Jumatano, 10 Januari 2018

ZIARA YA WAZIRI UMMY KATIKA HOSPITALI YA TAALUMA NA TIBA MLOGANZILA LEO

Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akimjulia hali mmoja wa wagonjwa aliyelazwa katika Hospitali ya Taaluma na Tiba Mloganzila alipotembelea hospitalini hapo mapema leo.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu leo Januari 10 ,2018 ametembelea Hospitali ya Taaluma na Tiba ya Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Cha Muhimbili (MUHAS) kampasi ya Mloganzila iliyofunguliwa rasmi  na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli Novemba 25 ,2017  .

Lengo la kutembelea hospitali hiyo ni kuangalia utoaji wa huduma za afya zinazotolewa katika hospitali hiyo.
 Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akimjulia hali mmoja wa wagonjwa aliyelazwa katika Hospitali ya Taaluma na Tiba Mloganzila alipotembelea hospitalini hapo mapema leo.

Baada ya kutembelea hospitali hiyo Waziri Ummy ameagiza Idara yote ya magonjwa ya ndani (Internal Medicine) iliyopo hospitali ya Taifa ya Muhimbili kuhamia mara moja katika hospitali hiyo wakiwemo Madaktari,Madaktari Bingwa,Wauguzi pamoja na wataalmu wengine wa idara hiyo.

Wakati huo huo Waziri Ummy ameagiza kuhamisha wagonjwa waliopo wodi namba 3,4,5,6,7 na 8 zilizopo kwenye jengo la Mwaisela Muhimbili na kupelekwa hospital ya Mloganzila isipokuwa wagonjwa walio mahututi na wenye sababu maalumu na baada ya kuondoka wagonjwa hao wodi hizo zifanyiwe ukarabati mara moja.
 
Waziri Ummy akizungumza na waandishi wa habari

“Nawaagiza waganga wafawidhi wa hospitali za Rufaa za Temeke,Mwananyamala na Amana kuanzia sasa rufaa zote za wagonjwa wa magonjwa ya ndani zije Mlongazila”, Alisema Mhe.Ummy.

Aidha, Waziri Ummy alisema Wizara imeshapokea Hospitali za Rufaa za Mikoa kutoka TAMISEMI hivyo amemuagiza Katibu mkuu wa Wizara hiyo kukamilisha kuwapangia baadhi ya Madaktari Bingwa waliopo hospitali hiyo ya Taifa na kuwapeleka hospitali za Rufaa za Mkoa na Kanda mapema Februari mwaka huu.

“Tumeomba kibali Utumishi wa Umma ili kuwahamisha Madaktari Bingwa zaidi ya ishirini (20) waliopo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) pamoja na mishahara yao,”Madaktari wetu ni Wazalendo wapo tayari kwenda kutoa huduma za matibabu ya kibingwa kwenye hospitali zetu za Mikoa na Kanda”.
 
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo na Hospitali hiyo, Prof. Said Aboud akiwafafanulia jambo waandishi wa habari wakati wa ziara hiyo.

Alisema Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kwa dhati kuwahudumia wananchi wote ikiwemo kupata huduma za matibabu ya kibingwa bila kubagua hivyo Wizara yake imejipanga kununua vifaa na vifaa tiba na kuvisambaza kwenye hospitali hizo za rufaa za Mikoa.

Alitaja Madaktari bingwa watakaohamishiwa kwenye hospitali za rufaa za mikoa na kanda miongoni mwao ni wa Magonjwa ya akina Mama na  Uzazi, Watoto,Upasuaji wa jumla,Radiolojia,Usingizi Macho pamoja na Magonjwa ya ndani.
Waziri Ummy akiwa ameambatana na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo na Huduma za Hospitali hiyo, Prof Aboud wakati wa ziara hiyo.

Mloganzila ni Hospitali ya Taaluma na Tiba ambayo imewekwa vifaa tiba vya kisasa na teknolojia ya hali ya juu na ina vitanda 571 vya kulaza wagonjwa  na vyumaba 13 vya upasuaji na inatoa huduma masaa ishirini na nne.

Imetolewa na

Catherine Sungura
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini- Afya
10/1/2018.

Picha zote na Alvin Daudi