Wauguzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) wakiwasaidia wagonjwa kupanda katika gari tayari kwa safari ya kuhamia Hospitali ya Mloganzila hivi karibuni.
Na Veronica Romwald, Dar es Salaam
“Sitaki mnipeleke huko mnapotaka niende, mimi nilikuja hapa
Muhimbili kutibiwa kama mmeshindwa bora ndugu zangu wanichukue na kunirudisha
nyumbani,”.
Ni kauli ya mmoja wa wagonjwa ambaye alikuwa akisukumwa na
wauguzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kupelekwa katika gari la wagonjwa
tayari kwa safari ya kuhamishiwa kwenda Hospitali ya Chuo Kikuu Cha Afya na
Sayansi Shirikishi Muhimbili kampasi ya Mloganzila (MAMC) – Mloganzila.
Mgonjwa huyo ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini, anasema
hajui kwanini anahamishwa kwenda huko na anazidi kulalama kwamba arudishwe
nyumbani kwake.
“Usijali mama, unapopelekwa (Mloganzila) ni pazuri zaidi ya hapa
unapotolewa (Muhimbili), hautakwenda peke yako utakwenda na sisi (wauguzi)
tutakuwa pamoja hadi utakapopona na kuruhusiwa kurudi nyumbani,” anaelezwa na
Muuguzi mmoja aliyekuwa akisukuma kitanda hicho.
Nashuhudia wagonjwa waume kwa wake wakiendelea kutolewa katika
wodi hiyo na kusaidiwa kupanda katika gari aina ya costa yenye namba T 563 CZX
tayari kwa safari.
“Humo ndani mnatakiwa kupanda na msaidizi (ndugu) mmoja,
hakikisheni kila mmoja amepanda na ndugu yake,” anasema Mkuu wa Kitengo cha
Mawasiliano ya Umma na Wateja Muhimbili, Aminiel Aligaesha aliyekuwa hapo
kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa sawa.
“Mwishoni mwa mwaka jana Rais John Magufuli akizindua MAMC
alisema baadhi ya wagonjwa waliolazwa Mwaisela wahamishiwe Mloganzila ili
kupunguza msongamano,” anasema.
Anasema Muhimbili walianza kutekeleza agizo hilo mwishoni mwa
Desemba, mwaka jana.
“Jengo hili lina vitanda 240 na wakati wote waliolala waliokuwa
wapatao 250 hadi 300 unakuta wengine walilala wawili au chini.
“Wagonjwa walikuwa hawapungui humu ndani, na hiyo ndiyo sababu
kuu iliyofanya wapunguzwe kutoka hapa kwenda Mloganzila, ndani ya mwezi mmoja
tutakuwa tumepeleka wagonjwa wapatao 170,” anasema.
Wauguzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) wakiwasaidia wagonjwa kupanda katika gari tayari kwa safari ya kuhamia Hospitali ya Mloganzila hivi karibuni.
Anaongeza “Muhimbili tunashirikiana kwa ukaribu na Mloganzila na
tumepanga madaktari wetu zamu kuhakikisha wanakwenda huko kutoa huduma.
“Mloganzila ina vifaa vya kisasa na tunapofanya matengenezo vya
kwetu tunasitisha huduma na kuwapeleka Mloganzila wagonjwa, hadi sasa
tumewafanyia vipimo wagonjwa wapatao 30 huko.
“Hivyo, niwatoe hofu wagonjwa wanaohamishiwa Mloganzila kwamba
hatua hii haitaathiri matibabu yao kwa namna moja au nyingine, watapa huduma
zote zinazostahili,” anasisitiza.
Hayo yanajiri nje ya wodi ya Mwaisela Januari 10, mwaka huu saa
kumi jioni ambapo nimefika na waandishi wenzangu punde tukitokea MAMC ambako
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu
alifanya ziara.
Waziri Ummy anasema serikali kupitia Wizara hiyo imehamisha
rasmi Idara ya Magonjwa ya Ndani (internal medicine) ya Muhimbili katika
kampasi ya Mloganzila (MAMC).
“Kutokana na hatua hiyo, tumeagiza madaktari bingwa 35 wa Idara
hiyo kuhamia Mloganzila mara moja pamoja na wagonjwa wapatao 270
waliolazwa katika idara hiyo kwa matibabu,” anabainisha.
Anasema hospitali hiyo ya MAMC sasa inatoa huduma saa 24 na
kwamba ina vifaa vya kisasa vya kutosha na madaktari bingwa wa kutosha.
“Tunahamisha madaktari wote wa Idara hiyo, wauguzi pamoja na
wataalamu wengine na kwa hatua hiyo. Naiagiza Muhimbili kuhakikisha
wanakarabati jengo la Mwaisela wodi namba mbili hadi saba,
wagonjwa watakaobaki huko ni wale walio mahututi,” anasisitiza.
Waziri Ummy akizungumza jambo na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo na hospitali ya MAMC, Profesa Said Abood hivi karibuni alipotembelea MAMC
Uhamisho Mkoani
Waziri Ummy anasema serikali imeanza kuwapangua madaktari bingwa
20 wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), kwenda katika Hospitali za rufaa za
Mikoa.
Kutokana na hatua hiyo anawataka waganga wakuu wa Mikoa na
wafawidhi katika Hospitali za Kanda kuanza kuwapeleka wagonjwa wa Magonjwa ya
nje Mloganzila na si Muhimbili.
“Tumejipanga kuhakikisha hospitali zote za Mikoa zinakuwa na
madaktari bingwa katika kada nane ikiwa ni pamoja na daktari bingwa wa magonjwa
ya uzazi na wanawake, watoto, Magonjwa ya jumla, masuala ya radiolojia.
“Tumepokea rasmi Hospitali za Mikoa na tumefanya ya
kutathimini miundombinu iliyopo na madaktari bingwa waliopo kwa ajili ya
kuanza kuwatawanya,” anabainisha.
Anaongeza “Hospitali ya Muhimbili itabaki kuwa Hospitali ya
kibingwa kwa magonjwa yanayohitaji upasuaji, ingawa hivi sasa bado wataendelea
pia kushirikiana kutibu pia magonjwa ya ndani.
Athari zake
Katika Kongamano la 49 la Afya Kitaifa na Mkutano Mkuu wa Mwaka
wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Rais wa chama hicho, Dk Obadia Nyongole
alisema Tanzania inakabiliwa na uhaba wa madaktari bingwa kwa kiwango cha
asilimia 82.
Alisema ili kukidhi mahitaji wanahitaji madaktari bingwa 2,453
wa fani mbalimbali hata hivyo waliopo hivi sasa ni 451 pekee ambao wanahudumia
nchi nzima.
Kutokana na hali hiyo, MTANZANIA lilihitaji kujua hatua
iliyochukuliwa na serikali kuwahamisha madaktari bingwa waliopo Muhimbili, je
ina athari gani.
Chama cha Madaktari
Dk Obadia kwanza anaipongeza serikali kwa hatua hiyo hata hivyo
anasema suala la kuboresha ni mtambuka na kwamba linategemea vitu vingi.
“Madaktari hawa wanaotolewa Dar es Salaam huko wanapotoka
wanaacha uhaba, nchi yetu ina uhaba mkubwa wa madaktari bingwa hivyo suluhu ya
kudumu ni kusomesha madaktari bingwa wa kutosha zaidi.
“Kwa hiyo tunaiomba serikali iendelee kusomesha madaktari katika
‘level’ ya ubingwa,” anasisitiza.
Anaongeza “Upatikanaji wa vifaa tiba ni kitu muhimu ambacho
nacho lazima kitazamwe na kufanyiwa kazi, ni mapema mno kusema madaktari
wamelichuliaje lakini sisi kama chama tulikaa vikao vya ndani na
tukalizungumza.
Mdahalo
“ Tuliita mdahalo wa kitaaluma na madaktari waliopo Dar es
Salaam, lakini kwa bahati mbaya kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo
wetu kongamano la kitaalamu halitaweza kufanyika.
“Hata hivyo tunaamini madaktari wataendelea kutupa maoni hilo
liweze kufanya na kuwa na tija zaidi kwa Taifa na naamini serikali itaendelea
kuweka milango wazi ili tuendelee kushauriana zaidi na sisi wanataaluma juu ya
njia nzuri zaidi ya kuitumia kuhakikisha kwamba uhamisho huu hauleti
sintofahamu kati ya wanataaluma na serikali ilivyopanga.
Mfano hai
Dk. Nyogole (pichani) anasema wanayo mifano hai wa mwaka 2011/12 kwamba kuna madaktari
waliotolewa na kupelekwa kwenye baadhi ya Hospitali za Mikoa hata hivyo
walipofika huko mamlaka za ajira zilisema hazina bajeti za mishahara yao.
“Walihamishiwa kule bila wao kuandaliwa kwa hiyo mazingira
yakawa si rafiki kwa wale madaktari ikabidi watafute sehemu zingine za kwenda
kufanya kazi,” anasema.
Ushauri
Dk. Obadia anasema ni muhimu wale ambao watawapokea madaktari
hao wahakikishe wanakuwa na taarifa sahihi na kuweka mazingira rafiki kwao.
“Sisi ni chama cha kitaaluma tupo tayari kwa majadiliano na
serikali, tutawasiliana na mamlaka husika ili kuweza kujadiliana namna gani
hilo litafanyika vizuri zaidi liwe na tija kwa Taifa, jamii tunayohudumia na
kwa madaktari wenyewe,” anasema
Waziri awatoa hofu
Waziri Ummy anasema madaktari watakaohamishwa, watahimishwa
pamoja na viwango vyao vya mishahara waliyokuwa wakipatiwa awali.
“Katika hili niwatoe hofu kabisa, ni kweli pia kwamba tuna uhaba
wa madaktari bingwa lakini tunafundishwa kuwatawanya wachache
waliopo ili kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma za kibingwa.
“Kwa sababu, kwa mfano... daktari bingwa wa wanawake Bugando
anaona zaidi ya wagonjwa 20lakini wa Muhimbili anaona wagonjwa watatu na
hospitali ya Rufaa ya Tanga hakuna daktari hata mmoja, lazima tuwatawanye
waliopo,” anasisitiza.
Hatua zaidi
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo na hospitali ya MAMC, Profesa Said
Abood anasema hivi sasa kila mwaka chuo Cha Muhas, Bugando vinazalisha
madaktari bingwa wapatao 150 hadi 180.
“Tunatarajia madaktari hao watakaotoka vyuoni watasaidia
kukabili uhaba wa madaktari bingwa ulipo hivi sasa nchini,” anasema.
Anasema pamoja na hayo wamejipanga kuhakikisha wanatoa huduma
bora kwa wagonjwa wote watakaofika na wale watahamishiwa katika hospitali hiyo
kutoka Muhimbili.
“Wagonjwa tutakaokuwa tunatibu ni wale ambao watakuwa hawahitaji
huduma za upasuaji, magonjwa hayo kitaalamu huitwa magonjwa ya ndani kama vile
malaria, figo, moyo, ngozi na mengineyo,” anasema.
Picha zote na Veronica Romwald
Makala haya kwa mara ya kwanza yametoka kwenye gazeti la MTANZANIA ambalo pia nalitumikia Januari 18, 2018
Chapisha Maoni