Sasa unakuta watu wengi waliokuwa na tatizo
walikuwa na umri mkubwa walipopewa ganzi kuna baadhi yao walijikuta wakipata
tatizo la shinikizo la juu la damu na hivyo kupoteza maisha.
“Lakini leo hii mambo yamebadilika, teknolojia
imekuwa kwa kiwango cha hali ya juu sana, siku hizi tunapomfanyia mtu upasuaji
hatuhitaji tena kumpa ganzi mwili mzima.
“Tunachofanya tunachoma ganzi katika eneo
tunalohitaji kufanya upasuaji na mtu anaweza kushuhudia kila tunachofanya
katika mwili wake na tunapomaliza ikiwa ulikwenda vizuri basi anaweza
kuruhusiwa kurudi nyumbani kwake hata baada ya saa mbili tangu upasuaji
kumalizika,” anasema.
Anaongeza “Tena anakwenda nyumbani kwake akitembea
bila kusaidiwa na mtu yeyote akiwa amepona kabisa tatizo lililokuwa
linamsumbua.
Anasema kutokana na mafanikio hayo sasa jamii
imekuwa na mwamko mkubwa wa kujitokeza kufanya uchunguzi na kisha kufanyiwa
upasuaji kutibu tatizo hilo.
“Ingawa bado kuna maeneo machache kwa mfano Tanga
kuna changamoto kidogo mwamko si mzuri kama ilivyo kwa maeneo mengine ya Pwani
kama Mtwara na Lindia,” anabainisha.
Anasema wanaume wengi wanaowafanyia upasuaji huo
huwa wanawatoa uvimbe wenye kilo zipatazo 20 hadi 30 na kwamba kama haukuathiri
zaidi basi huweza kushiriki tendo la ndoa kama kawaida na mwezi wake.
“Kuna kipindi nakumbuka tuliwahi kumfanyia upasuaji
mwanamume mmoja pale Hospitali ya Taifa Muhimbili alikuwa na uvimbe ambao
ulikuwa na kilo 60, ni hatari kubwa.
“Kutokana na kuongezeka huko kwa uvimbe ikiwa
mwanaume atachelewa kufanyiwa upasuaji basi huweza kumsababishia tatizo la
nguvu za kiume na au korodani zake kuoza,” anasema.
Anaongeza “Hivyo ikiwa korodani zake zitaoza basi
tutalazimika kumfanyia upasuaji kuziondoa lakini kama zitakuwa salama basi
tunaondoa tu ule uvimbe na anakuwa na uwezo wa kushiriki na kuzalisha kama
kawaida.
Chapisha Maoni