Alhamisi, 11 Januari 2018

DK. TULIA ATIMIZA AHADI YAKE KWA JKCI

Dk. Tulia (mwenye miwani),Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa Watoto wa JKCI, Sulende Kubhoja, Mkurugenzi wa DSTV Maharage Chande(mwenye koti na tai) na Kaimu Mkurugenzi Idara ya Utawala na Fedha, Agnes Kuhenga wakionesha waandishi wa habari moja ya televisheni ambazo zimetolewa na Taasisi ya Tulia Trust kwa ajili ya wodi za watoto JKCI.

Na Mwandishi Maalum, Dar es Salaam

Naibu spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson amekabidhi msaada wa televisheni kwa Taasisi hiyo ambazo zitafungwa katika wodi za watoto.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Dkt. Tulia alisema ametoa jumla ya televisheni sita kwa JKCI kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwamo kampuni ya DSTV.

“Kwa mara ya kwanza niliguswa kutoa msaada huu wa televisheni nilipokuja kumuona mtoto ambaye taasisi ya Tulia Trust imegharamia matibabu yake.

“Hadi sasa tumetoa jumla ya televisheni sita zenye jumla ya thamani ya Sh milioni 20,” alisema.

Naibu Spika huyo alisema taasisi ya Tulia Trust inajihusisha na uboreshaji wa huduma mbalimbali za kijamii hasa elimu, afya na miundombinu.
Dk. Tulia akifurahia zawadi ya kalenda aliyokabidhiwa na Kaimu Mkurugenzi Idara ya Utawala na Fedha, Agnes Kuhenga (mwenye koti) ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa Watoto wa JKCI, Sulende Kubhoja (mwenye koti na tai) ni Mkurugenzi wa DSTV Maharage Chande. 

“Huwa tunapokea maombi  kutoka kwa watu mbalimbali wenye uhitaji ambao wengi huja moja kwa moja kwetu, tunatoa misaada hiyo kwa kushirikiana na wadau,” alisema.

Alisema kupitia taasisi hiyo wanakusudia kuzisaidia hospitali nyingi zaidi kuanzia za mikoa, tarafa na zile zinazotoa huduma kwa watoto.

Dk. Tulia akizungumza na baadhi ya wazazi wenye watoto wanaotibiwa magonjwa ya moyo katika taasisi hiyo mapema leo.

“Tutafanikisha hilo kwa kushirikiana na wadau wetu na tayari wameitikia suala hilo, huwa tunasaidia kujenga  vyumba vya upasuaji, kugawa mifuko ya sementi, mabati, vitanda na vifaa tiba,” alisema.

Kwa upande wa  Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kwa Watoto  wa JKCI, Sulende Kubhoja (pichani) aliishukuru taasisi hiyo kwa kukabidhi msaada huo.

“Televisheni hizi naamini zitasaidia kuwafariji na kuwaondolea upweke watoto wanaolazwa wodini wakati wakisubiri huduma,” alisema.

Kaimu Mkurugenzi Idara ya Utawala na Fedha, Agnes Kuhenga amewaomba wadau wengine kuiga mfano wa Tulia Trust.Dk. Tulia akiwa amembeba mmoja wa watoto wanaotibiwa moyo katika taasisi ya JKCI.

Picha zote na Veronica Romwald