Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement
Na Veronica Romwald, Dar es Salaam

NOVEMBA, mwaka jana Jumanne Salum (34) aligundulika kuwa na dalili za awali za saratani ya tezidume aliamua kwenda kufanyiwa uchunguzi katika hospitali moja ya binafsi jijini hapa.

“Awali nilikuwa napata shida kupata haja ndogo tatizo hilo lilianza taratibu na liliongezeka kadri muda ulivyokuwa unasonga, nikaamua kuchukua hatua,” anasema.

Anasema alidhani ni ugonjwa wa kawaida lakini alishtushwa na majibu ya awali aliyopatiwa na daktari wake.

“Alinieleza nina dalili za awali za saratani ya tezidume, basi akanishauri tufanye vipimo zaidi ili kujiridhisha nikakubali, baada ya uchunguzi alisema kuna majimaji katika kiungo hicho ambayo yamevuka kiwango kinachostahili,” anasema.

Anasema daktari huyo alimuuliza maswali mbalimbali ikiwamo uwezo wake wa kushiriki tendo la ndoa na mwenzi wake.

“Sikumficha… nilimueleza kila kitu kwamba huwa siwezi kushiriki zaidi ya mara moja pindi ninapokutana faragha na mwenzi wangu.

“Basi alinieleza vyanzo mbalimbali vinavyosababisha tatizo hilo ikiwamo kitendo cha kutoshiriki vema tendo la ndoa kwamba ni mojawapo ya visababishi, nikastaajabu, nikaanza matibabu ambayo naendelea nayo hadi sasa,” anasema.

Kelvin Johnson anasema hana uwelewa wowote kuhusu saratani ya tezidume na iwapo kutoshiriki tendo hilo kunaweza kuwa chanzo cha mwanaume kupata ugonjwa huo.

Picha ya mtandao inaonesha mahala tezidume ilipo

“Mimi najua usipozingatia ulaji unaofaa, kufanya mazoezi, unywaji wa pombe kupitiliza ni miongoni mwa mambo yanayoweza kusababisha mwanaume kupata ugonjwa wa saratani ya tezidume.

“Kuhusu kutoshiriki tendo la ndoa ni suala jipya kwangu, sijawahi kusikia kabla labda kama wataalamu wa afya wakituelewesha juu ya hilo tuanze kuchukua hatua,” anasema.

MTANZANIA limezungumza na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Saratani wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Mark Mseti ambaye anafafanua kwa kina katika makala haya.

Tezidume ni nini?

“Tezidume ni kiungo muhimu kilichopo ndani ya mwili wa mwanamume, chini kidogo ya kibofu cha mkojo kikiuzunguka mrija wa kutolea haja ndogo.

“Kamwe huwezi kuiona kwa nje, ipo kwa ndani ni kiungo chenye umuhimu wa kipekee katika kukamilisha mfumo wa uzazi wa mwanamume,” anasema.

Anasema kiungo hicho hutengeneza majimaji maalumu ambayo huambatana na mbegu za kiume wakati wa tendo la ndoa zikilinda mbegu hizo hadi kulifikia yai la mama na kutengeneza mtoto.
“Kwa kawaida tezidume huwa na ukubwa unaolingana na punje ya njegere au mbaazi na huongezeka ukubwa kutokana na mambo mawili,” anasema.

Anataja mambo hayo kuwa ni kule kuongezeka kwa umri wa mwanaume au tatizo la saratani ya tezidume.

“Tezidume huweza kuongezeka hadi kufikia ukubwa wa tunda la apple,” anabainisha.

Saratani ni nini?

Anasema saratani ni jina ambalo limetungwa na wataalamu likiwa na mkusanyiko wa kundi la magonjwa mengi yanayofanana kwenye njia kuu mbili.

“Kwanza ni kule kukosekana kwa udhibiti wa uzalianaji wa seli au chembechembe hai za mwili, pili ni kutodhibitiwa kwa zile chembechembe hai zinazozaliana kwa wingi ambazo huweza kusafiri kutoka sehemu zilipozaliwa kwenda sehemu mbalimbali za mwili,” anasema.

Anasema chembechembe hizo, huko huendelea kuota na kuzaliana kwa wingi na pindi zinapoanza kusambaa humanisha ugonjwa umefikia hatua ya nne ambayo huwa ni ya mwisho.

Anasema inapotokea tezidume limepata saratani dalili kadhaa hujitokeza ambazo pia huwa zinafanana kwa ukaribu na dalili za magonjwa ambayo hushambulia njia ya haja ndogo.

“Hivyo, hatuwezi kujua iwapo ni saratani au la, hadi tutakapofanya vipimo mbalimbali hasa kile cha kuchukua sampuli (kinyama) kutoka kwenye tezidume na kuifanyia uchunguzi maabara,” anabainisha.
Takwimu za WHO

Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) za mwaka 2012 kila mwaka wagonjwa wapya milioni 14.1 hugundulika kati ya hao milioni 8.2 hufariki dunia ikiwa ni sawa na asilimia 13.

WHO inakadiria kwamba vifo hivyo vinategemewa kuongezeka kufikia milioni 22 ifikapo 2030.

Hali ilivyo nchini

Takwimu zilizotolewa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Oktoba, 2017 zinaonesha kila mwaka wagonjwa wapya 50,000 hughundulika wakiwa na magonjwa ya saratani.

Waziri Ummy Mwalimu anasema Tanzania ni mojawapo ya nchi za Kusini mwa Afrika ambazo zinakadiriwa kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa na kwamba idadi hiyo inakadiriwa kuongezeka kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2020.

Kulingana na Waziri Ummy, taarifa kutoka Taasisi ya Saratani ya Ocean Road kwa kipindi cha mwaka 2006 hadi 2015 zinaonyesha kwamba aina za Saratani inayoongoza kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa ni ya mlango wa kizazi yenye asilimia 34.

“Ikifuatiwa na saratani ya ngozi (kaporsis Sarcoma) asilimia 13, saratani ya matiti asilimia 12, saratani ya mfumo wa njia ya chakula asilimia 10, saratani ya kichwa na shingo asilimia saba.

“Saratani ya Matezi asilimia sita, saratani ya damu asilimia nne, saratani ya Kibofu cha mkojo asilimia tatu, saratani ya ngozi asilimia tatu, saratani ya macho asilimia mbili.

“Nyingine ni saratani ya tezi dume asilimia mbili, mbaya zaidi, asilimia 80 ya  wagonjwa wote hao hufika Ocean Road wakiwa katika hatua za mwisho za  ugonjwa na kufanya matokeo ya matibabu kutokuwa mazuri,” anasema.

Kuhusu tendo

Dk. Mseti (Pichani) anasema zipo tafiti ndogondogo ambazo zimewahi kufanyika duniani ambalo zinathibitisha ukweli uliopo juu ya suala hilo.

“Ingawa hakuna utafiti mkubwa uliofanyika kuthibitisha mtu anapofanya ngono mara ngapi kwa wiki hawezi kupata saratani hiyo.

“Lakini zipo tafiti ndogo ndogo ambazo zinaeleza mwanaume ambaye yupo ‘sexually active’ ana uwezekano mdogo kupata saratani ya tezidume kuliko yule ambaye hayupo ‘sexual active’,” anabainisha.

Anaongeza “Hata hivyo, hii haimaanishi mtu awe mzinzi la hasha, kwa sababu akiwa na wapenzi wengi atapata magonjwa hasa ya zinaa ikiwamo Ukimwi na kuyaweka maisha yake hatarini zaidi.

“Inashauriwa angalau mwanaume ashiriki mara tatu kwa wiki ingawa wapo wengine wanaojiweza zaidi ya hapo,” anasema.

Dalili zenyewe

Anasema zipo dalili nyingi ambazo hujitokeza na kawaida katika hatua ya awali huwa hazimsababishii usumbufu wa aina yoyote mwanaume husika.

Anasema hiyo ndiyo sababu wanaume wengi hufika hospitalini wakiwa wamechelewa.

“Dalili za awali ambazo mwanamume akiziona tunamshauri awahi hospitalini kwa uchunguzi ni pamoja na kutoa mkojo ambao hauna nguvu, wakina baba kwa kawaida mkojo wao huweza kuruka umbali wa mita moja hadi mbili.

“Ingawa kadri umri unavyoongezeka ile kasi ya kurusha mkojo hupungua, kwa mtu ambaye ana tatizo la saratani ya tezidume ile kasi hupungua zaidi hata akiwa na umri mdogo,” anasema.

Dk Mseti ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Tiba na Mifumo ya Kulipia (bima za afya) ORCI, anataja dalili nyingine ni kutoa mkojo ambao hukatika-katika.

“Ingawa, dalili hii hatuwezi kusema moja kwa moja kila ambaye mkojo wake hauruki kwa kiwango hicho ana tatizo kwani wapo baadhi ya wanamume ambao tangu wamezaliwa wanapata mkojo unaokatika-katika.

“Lakini kwa yule ambaye zamani walikuwa wakienda haja ndogo wanatoa mkojo bila kukati-katika mwanzo hadi mwisho na ghafla anaanza kupata mkojo unaokatika-katika ni wazi hiyo ni dalili ya awali ya saratani hii,” anasema.

Daktari huyo anataja dalili nyingine ya awali ni mwanaume kushindwa kutoa mkojo pindi tu anapofika chooni.

“Yaani anahisi kabisa kutoa haja ndogo lakini akifika chooni mkojo hautoki, inabidi asubiri… aubembeleze na wengine hadi wajikamue ndipo utoke, si dalili nzuri,” anabainisha.

Anaongeza “Kitendo cha mkojo kutoka huku ukiwa unawasha washa au kuchoma choma inaweza kuwa dalili ya awali ya saratani, ingawa inaweza pia kuwa dalili ya magonjwa mengine ya kuambukiza ni muhimu kuwahi hospitalini.

Anataja nyingine ni mkojo kushindwa kutoka vema na kwamba wapo ambao hulazimika kujikamua tumboni na hivyo kujikuta wakipata maumivu ya tumbo na mkojo hutoka ukiambatana na maumivu makali.

“Inapofikia hapo maana yake ni kwamba tayari saratani ya tezidume imekua na sasa imeubinya (imekandamiza) ule mrija wa mkojo hivyo unashindwa kabisa kupita ipasavyo,” anabainisha.

Anaongeza “Kwa kawaida mkojo huwa unatoka mweupe hasa mtu anapokuwa anakunywa maji ya kutosha, lakini unapotoka ukiwa na damu damu ni dalili ya hatari.
Visababishi

Anasema sababu kuu ni kuzaliwa jinsi ya kiume kwamba kila mwanaume ana uwezekano wa kupata saratani hii.

“Umri unapoongezeka hasa kuanzia miaka 50 na kuendelea muhusika anaweza kupata saratani hii, pia unywaji wa pombe kupita kiasi, unene uliopitiliza ni miongoni mwa visababishi,” anasema.

Anasema wapo pia ambao hupata saratani hiyo kutokana na sababu ya kurithi hasa ikiwa kwenye familia au ukoo kuna ndugu wa damu ambaye amewahi kuugua saratani hiyo.

Hukua taratibu

Anasema saratani ya tezidume ni miongoni mwa saratani ambazo hukua taratibu mno na inaponekana maana yake huwa imeanza muda mrefu.

“Na hii ndiyo taasisi yetu sasa hivi inajikita zaidi katika kuelimisha jamii, watu wajitokeze mapema kufanya uchunguzi wa awali,” anasema.

Anaongeza “Wengi walikuwa wanaogopa baada ya kusikia kipimo ni kidole lakini wasiogope hicho ni kipimo cha juu mno, awali tunafanya hicho cha PSA (cha damu).

Uchunguzi

Anasema muhusika anapofika hospitalini hufanyiwa vipimo mbalimbali ili kujua iwapo ana tatizo hilo au la.

“Tunaanza kwa kufanya vipimo vya awali… tunapima mkojo wake tujue nini hasa kinamsumbua iwapo ni saratani ya tezidume au magonjwa mengine ya maambukizi,” anasema.

Anaongeza “Tunafanya kipimo cha ultra sound ambacho hutuwezesha kuona vizuri ile tezidume na mtaalamu anaweza kutueleza pia limekua kwa ukubwa gani.

“Watu wengi hudhani zile kende (korodani) ndiyo tezidume la hasha, hivi ni viungo viwili tofauti, tezidume ipo chini kidogo ya kibofu ndani ya mwili wa mwanamume.

“Ule mrija wa mkojo unapita katikati ya tezidume na ndiyo maana dalili nyingi nilizotaja utaona ni kupata shida wakati wa kukojoa kwa sababu linapoongezeka ukubwa huziba ile njia,” anabainisha.

Kuhusu kidole

Anasema ni kipimo muhimu pia katika kufanya uchunguzi na kwamba kamwe huwa hawakifanyi kwa nia mbaya kama wengi wanavyodhani.

“Mtaalamu anajua jinsi ya kutumia kipimo hiki, anapoingiza kidole chake huweza kulipapasa lile tezidume kwa ndani na akajua iwapo kuna tatizo au la,” anasema.

Anasema kipo pia kipimo cha damu (Full Blood Picture) ambacho hukitumia kufanya uchunguzi huo na huchunguza viungo vingine vya mwili ikiwamo ini, figo na vinginevyo iwapo vinafanya kazi yake sawa sawa au la.

“Tunatumia kipimo maalumu kinaitwa PSA (Prostate Specific Antigen), ni kipimo cha juu sana kwa mtu ambaye ana tatizo hili,” anasema.

Anafafanua kwamba PSA ni kemikali maalumu ambayo hutengenezwa na tezidume huwa wanatumia kipimo cha damu kupima kiwango cha kemikali hiyo mwilini.

“Kwa kawaida, mwanaume aliyekamilika kiwango cha kemikali yake huwa ni kati ya sifuri hadi nne hiki ni kiwango cha kawaida na huashiria hana tatizo.

“Lakini inapokuwa zaidi ya nne hadi 20 hapo humaanisha kemikali hiyo imetengenezwa kwa wingi na matokeo hayo yanatoa tafsiri kwamba kuna hali isiyo ya kawaida kwenye tezidume.

“Inaweza ikawa ni ukuaji wa kawaida wa tezidume (usio ugonjwa) kutokana na umri mkubwa au maambukizi na pia inaweza kuwa ni saratani,” anasema.

Kwanini

Anasema mara zote ukuaji wa tezidume usio wa saratani (Benign Proestate Hypertrophy – BPH) dalili zake huwa zinafanana  dalili zake na ukuaji wa tezidume ulio saratani.

“Dalili zinafanana kwa ukaribu kwa mfano wanaume wengi wenye umri mkubwa hupata matatizo ya haja ndogo ile ni kutokana na kukua kwa tezidume lakini tutajua ni ukuaji wa kawaida au saratani pindi tutakapomfanyia vipimo,” anabainisha.

Anasema mara nyingi vihatarishi vya saratani ya tezidume vinafanana na vihatarishi BPH lakini kwa BPH kihatarishi kikuu ni umri mkubwa.

“Mwanaume mwenye umri mkubwa atapata shida ya haja ndogo kwa sababu ya kule kukua kwa tezidume yake,” anafafanua.

Anaongeza “BPH humaanisha tezidume limekua lakini seli zimeendelea kudhibitiwa ingawa nayo huweza kupandisha kiwango cha PSA huwa juu ya nne lakini haizidi 20.

“Tutamfanyia upasuaji mgonjwa kuongeza kidogo njia yake ya mkojo ili utoke kwa wepesi kama kawaida.
Anasema ikiwa mgonjwa atakutwa na PSA zaidi ya 20 huwa ni dalili kubwa kwamba ule ukuaji wa tezidume si wa kawaida bali saratani.

“PSA test zipo aina mbili, kuna qualitative PSA test, hii hutuonesha iwapo kile kiwango kimezidi au la na kuna quantitative PSA test  ambacho hutuonesha idadi, zipo ngapi.

“Kuna watu huwa wanafika hadi 1000 wakati normal range haitakiwi kuzidi nne, mgonjwa atalazimika pia kwenda kwa daktari bingwa wa upasuaji wa mkojo ambaye atamfanyia kipimo maalumu cha ‘cystescopy’.

Kinavyofanyika

“Daktari huingiza mpira wenye kamera kwenye njia ya mkojo hadi sehemu ya ndani akiangalia ile njia jinsi ilivyo na ile tezidume ataenda hadi kwenye kibofu pia kwani dalili zile zinaweza kuashiria kuna shida kwenye kibofu au tezidume,” anasema.

Anaongeza “Vipimo vinapotoka ikiwa vimeonesha kuna uvimbe kwenye tezidume mgonjwa hufanyiwa kipimo kingine cha biopsy ambacho daktari huchukua sampuli (kinyama) kutoka kwenye ile tezidume na kuifanyia uchunguzi maabara.

“Kuna namna mbili za kuchukua sampuli, kwa njia ya haja kubwa au ndogo kulingana na daktari atakavyoamua, atachonga ile tezidume kutoa sampuli hiyo na majibu hayo ya maabara ndiyo yatabainisha iwapo ni ukuaji wa kawaida wa tezidume au saratani,” anasema.

Matibabu

Anasema saratani inapogundulika mapema hutibika na matibabu ya awali yanaweza kufanyika kuliondoa kabisa lile tezidume.


“Unaweza kufanyiwa upasuaji kwa njia ya mikono au kwa teknolojia, lakini huwa kuna ‘risk’ ikiwamo kupoteza nguvu za kiume ikiwa baadhi ya mishipa itakatwa kwa bahati mbaya,” anasema.

Anaongeza “Lakini ikiondolewa bila kubughuzi vitu vingine hakuna madhara yoyote yanayoweza kujitokeza, ikiwa ugonjwa umeanza kusambaa kwenda kwenye viungo vingine vya mwili basi huwa tunawapa tiba nyingine ikiwa ile ya hormonal therapy.

“Hapo tunatibu kwa njia ya vichocheo, ili tezidume ikue huwa inasimamiwa na homoni ya  kiume iitwayo testosterone inayotengenezwa kwenye korodani kwa amri ya homoni nyingine inayotengenezwa kichwani kwenye ‘Pituitary gland’.

“Tunafanya upasuaji na kukata mawasiliano, kuzuia homoni inayotoka kichwani hatua hiyo itafanya tezidume inywee na ile PSA itashuka, tunaweza pia kufanya upasuaji mdogo wa kuziondoa kabisa zile korodani,” anabainisha.

Anasema kwa kundoa korodani moja kwa moja tezidume hunywea na mkojo kuanza kupita kama kawaida.

“Lakini ukiondoa korodani pekee bado kuna homoni ya testosterone ambayo inatengenezwa kwenye tezi zingine zilizopo juuya figo (hdrino glands) hivyo itabidi umpatie dawa maalum mgonjwa ili kuzuia homoni hizo,” anasema.

Anasema wapo wanaume ambao huwa hawapo tayari kufanyiwa upasuaji kuondoa korodani zao hivyo huwapatia matibabu ya sindano kila baada ya miezi mitatu kuzia uzalishaji wa homoni hiyo.

“Kuna ambao pia huwa tunawapa dozi ya vidonge ambavyo humeza kila siku kuzuia uzalishaji wa homoni hiyo,” anasema.

Anasema hata hivyo tiba hiyo hufanya kazi miaka miwili hadi mitatu baada ya hapo huwa haiwezi tena kuzuilika na tezidume huendelea kukua.

“Inapofikia hatua hiyo, huwa tunawabadilishia tiba na kuanza kuwapatia ile ya chemotherapy (tiba ya dripu ya saratani) kwa mizunguko sita kila baada ya wiki tatu, mgonjwa hupata madhara kadhaa.

“Huchoka mwili, hunyonyoka nywele lakini huwa ni kwa kipindi kile cha tiba, akimaliza basi nywele huota kama kawaida na kule kuchoka huisha,” anabainisha.

Tiba ya mionzi

“Yenyewe hutokea kwa mashine, mashine tuliyonayo sasa tunatoa mionzi ya variation yenye uwezo wa kuzia ule  uzalianaji wa seli” anasema.

Anaongeza “Lakini tayari tumeanza kufunga mashine mbili zenye uwezo wa kutibu tatizo hili na tunatarajia kutoa tiba hiyo mapema Januari, mwakani.

“Mionzi ya mashine hizi ipo aina mbili, kuna ya nje na ndani… huwa wanapandikiza mbegu (gold seeds) ni sindano fulani ambazo huwa zina-radiate mule ndani na kutibu saratani,” anabainisha.

Athari

Anasema pamoja na hayo ni muhimu muhusika kuwahi hospitalini kwa uchunguzi ili kutibiwa mapema pindi anapogundulika kuwa na saratani hiyo.

“Kwa sababu akichelewa kupata matibabu haya, huwa inakimbilia kwenye uti wa mgongo na kusababisha maumivu ya kiuno, mgongo, miguu na hatimaye hupooza kabisa na kushindwa kutembea,” anasema.

Anaongeza “Ikiwa hali hiyo itajitokeza na akafika hospitalini ndani ya saa 72 tunamfanyia tiba ya mionzi ya dharura na tiba hiyo inatolewa pia pale Hospitali ya Bugando.

Wito

Anawashauri wanamume kujitokeza kufanyiwa uchunguzi mapema ili kupatiwa matibabu kwa wakati ikiwa wanagundulika kuwa na tatizo hilo.

“Unaonekana kuwa ni ugonjwa unaoshambulia zaidi watu wenye hali ya juu ya kiuchumi na kielimu kuliko wa hali ya chini, inaamana huenda ni mfumo wa maisha wanayoishi kundi hilo.

“Unywaji wa pombe kupitiliza, uvutaji sigara ni miongoni mwa visababishi vinavyotajwa kusababisha ugonjwa huu,” anasema Dk. Mseti.

Naye, Mkurugenzi wa Idara ya Kinga wa taasisi hiyo na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Saratani, Crispin Kahesa, anasema kila mwaka huwa wanaona wagonjwa 120 wa saratani ya tezidume.

“Hivyo, tunashauri kwamba ni muhimu mwanaume kuzingatia ulaji unaofaa hasa vyakula vinavyojenga mwili na kufanya mazoezi ya viungo kuepuka ugonjwa huo.

“Idadi ya watu wanaougua magonjwa ya saratani inazidi kuongezeka, mwaka 2016 tuliona wagonjwa wapatao 5200 lakini idadi imeongezeka kwa asilimia 20 katika mwaka 2017 ambapo tumeona wagonjwa zaidi ya 6,000,” anasema.

Anasema idadi hiyo imeongezeka kwani wamefanya uhamasishaji mkubwa kwa kushirikiana na vyombo vya habari na wadau mbalimbali kuwasihi wananchi wajitokeze mapema ili kufanyiwa uchunguzi.

“Wengi wamehamasika na kuja kufanya uchunguzi wa awali, imechangiwa pia na uboreshaji wa huduma za afya ambazo zimesogezwa karibu zaidi na wananchi awali zilikuwa zinatolewa hapa ORCI lakini sasa zinatolewa pembezoni mwa nchi ikiwamo Mwanza, Mbeya, KCMC (Kilimanjaro).

“Kumekuwa pia na ongezeko la hali ya upatikanaji wa dawa kiasi cha mara kumi zaidi mwaka 2017 kuliko ilivyokuwa 2016.

“Lakini bado tunazidi kuhamasisha jamii ibadilishe mfumo wa maisha hasa wazingatie suala la ulaji unaofaa, kufanya mazoezi na kupima afya mara kwa mara ili kuepuka magonjwa ya saratani na mengineyo,” anasisitiza.

Makala haya kwa mara ya kwanza yametoka Januari 11, 2018 katika gazeti la MTANZANIA ambalo nalitumikia.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement