Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement
Madaktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo na Mgongo wa MOI wakimfanyia upasuaji mgonjwa wa kuondoa uvimbe chini ya fuvu la kichwa, hivi karibuni.
Na Veronica Romwald, Dar es Salaam
HERI ya mwaka mpya msomaji wa gazeti  letu la MTANZANIA na hasa jarida la Jamii na Afya, kwa pamoja tunapaswa kumshukuru Mwenyezi Mungu kutujalia kufika mwaka mpya wa 2018.
Kwa sababu wapo wengi ambao walitamani kufika lakini haikuwa hivyo, leo hii wamefariki dunia, hawapo tena, mengi yametokea mwaka 2017.
Leo katika jarida la Jamii na Afya tunakuletea baadhi ya mambo yaliyotokea katika sekta ya afya ambayo kimsingi yameweka msingi wa nia ya serikali kutoa huduma za matibabu ya kibingwa nchini dhidi ya magonjwa mbalimbali.
Upasuaji wa Kibyongo
Katika mwaka 2017, jumla ya watu 13 walifanyiwa upasuaji wa kutibu tatizo la kibyongo “scoliosis’ katika Taasisi  ya Tiba ya Mifupa, Mgongo, Ubongo na Mishipa ya Fahamu Muhimbili (MOI).

Akizungumza na MTANZANIA mapema Desemba, Meneja Uhusiano na Ustawi wa MOI, Almasi Jumaa alisema upasuaji huo wa aina yake ulianza kutolewa katika taasisi hiyo Januari, 2017.

Ulifanywa na madaktari bingwa wa upasuaji wa mifupa na mgongo (Spine Surgeons) wakishirikiana na wale wa upasuaji wa ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu(Neurosurgeons) wa taasisi hiyo.

“Madaktari hao wazalendo wamefanya upasuaji huo kwa mafanikio makubwa nab ado kuna wagonjwa wengine 30 ambao wanaendelea kufanyiwa uchunguzi kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji huo,” alisema.

Upasuaji huo huhitaji wataalam bobezi aliuelezea kuwa ni mgumu na mkubwa kufanyika kwani huwa wanafanya ili  kunyoosha mgongo uliopinda na kuonekana kama herufi “S” unyoke na kuwa wa kawaida.

“Wakati mwingine mgonjwa inabidi afanyiwe upasuaji kwa hatua. Anaweza kufanyiwa upasuaji hata mara tatu ili kuhakikisha mgongo unanyooka kabisa”.

Jumaa alisema kabla ya kuanza kufanyika upasuaji huo MOI wagonjwa walikuwa wakipewa rufaa kwenda nje ya nchi ambako gharama za matibabu ni ghali. 

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu

“Gharama ya matibabu ya upasuaji huu kwa mgonjwa mmoja nje ya nchi ni kiasi cha Dola 20,000 hivyo kwa wagonjwa 13 serikali ingegharamia Dola 260,000 ambazo ni sawa na zaidi ya Sh milioni 500 ambazo tumeziokoa kwa kufanya upasuaji huo nchini,” alibainisha.

Alitoa wito kwa watanzania kwamba wale wote wenye watoto wenye matatizo ya vibiongo vya kupinda mgongo(scoliosis) wawawahishe hospitali ili wafanyiwe uchunguzi wa kitaalam.

Upasuaji wa ubongo
Kwa mara ya kwanza, Novemba 2017, Taasisi ya MOI ilifanikiwa kufanya upasuaji mkubwa wa ubongo mgonjwa aliyepooza mwili kutokana na ajali ya barabarani.

Wiki mbili baada ya upasuaji huo kufanyika mgonjwa huyo aliweza kusimama, kutembea na kula chakula mwenyewe bila pasipo kusaidiwa na mtu.

Upasuaji huo wa aina yake umefanywa katika taasisi hiyo na madaktari bingwa upasuaji wa ubongo, uti wa mgongo na mishipa ya fahamu wazalendo.

Ulifanywa na madaktari bingwa Nicephorus Rutabasibwa na mwenzake Laurent Lemery.

Akizungumza na MTANZANIA katika mahojiano maalum, Dk Rutabasibwa alisema pasuaji huo kitaalamu unaitwa Craniocervical Stabilization and Fussion.

"Ni upasuaji mkubwa unaohusisha kuunganisha mishipa ya fahamu iliyovunjika ya mgonjwa, alikuwa amevunjika mno katika pingili za mifupa ya kichwa hasa eneo la kichogo inapoungana na uti wa mgongo,” alisema.

Daktari huyo alisema kutokana na kuvunjika kwa uti wa mgongo ndiko kulipelekea mgonjwa huyo kupooza mikono na miguu yake.

“Tulipompokea alikuwa hawezi kushika kitu chochote hata kutembea, alikuwa analala tu kitandani muda wote baada ya kufanikisha upasuaji huo aliweza kuinuka na kufanya kila kitu pasipo kusaidiwa,” alibainisha.

Alisema ni upasuaji ghali mno na kwamba walimuwekea implant (vipandikizi) nane, na kila kimoja kinauzwa Dola 1000 sawa na Sh milioni mbili, imegharimu takriban kiasi cha zaidi ya Sh milioni 10 kumtibu,” alibainisha.

Alisema iwapo mgonjwa huyo angepelekwa nje ya nchi kufanyiwa upasuaji huo ingegharimu zaidi ya Sh milioni 25 ikiwa ni gharama za tiba,usafiri na gharama za daktari msindikizaji.

“Zaidi ya asilimia 50 ya wagonjwa tunaowahudumia hapa MOI ni wa ajali hasa za bodaboda, ni muhimu wakafuata sheria za usalama barabarani kuepuka ajali,” alishauri.
Taasisi ya Ocean Road

Matibabu ya Tezidume

Saratani ya tezidume ni miongoni mwa magonjwa yanayotajwa kutesa wanaume wengi nchini, mwishoni mwa mwaka 2017, Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) ilifunga rasmi mashine mbili zenye uwezo wa kutibu ugonjwa wa saratani ya tezidume.

Akizungumza na MTANZANIA, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Saratani wa ORCI, Mark Mseti alisema wanatarajia kuanza kutoa matibabu hayo mapema Januari, 2018 baada ya mafundi kukamilisha kazi hiyo.

“Ni mashine zenye uwezo wa hali ya juu mno ambazo zinatumika katika mataifa makubwa duniani katika kutoa matibabu dhidi ya saratani ya tezidume.

“Hizi ni tofauti na zile tulizonazo ambazo zilifungwa kwa muda mrefu sasa, hizi zinazofungwa sasa zina uwezo wa kutibu kabisa tatizo la saratani ya tezidume,” alisisitiza.

Dk. Mseti pamoja na maboresho hayo changamoto kubwa wanayoiona ni wanaume kuwa waoga kujitokeza kufanya uchunguzi kujua iwapo wanakabiliwa na tatizo hilo au la.

“Wengi wanaogopa kipimo (cha kidole) lakini niwatoe hofu kwamba siku hizi tunacho kipimu maalum cha damu kinaitwa kitaalamu PSA, tunakitumia hicho kufanya uchunguzi wa awali,” alibainisha.

Aliongeza “Hivyo nawasihi wajitokeze, saratani inapogundulika mapema matibabu yake nayo yanakuwa rahisi na kwa kuwa mgonjwa anapewa matibabu sahihi huwezekano wa kupona ni mkubwa ikilinganishwa na akichelewa matibabu.
Upandikizaji vifaa vya usikivu
Akizungumza na MTANZANIA hivi karibuni, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma na Huduma kwa Wateja, Aminiel Aligaesha alisema mapema Januari, 2018 wanatarajia kufanya upasuaji huo kwa awamu ya pili.
Julai, 2017 Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu alizindua rasmi huduma ya upasuaji na upandikizaji kifaa cha usikivu kwa uatoto waliozaliwa na tatizo hilo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Mkurugenzi wa Muhimbili, Profesa Lawrence Museru alisema hatua hiyo imeiwezesha serikali kuokoa
Alisema hali inaonesha tatizo hilo la usikivu limekuwa likiongezeka katika jamii ya watanzania kama ilivyo kote Duniani na kwamba utafiti wa makadirio ya Hospitali hiyo unaonesha kwa mwaka takribani watoto kati 200 watahitaji huduma hiyo nchini.
“Utaalamu ambao umeendelezwa takribani miaka 20 ya hivi karibuni unaonyesha kuwa watoto hawa wakigundulika mapema na kuwekewa vifaa vya usikivu (Cochlear Implant) wataishi kama kawaida, wakati wasipopata huduma hii watakuwa viziwi” alinukuliwa Prof. Museru.
Alisema kwa mara ya kwanza  mwaka 2003,Muhimbili ilipeleka mgonjwa mmoja kwenda kutibiwa nchini India tangu hapo wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo wamekuwa wakiongezeka huku huduma hiyo ikiwa na gharama kubwa inayofikia hadi kati ya Sh milioni 80 hadi Sh milioni 100 kwa mgonjwa mmoja.
Hadi kufikia 2016 ni wgonjwa 50 tu waliokuwa wamefaidika  kupata huduma hiyo ya ufadhili kutoka Serikalini na kwamba kuanzishwa  kwa huduma nchini, Serikali itapunguza gharama kwa asilimia 60 na kufikia wastani wa Sh milioni 36 kwa mgonjwa mmoja hivyo hatua hiyo itasaidia wagonjwa wengi kufanyiwa upasuaji huo nchini
Kutokana na kuanza kutolewa kwa huduma hiyo nchini, Waziri Ummy alisisitiza kwamba serikali haitagharamia tena matibabu ya huduma hiyo nje ya nchi na ikiwa kuna mtu atahitaji kwenda nje ataenda kwa gharama zake mwenyewe.
Upandikizaji figo
Novemba 21, 2017 Madaktari Bingwa wa Magonjwa ya Figo wa Hospitali ya Taifa Muhimbili wakishirikiana na wenzao wa Hospitali ya BLK ya New Delhi, India kwa mara ya kwanza walifanikiwa kufanya upasuaji wa kihistoria wa upandikizwaji wa figo.
Walimfanyia upasuaji huo mwanamke mwenye umri wa miaka 29 ambaye alipatiwa figo na ndugu yake na alikuwa katika hatua ya tano ya ugonjwa huo.
Waziri Ummy alinukuliwa akisema kwamba upasuaji huo wa kihistoria ni kielelezo cha juhudi za serikali ya Awamu ya Tano za kuboresha huduma za afya nchini zikiwemo zile za ubingwa wa daraja la juu.
“Upasuaji huu ni juhudi zinazofanywa na serikali za kupunguza rufaa za wagonjwa wanaohitaji huduma hizo nje ya nchi na hivyo itaokoa fedha ambazo zingelipwa nje ya nchi kugharamia matibabu hayo na badala yake fedha hizo zitatumika katika maendeleo katika maeneo mengine,” alisema.
Zaidi ya mwaka mmoja hospitali hiyo ilijikita kuwekeza katika kuongeza ujuzi wa wataalamu wa aina mbalimbali ambapo ilipeleka nchini India wataalamu wa upasuaji wa kupandikiza figo kwa mafunzo ya vitendo na wataalamu wawili walipelekwa nchini Norway.
Alisema kuanza kutolewa kwa huduma hiyo nchini, kutawezesha serikali kuokoa fedha na kupunguza gharama ya kupeleka wagonjwa nje ya nchi kufuata matibabu hayo.
Alisema kwa mwaka iligharamia matibabu ya wagonjwa 35 ambapo kila mmoja ilikuwa ni Sh milioni 80 hadi Sh milioni 100 kugharamia matibabu ya mtu mmoja hata hivyo kwa huduma hiyo kutolewa nchini itakuwa ni Sh milioni 21 pekee.
Hospitali ya kisasa
Novemba 25, 2017, Rais John Magufuli, alizindua rasmi Hospitali ya Rufaa ya Taaluma na Tiba (MAMC) ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) iliyoko Mloganzila, jijini Dar es Salaam.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Mpoki Ulisubsya kupitia taarifa yake aliyoitoa kwa vyombo vya habari Desemba 14, 2017 alisema ilikuwa imeanza kutoa huduma za matibabu.

Dk. Ulisubsya alisema inapokea wagonjwa waliopewa rufaa kwa ajili ya matibabu ya magonjwa ya ndani (internal medicine).

Alisisitiza hospitali hiyo ina uwezo wa kutoa huduma za kibingwa kwa kiwango kama kile ambacho kinatolewa na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na kwamba, MAMC inashirikiana na wataalamu mabingwa kutoka MNH katika kuhudumia wagonjwa.

“Wizara inawahakikishia wananchi na wadau wote kuwa, huduma zinazotolewa na MAMC zinajumisha pia huduma za daraja la ubingwa wa ngazi ya juu  (super specialized services) na zenye ubora stahiki,” alisema.

Maandilizi upandikizaji ini

Mwishoni mwa mwaka 2017, Muhimbili ilipeleka nchini India wataalamu wake saba ambao wamekwenda kujifunza jinsi ya kufanya upasuaji wa kupandikiza ini na kutibu magonjwa ya mfumo wa chakula.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma, Aminiel Aligaesha anasema mafunzo hayo yatachukua muda wa miezi mitatu.

Anasema timu hiyo ya wataalam inajumuisha madaktari bingwa wanne wa magonjwa ya mfumo wa chakula na ini, wauguzi wawili wanaosimamia mifumo ya hadubini na mhandisi wa vifaa tiba anayesimamia mitambo ya hadubini.

“Lengo la Hospitali ni kuendelea kutekeleza azma ya serikali kwa vitendo ya kupunguza rufaa za nje ambazo serikali ilikuwa ikigharamia fedha nyingi kutokana na kutokuwapo kwa wataalam wa kutibu magonjwa hayo.

"Utekelezaji huu unasaidia wagonjwa kupata huduma sahihi wakiwa hapahapa nchini na kupunguza vifo visivyo vya lazima kwani wakati mwingine ililamizimika wagonjwa hawa kusubiri kwa muda mrefu,’’ anasema Aligaesha.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement