*Matokeo yabainisha sababu.
Na Veronica Romwald, Dar es Salaam
MAGONJWA yasiyo kuwa ya kuambukiza (NCD’s) ni yale ambayo
mtu anapoyapata huwa hawezi kumwambukiza mwingine na ataishi nayo hadi siku
atakapofariki dunia.
Kundi hilo linajumuisha magonjwa ya saratani, magonjwa ya moyo,
magonjwa sugu ya njia ya hewa, seli mundu (sickle cell disease), magonjwa ya
akili na dawa za kulevya, figo, kisukari, ubongo, macho na mengineyo.
Utafiti uliofanywa mwaka 2005 duniani na Shirika la Afya
Duniani (WHO) ulionesha kati ya vifo milioni 58 vilivyokuwa vimetokea, vifo
milioni 35 vilitokana na magonjwa yasiyo kuwa ya kuambukiza.
Nchini Tanzania utafiti uliofanyika katika wilaya nne
kuanzia mwaka 1994 hadi 2002 ulionesha asilimia 18 hadi24 ya vifo vilivyokuwa
vimetokea, vilitokana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
Magonjwa hayo yanatajwa kuchangia asilimia 27 ya vifo vyote
duniani na tafiti zinaonesha yanazidi kuongezeka hasa katika nchi zilizopo
chini ya Ukanda wa Jangwa la Sahara, Tanzania ikiwamo.
WHO linakadiria kuwa asilimia 20 ya vifo vyote vilivyotokea nchini mwaka 2005 vilitokana na magonjwa
yasiyo ya kuambukiza.
Utafiti huo unabainisha magonjwa ya moyo yalichangia vifo
kwa asilimia tisa, saratani asilimia nne, mfumo wa hewa asilimia mbili,
kisukari asilimia moa na magonjwa mengine sugu asilimia nne.
Utafiti wa viashiria vya magonjwa yasiyo ya kuambukiza
uliofanywa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa
kushirikiana na Taasisi ya utafiti wa magonjwa ya binadamu (NIMR) mwaka 2012
ulionyesha kuna ongezeko kubwa la viashiria vinavyosababisha magonjwa yasiyo ya
kuambukiza.
Serikali za nchi mbalimbali sasa zimeelekeza nguvu zake
katika kufanya kampeni kuelimisha jamii kuhusu magonjwa hayo ambayo yanatajwa
kugharimu maisha ya watu wengi.
Magonjwa hayo yanaweza kuepukika kwa watu kuzingatia ulaji
unaofaa, kufanya mazoezi, kupima afya mara kwa mara, matumizi yanayostahili ya
dawa.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu
Changamoto kubwa inayotajwa katika kukabili magonjwa haya
ni gharama kubwa za matibabu ambazo mtu hukabiliana nazo hasa pale anapokuwa
hana bima ya afya.
Mgonjwa
Hamis Ibrahim Mkazi wa Singida anamuuguza mtoto wake ambaye
amefanyiwa upasuaji katika taasisi hiyo hivi karibuni.
“Mwanangu aligundulika kuwa na tatizo la moyo mwaka 2004
kabla ya kufika hapa nilizunguka hospitali nyingi mno lakini tatizo
halikugundulika.
“Hadi pale nilipokwenda katika hospitali moja ya rufaa ipo
huko Manyoni ndiko ikagundulika kwamba ana tatizo, ‘valve’ zake zilikuwa zina-fail kusukuma damu
na moyo wake ulionekana kuwa unatanuka,” anasema.
Anasema awali ilimgharimu fedha nyingi kulipia matibabu ya
mtoto wake huyo ikafika wakati akashindwa kumudu gharama hizo.
“Nilikuwa natumia hadi zaidi ya Sh 200,000 kila nilipomleka kufanyiwa uchunguzi pamoja na dawa, nikashauriwa kukata bima nikakata toto afya
ya NHIF ambayo kidogo naona inanipunguzia mzigo wa gharama za matibabu,”
anasema.
Anaongeza “Nashukuru
serikali naiomba isogeze huduma hizi karibu zaidi na jamii wawasaidie wanaougua
ugonjwa huu wapo mikoani pia wengine hawawei kuja huku, ikiwezekana kila mkoa
upate haya matibabu.
Utafiti
Pedro Pallangyo ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ambaye hivi karibuni amefanya utafiti
kujua hali halisi na changamoto zinazowakabili wagonjwa wa moyo nchini.
MTANZANIA
limefanya naye mahojiano na anaeleza kwa kina kile alichokibaini kupitia
utafiti wake huo, karibu.
Dk. Pallangyo anasema kwa kawaida wagonjwa wanaolazwa
hospitalini hapo hupatiwa dawa zinazostahili kutibu magonjwa ya moyo
yanayowakabili.
“Lakini kati yao wapo ambao wanaporuhusiwa kurejea nyumbani
hushindwa kununua dawa wanazokuwa wameandikiwa na madaktari wanazotakiwa kuzitumia
kipindi chote wanapokuwa nyumbani kabla
ya kurejea tena hospitalini,” anasema.
Anaongeza “Matokeo yake, kama wana tatizo la moyo kushindwa
kufanya kazi, wakilazwa hospitalini huwa na hali nzuri lakini wakirudi nyumbani
hali hubadilika na kuwa mbaya kuliko awali kwa sababu hawatumii dawa.
“Kutokana na hali hiyo wengi hurudishwa hospitalini, kwa
kipindi cha miezi sita tulifanya utafiti huu kwa wagonjwa 459 kuangalia
mwenendo wao wa matumizi ya dawa na mambo mengineyo,” anasema.
Dk. Pedro (anayezungumza pichani) anasema utafiti huo ulihusisha wagonjwa waliokuwa na umri
wa kati ya miaka 46 na kuendelea na kwamba silimia 57 walikuwa wanawake huku
asilimia 43 ikiwa ni wanaume.
“Kati ya wagonjwa hao asilimia 22 walikuwa na bima ya
afya na asilimia 68 walikuwa wakiishi
katika maeneo ya mijini,” anasema.
Matokeo
Dk. Pallangyo ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Utafiti na
Mafunzo wa JKCI anasema katika utafiti huo walibaini asilimia 80 ya wagonjwa
wote 459 waliofanyiwa utafiti huo walikuwa na matumizi mabaya ya dawa.
“Hawakutumia dawa kama inavyotakiwa na walivyokuwa
wameelekezwa na wataalamu na hiyo ilikuwa kisababishi kikubwa kilichochangia
kulazwa mara kwa mara na kuwa kwenye hatari ya kupoteza maisha,” anasema.
Daktari huyo anasema matokeo ya utafiti huo yalibainisha
kwamba asilimia 85 ya wagonjwa waliohojiwa walieleza sababu kubwa
iliyowapelekea kuacha kuzingatia matumizi ya dawa ni kukosa fedha za kununulia
dawa hizo.
“Sababu nyingine ambayo ilitajwa na kushika nafasi ya pili
ilikuwa ni usahaulifu, baadhi ya wagonjwa walieleza kwamba kuna wakati
walisahau kumeza dawa walizoandikiwa,” anasema.
Anasema walitumia tool ya Morsw (kipimo cha kitaalamu)
kinachoshauriwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) katika kufanya tafiti za namna
hiyo.
Sababu
Anasema sababu kubwa ambayo imeonekana kuchangia hali hiyo
ni gharama za ununuzi wa dawa hizo ambapo utafiti unaonesha asilimia 87.3 ya
wagonjwa waliohojiwa walieleza sababu hiyo.
“Kuhusu usahaulifu ilipatikana asilimia 53.9… utaona
matokeo haya hayawezi kuleta jumla ya asilimia 100 na hii ni kwa sababu katika
wagonjwa tuliohoji wengine walikuwa na sababu zaidi ya moja,” anasema.
Dk. Pallangyo anasema kati ya wagonjwa waliohojiwa asilimia
34.4 walieleza kuwa waliacha matumizi ya dawa kutokana na wingi wa dawa
walizokuwa wameandikiwa kwa ajili ya kuzitumia kutibu tatizo walilonalo.
“Yaani kutokana na ule wingi walilazimika kuacha baadhi ya
kupunguza au kupumzika, na asilimia 26 waliacha matumizi ya dawa kutokana na
uzembe,” anasema.
Anasema kwa kupata matokeo hayo walijaribu kuangalia kwa
kina nini hasa vilikuwa visababishi vilivyochangia wagonjwa hao kuwa na
uzingatiaji mdogo wa matumizi ya dawa walizotakiwa kutumia.
“Tulibaini umri haukuwa tatizo, jinsi haikuwa tatizo lakini
kwa upande wa elimu tulibaini kulikuwa na tatizo, wagonjwa waliokuwa na elimu
ndogo (Elimu ya Msingi kushuka chini) walikuwa na uzingatiaji mdogo
kulinganisha na wagonjwa waliokuwa na kiwango cha Elimu ya Msingi na
kuendelea,” anasema.
Anasema kwa upande wa kigezo cha ajira nacho kilikuwa ni
sababu kwani utafiti ulibaini wale waliokuwa hawana ajira ya kuwaingizia kipato
walikuwa na uzingatiaji mdogo wa matumizi ya dawa kuliko waliokuwa na ajira ya
kueleweka.
Anasema kwa mujibu wa matokeo ya utafiti huo wagonjwa
waliokuwa wanaishi katika maeneo ya vijijini tulibaini walikuwa na uzingatiaji
mdogo wa matumizi ya dawa kulinganisha na wale waliokuwa wakiishi mijini.
Anaongeza “Aidha, wagonjwa ambao hawakuwa na bima walikuwa
na uzingatiaji mdogo wa matumizi ya dawa mara nane zaidi ya wale ambao walikuwa
na bima.
“Hivyo vigezo vya msingi ambavyo tuliona vilichangia hali
hiyo, ni elimu duni, tatizo la ajira, makazi wanakoishi na kutokuwa na bima
afya,” anabainisha Daktari huyo ambaye pia ni mshindi wa tuzo ya watafiti
vijana Barani Afrika kwa mwaka 2017.
Hali
mbaya
Dk. Pallangyo anasema katika utafiti huo walienda mbali
zaidi na kuangalia maendeleo ya wagonjwa waliolazwa mara kadhaa baada ya
mahojiano ya awali.
“Tulibaini baada ya mahojiano ya awali, wagonjwa ambao hawazingatii matumizi ya dawa kama
walivyotakiwa wana uwezekano wa kulazwa mara kwa mara huwa ni asilimia 70
kuliko wale ambao huzingatia,” anasema.
Anaongeza “Matokeo yanaonesha pia wagonjwa ambao huwa na
uzingatiaji mbaya wa matumizi ya dawa hali inayopelekea kulazwa mara kwa mara
hospitalini wapo kwenye hatari ya kufariki dunia mara tatu zaidi ya wale
wanaozingatia matumizi sahihi ya dawa.
“Hii tuliibaini baada ya kuwafuatilia kwa ukaribu wagonjwa
hao ambapo kati yao walikuwapo ambao walipoteza maisha ndani ya miezi sita ya
utafiti huu,” anasema.
Dk. Pallangyo anasema kutokana na matokeo ya utafiti huo
inawezekana sababu hizo zinachangia pia vifo vya wagonjwa kwa kutozingatia
matumizi sahihi ya dawa katika magonjwa mengine.
Madaktari wa JKCI na wenzao wa Hospitali ya Apolo, India wakishirikiana kumfanyia upasuaji mgonjwa wa moyo kwa kumuwekea milango miwili ya moyo ya chuma
Umasikini
huchangia?
“Huenda hii inatokea kwa sababu, jamii nyingi bado ni
masikini, kusema ule ukweli bado wananchi hawawezi kumudu gharama za kutibu magonjwa yasiyo kuwa ya
kuambukiza,” anabainisha.
“Ukicha matokeo ya utafiti huu, sasa hivi tunafanya utafiti
mwingine ambapo tayari tumehoji wagonjwa 500 na lengo ni kuwafikia 1,000
tukiangazia hasa kigezo hiki cha gharama na hali ya kipato cha mwananchi.
“Tunatarajia kukamilisha utafiti huu na kutoa matokeo yake
ifikapo Januari, mwakani, lakini kwa kuzingatia utafiti huu tuliokamilisha,
tunaishauri Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja
na wadau mbalimbali wa sekta ya afya kwamba lazima watafute mbinu ama njia
mbalimbali kuhakikisha kila mwananchi anakuwa na bima ya afya.
“Ifike mahali bima ya afya iwe ni haki ya msingi kwa kila
mwananchi badala ya wachache tu kuwa nayo, maana kwa matokeo haya inaonesha
wazi kwamba mtu akiwa na bima ya afya anakuwa hana ‘stress’ za jinsi gani atamudu
gharama za matibabu na dawa,” anasema.
Dk. Pallangyo anaongeza “Lakini pia itafakari jinsi gani
kila mwananchi atakayekata bima ya afya atakuwa analipa kwa sababu sisi
wafanyakazi tunakatwa kwenye mshahara lakini kuna kundi la watu ambao
wamejiajiri wenyewe katika ajira ambazo si rasmi.
“Tunaona pia kuna haja zaidi ya kuwapatia elimu wananchi
kuhusu umuhimu wa kukata bima ya afya na kuzingatia matumizi ya dawa kulingana
na walivyoelekezwa na wataalamu wa afya katika kutibu magonjwa mbalimbali,”
anasema Daktari huyo.
Chapisha Maoni