Alhamisi, 11 Januari 2018

MKATABA 'HUKUMU UJENZI WA VYOO' ULIVYOZAA MATUNDA DODOMA

Na Veronica Romwald, aliyekuwa Dodoma

HAIKUWA rahisi Kijiji cha Gwandi, Kata ya Zajirwa, Tarafa ya Itiso, Wilaya ya Chamwino mkoa wa Dodoma, kufikia lengo la kila kaya kuwa na choo bora.

Kijiji hicho kina vitongoji 10 vyenye wakazi zaidi ya 4,000 kati ya wakazi hao kulikuwa na kaya 931 na kati kaya zaidi ya 500 hazikuwa kabisa na vyoo.

Rozina Mpombo ni Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho anasema kaya zaidi ya 300 ndizo zilizokuwa na vyoo ambavyo hata hivyo havikuwa bora.

“Miongoni mwa kaya hizo kuna taasisi 15 pia za serikali, zisizo za serikali na za dini za kikristo na kiislamu. Taasisi ambazo zilikuwa na vyoo japo si bora ni tano pekee, hata taasisi yangu ya utawala haikuwa na choo kabisa,” anabainisha.

Anasema hata hivyo hivi sasa taasisi zote na kaya zote zina vyoo bora na hilo limewezekana baada ya kuhamasishwa katika kikao maalum wilayani.

“Tuliitwa wilayani kulikuwa na maofisa tarafa, wadau wa maendeleo, madiwani, wenyeviti na watendaji tulihamasishwa na tulichefuliwa, nilitoka na hasira kwanini wananchi wangu wanakula uchafu kwenye kijiji changu nikafanya maamuzi.

“Nilifika na mwenyekiti wangu nikamsihi aweke siasa pembeni tukaita vikao vya kijiji na tukaelimisha jamii ili tufikie lengo letu, jamii ilituelewana na viongozi wa vijiji walituelewa tukashirikiana vema,” anasema.

Anasema wataalamu wa Shirika la Plan International kupitia mradi wake wa Usafi wa Mazingira Tanzania (Umata) waliungana nao kuwaongezea nguvu.

Anasema walianza kupitia kaya moja baada ya nyingine kuhakikisha iwapo kweli wananchi wameitikia wito wa kujenga na kutumia vyoo bora.

“Awamu hii tukabaini tena kuna kaya zaidi ya 500 ambazo hazikuwa na vyoo, lakini katika kuhamasisha huko tulipitia changamoto nyingi,” anasema.

Vitisho

“Siku moja tulikimbizwa na kijana mmoja ambaye alitoka na panga lake nje na kututishia, tulitoka lakini tulijiuliza tutarudi vipi kwa sababu hatuwezi kumuacha na lengo letu awe na choo na akitumie.

“Tulirudi tena na tena tukakaa naye tukamuelimisha, akatuelewa na sasa amejenga choo chake na anakitumia, uelewa wa jamii ulikuwa mdogo ilituchukua muda mrefu kidogo kuipokea elimu hii,”  anasema.

Anasema changamoto nyingine ilikuwa ni umbali kutoka eneo moja hadi jingine na kwamba kijiji hicho pia kipo mpakani hali iliyofanya wanakijiji kukwepa suala hilo.

“Yaani unamuelimisha mtu anasema hajengi choo kwa sababu hayupo kwenye kijiji changu, ikabidi tubadili mbinu na kuwaeleza ujenzi wa vyoo ni suala la kitaifa na si kijiji pekee na ikiwa mtu hataki kujenga ahame aende kwingine, wakatekeleza,” anasema.

Anasema sasa wameweka utaratibu wa kuafuatilia kwa ukaribu kila mara kuhakikisha jamii inaendelea kujenga na kutumia vyoo.

“Na tumeweka amri ni marufuku mgeni yeyote kuhamia kwenye kijiji chetu ikiwa sehemu anayekwenda kuhamia hakuna choo bora,” anasema.

Anasema suala hilo linasimamiwa kwa ukaribu na maofisa watendaji wa kijiji hicho.

“Hawezi kuruhusu mgeni kuhamia kama anapokwenda kuishi hakuna choo bora,” anasema.

Kijiji kingine

Kijiji cha Chibwe ni mojawapo ya vijiji vilivyosajiliwa mwaka 2014, kijiji hicho kipo katika Kata ya ya Igandu, Tarafa ya Mvumi, Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma.

Sospeter Matonya ni Mtendaji wa kijiji hicho kipya anasema awali wananchi wengi walikuwa hawajajenga vyoo bora kijijini hapo na kwamba walikuwa hawazingitii suala la kunawa mikono pindi wanapotoka chooni.

“Kijiji kina jumla ya kaya 352, tulifanya ukaguzi tukabaini kaya 156 pekee ndizo ambazo zilikuwa na vyoo huku kaya 196 hazikuwa na vyoo kabisa,” anasema.

Anasema wakazi wa kijiji hicho walikuwa wamejenga tabia ya kutumia choo kimoja zaidi ya kaya moja.

“Yaani unaweza kukuta katika eneo kuna kaya tatu, nne, tano na kuendelea wote wanatumia choo kimoja, lakini baada ya Mkuu wa Wilaya kwa kushirikiana na Shirika la Plan International kupitia mradi wa Umata tulihamasika kujenga choo kwa kila kaya.” Anasema.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu

Anaongeza “Tulianza kwanza kuhamasishwa sisi viongozi baadae tukatoka na kwenda kuhamasisha jamii kwamba kila kaya ijenge na kutumia choo chake.

“Tena kijengwe kwa kuzingatia ubora unaotakiwa, kiwe na mlango, shimo lililosakafiwa, kiezekwe na kiwe na kibuyu chirizi,” anasema.

Anasema baada ya jamii kupewa elimu juu ya umuhimu wa matumizi ya vyoo bora na kunawa mikono baada ya kutoka chooni sasa hivi zaidi ya kaya 200 kijijini hapo zimejenga vyoo bora.

“Hatukutumia nguvu kubwa wa gharama tulichofanya ni kuwahamasisha wananchi, tuliwahimiza kwamba yule ambaye hatajenga choo tutampeleka mahakamani basi wakahamasika na kujenga vyoo vyao wenye kwa kasi kubwa na sasa wanavitumia,” anabainisha.

Janeth Mganga ni mmoja wa wananchi katika kijiji hicho anasema baada ya kuhamasika alishauriana na mumewe wakajenga choo wakaweka ukuta wakaezeka vizuri wakaweka na milango,

“Tukaanza kutumia choo chetu na zile familia zingine nne zikaona vema na kufuata nyayo zetu, zikajenga vyoo vyao,” anasema.

Anaongeza “Baada ya kukamilisha choo changu, kwa kuwa wanakijiji wenzangu walikuwa wakinicheka kwa kuwa sikuwa na choo, niliamua kuandika ujumbe maalum kwenye kuta zake.

“Niliweka tangazo, yeyote nitakayemuta nitamkamata na kumchukulia hatua, nikaandika pia ‘usione vimeng’aa vimegharamikiwa, jenga choo kwa familia yako, basi wale ambao hawakuwa wamejenga vyao walihamasika na kujenga pia,” anasema.

Mkataba

Isabela Mgombaheka ni Mtendaji wa kijiji cha Msonjile B na Kaimu Mtendaji wa kijiji cha Msonjile A ambavyo vipo Kata ya Sejeli  Tarafa ya Kongwa Wilaya ya Kongwa.

Anasema wao waliamua kutumia mbinu ya kuwaandikisha mkataba maalum wa hukumu ya ujenzi wa vyoo wakazi wa vijiji hivyo ili kufikia lengo la kila kaya kujenga na kutumia choo bora.

“Kijiji cha Msonjile B kina wakazi wapatao 3048 kaya 581 taasisi za kidini na utawala saba,” anasema.

Anasema kabla ya kuanza kwa mradi wa Umata katika kijiji hicho kulikuwa na kaya 200 ambazo hazikuwa zimejenga vyoo bora.

“Ilituchukua muda mrefu kuishawishi jamii katika kijiji hiki kujenga na kutumia vyoo bora, kwa sababu wengi hapa ni wafugaji na hawaamini kabisa katika ujenzi wa vyoo kwa sababu wengi wamezoea kuishi kwa kuhamahama kutoka eneo moja hadi jingine wakitafuta malisho ya mifugo yao,” anasema.

Anaongeza “Tulijitahidi kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa matumizi ya vyoo bora na unawaji mikono kupitia mradi wa Umata.

“Tulifanya kazi hiyo kwa kushirikiana na kamati za afya za kitongoji za kijiji hatimaye April 11, mwaka tulitambulika kuwa kijiji kilichokidhi vigezo kuwa na vyoo kundi A, B na C,” anasema.

Anasema wakati akiwa Mtendaji wa kijiji cha Msonjile B, alipokea barua ya kukaimishwa kijiji cha Msonjile A ambako pia alikuta kaya 59 ambazo hazikuwa na vyoo,
Waziri Ummy alipofanya ziara mkoani humo hivi karibuni kukagua utekelezaji wa awamu ya kwanza ya kampeni ya usafi wa mazingira (NIPO TAYARI)

Mkakati

Anasema walitumia mbinu ya kutoa elimu kwa jamii na kufanya ufuatiliaji wa mara kwa mara ili kujihakikishia kwamba jamii imejenga vyoo bora.

“Ilibidi tutumie mbinu hiyo na nyingine nyingi ili tufanikishe lengo hasa kupeleka elimu kwa jamii kuwajengea uwelewa wa umuhimu wa matumizi ya vyoo.

“Lakini pia tuliandaa mkataba huo maalum ambao tuliwasainisha wale ambao tuliwabaini hawana vyoo na tuliwapa siku maalum wahakikishe wamejenga kabla ya siku hizo kwani zikiisha tutawafikisha mahakamani kwa mujibu wa mkataba huo,” anasema.

Anaongeza “Wengi walihamasisha na kujenga vyoo kabla ya kuisha kwa muda ambao tuliwapangia kulingana na mkataba tuliowasainisha.

“Tulitumia pia sheria ndogondogo za vijiji zilizopo, kwa kutumia sheria hizo tuliwakamata wale ambao walifanya uzembe na kuwatoza faini na fedha hizo zilitusaidia kuwajengea vyoo wale ambao walikuwa hawajiwezi kabisa.

“Kwa mfano, tuliweza kumjengea choo kikongwe mmoja, mlemavu mmoja na kipofu mmoja na wale ambao tuliwatoza faini tuliwapa mkataba kwa kuwapa muda maalum ili wahakikishe wanajenga choo,” anasema.

Anasema kwa kuwa choo bora kinahitajika kuwa kimesakafiwa vema na kwa kuwa jamii nyingi hazikuwa na uwezo wa kifedha walitumia mbinu nyingine mbadala.

“Tulinunua mifuko ya sementi kwa kushirikiana na kamati ya afya na wadau wetu wa Umata, tukazileta kijiji na kuwauzia wananchi kwa bei nafuu kabisa ili wale ambao hawakuwa na uwezo waweze kumudu gharama, tukafanikiwa katika hilo,” anasema.

Anaongeza “Sasa watu wamehamasika na wameelewa umuhimu wa kujenga na kutumia vyoo bora bila kusahau unawaji mikono mara baada ya kutoka chooni.

Mafanikio

Mkurugenzi wa Umata, Nyanzobe Malimi anasema wamefanikiwa kuhamasisha jamii kujenga vyoo na kwamba tayari asilimia 65 ya kaya vyoo vyao vimeboreshwa.

“Haikuwa kazi rahisi kufikia kiwango hicho, kati ya kaya hizo asilimia 31 ndizo ambazo zina vyoo bora zaidi yaani kile ambacho kina sakafu inayoweza kusafishika na mlango,” anasema.

Anasema hadi sasa ni asilimia nne tu ya kaya ambazo hazina kabisa vyoo.

Anasema jamii sasa inaona umuhimu wa kunawa mikono hasa baada ya kutoka chooni na kwamba hilo wamekuwa wakilizingatia ili kujikinga dhidi ya magonjwa yatokanayo na hali ya uchafu.

“Haikuwa rahisi kufikia mafanikio haya, tumepitia changamoto nyingi, kwa mfano kuna maeneo tunakwenda unakuta mwenyekiti wa kijiji hana choo inakuwa ngumu kumuhamasisha mwananchi wake kujenga choo wakati yeye mwenyewe hana.” Anabainisha.

Anaongeza “Changamoto nyingine zilijitokeza katika maeneo ambako tulikuwa tunakwenda na kukuta viongozi wanatoka vyama tofauti vya siasa.

“Unakuta diwani anakaa pembeni na kuacha kuhamasisha wananchi wake kujenga vyoo bora, ilitupa shida lakini tunashukuru jamii ilitusikiliza na kutuelewa.

“Sasa hivi vijiji 76 vimefikia kiwango cha kuishi kwenye makazi safi na salama yasiyo na kinyesi, tunasema ‘Open Defecation Fee (ODF)’ na wanapewa vyeti na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kuvitambua,” anasema.


Makala haya kwa mara ya kwanza yametoka Januari 11, 2018 katika gazeti la MTANZANIA ambalo nalitumikia