Na Veronica Romwald, Dar es Salaam
TATOO ni michoro ambayo huchorwa
sehemu mbalimbali katika mwili wa binadamu, vijana ndilo kundi ambalo
hupendelea zaidi kuchora michoro hiyo.
Michoro hiyo hubeba ujumbe mbalimbali
kulingana na matakwa ya wale waliojichora.
Juma Kassim kijana mwenye umri wa
miaka 28 mkazi wa Sinza Kijiweni amechora tattoo ya jina la mwenzi wake
shingoni mwake.
“Nampenda mpenzi wangu niliamua
kuchora tattoo hii shingoni ili kumuonesha jinsi gani nampenda na namthamini,”
anasema.
Kassim anasema hakusudii kuja kuifuta
tattoo hiyo kamwe katika maisha yake.
“Umesema ikiwa itatokea nikaachana na
mpenzi wangu kwamba nitaifuta au la, siwezi kuifuta hata itokee jambo gani, hii
nimeichora itakaa milele katika mwili wangu,” anasema.
Maria Elius anasema yeye amechora
tattoo kwa kuandika jina la mama yake.
“Mama yangu amefariki mwaka 2013
nilijihisi mpweke mno, baba yangu simjui, sijawahi kumuona… nilielezwa na mama
kwamba alimkimbia nikiwa bado sijazaliwa.
“Hivyo, alinikataa nikiwa tumboni mwa
mama, nikaishi bila kumjua baba yangu hadi leo, mama alipofariki nilibaki kwa
babu yangu, mwaka 2015 nikaamua kuchora tattoo hii,” anasema.
Anasema kila anapoitazama tattoo hiyo
aliyoichora katika mkono wake wa kulia anahisi yupo karibu na mama yake.
“Najua si kweli lakini najihisi
vizuri pale ninapomkumbuka naitazama tattoo hii najisikia faraja,” anasema.
Daktari
Hivi karibuni MTANZANIA limefanya
mahojiano maalum na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ngozi wa Hospitali ya Taifa
Muhimbili, Annete Kissongo.
Anasema vijana wengi hupenda
kujichora tattoo katika miili yao bila kujua kwamba zinaweza kuwasababishia
madhara mbalimbali.
“Kwa kawaida, mtu anapochora ile
tattoo mwilini mwake ile rangi huenda moja kwa moja hadi katika sehemu ya ndani
ya ngozi iitwayo dermis,” anabainisha.
Athari zake
Anasema tattoo huweza kusababisha
magonjwa ya maambukizi hasa ikiwa chombo cha kuchorea kitatumika pasipo
kusafishwa vema na kutumiwa na wengi.
“Kile chombo kinachotumika ikiwa
kimetumika kwa kundi kubwa la watu, kama wana magonjwa ya maambukizi kwa mfano
HIV, homa ya ini na mengineyo huwa inaongeza uwezekano wa kuambukizana magonjwa
hayo na mengineyo,” anasema.
Dk. Anette anasema wakati mwingine
mtu huweza kupata maambukizi ya bakteria (bacteria infection).
Anaongeza “Ile rangi inayotumika
kuchora tattoo inaweza kumsababishia muhusika kupata allege (mzio).
Anasema athari huwa kubwa zaidi kwa
muhiska ikiwamo kupata makovu makubwa yasiyokuwa ya kawaida kitaalamu yanaitwa
keloids.
“Makovu hayo huwa makubwa kuliko
kidonda cha kawaida au mchoro wa kawaida wa tattoo, haya hutokea zaidi kwa watu
weusi na huharibu kabisa ule mwonekano wa ngozi ya muhusika,” anabainisha.
Anasema wapo ambao makovu hayo hufika
mahali na kuanza kupungua hata hivyo wengi huwa yanaongezeka ukubwa.
Utafiti
Inaelezwa tattoo inaweza
kumsababishia muhusika kupata saratani.
Hiram Castillo wa Kituo cha Radiation
cha nchini Ufaransa ni miongoni mwa waandishi wa utafiti huo.
Wanasema kwamba kemikali za wino wa
tattoo huweza kusafiri katika damu na kukusanyika katika mfumo wa lymph.
Hali hiyo huufanya mwili kuvimba na
hivyo kuzuia uwezo wake wa kupambana na maambukizi dhidi ya magonjwa
mbalimbali.
Watafiti hao wanataja kemikali ya
titan-dioksaidi ambayo hutumiwa kuunda wino mweupe ni miongoni mwa kemikali
zinazoongeza hatari ya mtu kupata saratani.
“Mtu anapotaka kupata tattoo,
mara nyingi huwa makini sana katika kuchagua sindano ambazo hazikutumika awali
lakini hakuna mtu anayeangalia kemikali ya rangi, lakini utafiti wetu unaonesha
wanapaswa kufanya hivyo,” anasema Castillo.
Wanasayansi hao wa Ufaransa na
Ujerumani walitumia X-rays na kipimo cha fluorescence kuchunguza chembe ndogo,
waliripoti ushahidi mkubwa unaoonesha kwamba wino wa tattoo huzunguka mwili
kabla ya kujenga amana (depostis).
Matokeo ya utafiti huo yamechapishwa
katika majarida mbalimbali pamoja na mtandao wa daily mail Septemba 12, mwaka
huu.
Zinawatesa vijana
Dk Anette anasema katika kitengo
chicho wamekuwa wakipokea vijana wanaohitaji huduma ya kufutwa tattoo
walizojichora mwilini.
Anaongeza “Lakini kwa sasa hapa
Muhimbili hatuna ‘procedure’ ya kufuta tattoo (Laser surgery) na huwa
hazifutiki kirahisi.
“Wanakosa ajira kwa sababu zipo
taaluma ambazo hazipokei watu wenye tattoo au makovu,” anasema.
Chapisha Maoni