Picha na mtandao
NA
VERONICA ROMWALD - DAR ES SALAAM
SARATANI
ya mlango wa kizazi hutokana na mabadiliko ya ukuaji usio wa kawaida wa
chembe-chembe au seli za mlango wa uzazi.
Mabadiliko
hayo husababisha chembe-chembe hizo kushamiri na kukua kwa kasi kinyume na
mpangilio wa maumbile, husababisha misuli au viungo vingine vya mwili
kuathirika.
Saratani
hiyo huweza kusambaa na kushambulia viungo vingine ikiwamo kibofu cha mkojo,
uke na sehemu ya chini ya utumbo mkubwa na baadaye figo, ini na viungo vingine
vya mwili.
Shirika
la Afya Duniani (WHO) linaeleza kwamba saratani ya shingo ya kizazi inazidi
kuwa tishio duniani kwa kusababisha vifo vya wanawake wengi.
Linakadiria
kila mwaka wanawake zaidi ya 400,000 hugundulika kuwa na saratani hiyo Duniani.
Chanzo ni
kirusi.
Kirusi
cha Human Pappiloma (HPV) ndicho ambacho husababisha saratani hii, inaelezwa
kirusi hiki hubebwa katika mwili wa mwanaume.
Daktari
Bingwa wa Magonjwa ya Saratani wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI),
Crispin Kahesa anasema kirusi hicho huingia mwilini mwa mwanamke wakati wa
kujamiiana.
"Ingawa
kirusi hiki kinabebwa na mwanaume hata hivyo anayeathirika ni mwanamke hasa
wale ambao huanza kushiriki ngono mapema," anasema.
Kwanini
Anasema
kitaalamu kirusi hicho huchukua muda wa miaka 10 hadi 20 kuanza kuonesha athari
zake tangu kilipoingia katika mwili wa mwanamke.
“Ndiyo
maana si rahisi kuona athari mara moja, mwanamke anayeanza kushiriki ngono
mapema athari zitaonekana baada ya miaka 10 hadi 20 tangu apate maambukizi
hayo," anasema.
Tafiti
Tafiti
zinaonesha wanawake wengi nchini huanza kuonesha dalili za ugonjwa huo
wanapofikisha umri wa miaka 40 na kuendelea.
Inadhaniwa
kwamba huenda wengi kati yao walianza kushiriki ngono wakiwa na umri wa miaka
25 kushuka chini.
Inaelezwa
wasichana wanaoshiriki ngono na wanaume wengi wapo kwenye hatari zaidi ya
kupata ugonjwa huo kuliko wale wanaoshiriki na mwanaume mmoja.
Ushuhuda
wa mgonjwa
Sophia
Mgimba (43) Mkazi wa Mbeya mama wa watoto sita ni miongoni mwa wanawake
wanaotibiwa ugonjwa huo ORCI.
Anasema
January, mwaka jana alianza kupata maumivu makali ya tumbo na kumwagika damu
katika sehemu zake za siri.
"Nilienda
katika Hospitali ya Meta kule Mbeya kupata matibabu, walichukua kinyama
wakakileta huku Ocean Road kwa uchunguzi zaidi," anasema.
Anasema
majibu ya vipimo yalionesha kwamba ana tatizo la saratani ya shingo ya kizazi.
"Nikapewa
rufaa pale Meta kuja Ocean Road kwa matibabu zaidi ya kibingwa, sikuwa na fedha
za safari, nilisaidiwa na hospitali hiyo pamoja na ndugu zangu," anasema.
Sophia
anasema haikuwa rahisi kwake na mumewe kupokea majibu hayo kwani yalionesha
kwamba saratani hiyo ilikuwa inasambaa kwenda kwenye kibofu cha mkojo.
"Mume
wangu alifadhaika mno na mimi niliumia mno kwa majibu hayo lakini nikajipa moyo
ipo siku nitapona ikiwa Mungu ameamua niishi," anasema.
Anaongeza
"Katika familia yetu baba yangu aliugua saratani ya koo na Kuna baba yangu
mdogo aliugua saratani ya mguu, wote wamefariki dunia kwa sababu walichelewa
matibabu.
Imani
potofu
Anasema
wodini huwa wanasimuliana kuhusu magonjwa ya saratani yanayowakabili.
"Umeona
kuna wengine wamefika hali zao si nzuri, wengi wanasema wamezunguka sehemu
mbalimbali kutibiwa kwa waganga wa kienyeji wakiamini wamerogwa.
"Simulizi
za imani juu ya kurogwa ni nyingi matokeo yake wanakuja hospitalini wakiwa
wamechelewa," anasema.
Anaongeza
"Nashukuru mimi nimewahi matibabu, sasa hali yangu ni nzuri na namwamini
Mungu najua nitapona kabisa.
Visababishi
Daktari
Bingwa wa Magonjwa ya Saratani ORCI, Maguha Stephano, anasema vipo visababishi
vingi ambavyo huchangia mwanamke kupata saratani hiyo.
"Uvutaji
wa sigara, kuanza ngono mapema, ndoa za mitala na kuwa na wapenzi wengi ni miongoni
mwa visababishi," anabainisha.
Dk.
Maguha anaongeza "Sigara ni kisababishi kikuu cha magonjwa mengi ya
saratani, wanawake wanaoishi na maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) wana
hatari zaidi ya kupata saratani ya shingo ya kizazi kuliko wale wasiougua
ugonjwa huo.
Picha inaonesha hatua mbalimbali za saratani ya shingo ya kizazi inavyotokea (na mtandao)
Kuna aina
zaidi 40 ya virusi
Wataalamu
wanasema zipo aina zaidi ya 40 za virusi vya HPV ambavyo vinaweza
kusababisha maambukizi kwenye njia za uzazi za wanaume na wanawake na katika
sehemu za mdomoni na kooni.
Wanasema
hata hivyo aina ya 16 hadi 18 ndizo ambazo husababisha saratani zote za mlango
wa kizazi duniani kwa asilimia 70.
Wanasema
wanawake wengi duniani wanaopata maambukizi ya virusi hivyo huwa hawapati
saratani isipokuwa asilimia 10 tu ndio ambao huonesha dalili za awali za ugonjwa
huo baada ya miaka 10 hadi 20 tangu wapate maambukizi.
Wanasema
inaaminika asilimia 70 ya watu duniani hupata maambukizi ya virusi hivyo hiyo
inamaanisha watu saba kati ya 10 walishapata virusi hivyo katika maisha yao.
Hata
hivyo wanasema maambukizi ya HPV huwa hayaoneshi dalili zozote na huweza
kusababisha mtu kupata ugonjwa wowote na kwamba asilimia 10 ya walioambukizwa
hubaki na virusi hivyo mwilini.
Hali
halisi
Magonjwa
ya saratani ni tishio hivi sasa nchini, Shirika la Afya Duniani (WHO) linakadiria
kila mwaka takriban wagonjwa wapya 50,000 hugundulika kuwa na aina mbalimbali
za saratani.
WHO
linaeleza kati ya wagonjwa wapya wanaogundulika, 13,000 pekee sawa na asilimia
26 hufanikiwa kufika hospitalini kwa matibabu.
Kwa
mujibu wa Shirika hilo, asilimia 70 ya wagonjwa hufika wakati ugonjwa ukiwa
umefika hatua za juu za mwisho yaani tatu na nne ambazo ni ngumu kupona.
Takwimu
za ORCI
Mkurugenzi
Mtendaji wa ORCI, Dk. Julius Mwaiselage anasema mwaka 2016/17 takwimu
zinaonesha saratani ya shingo ya kizazi na ya matiti ndizo zinaongoza kwa idadi
kubwa ya wagonjwa.
"Saratani
ya shingo ya kizazi inaongoza kwa asilimia 32.8, matiti asilimia 12.9
zikifuatiwa na satatani ya ngozi (Kaposis Sarcoma) asilimia 11.7, kichwa na
shingo asilimia 7.6, matezi asilimia 5.5, damu asilimia 4.3.
"Nyingine
ni saratani ya kibofu Cha mkojo asilimia 3.2, ngozi asilimia 2.8, macho
asilimia 2.4 na tezidume asilimia 2.3," anabainisha.
Waziri Ummy Mwalimu
Mpango wa
chanjo
"Saratani
ya shingo ya kizazi inaweza kuepukwa iwapo mtu atajiepusha kushiriki ngono
mapema, kuwa na mwenzi mwaminifu, kubeba ujauzito katika umri mdogo, kutumia
kondomu na kuepuka uvutaji sigara," anasema Meneja Mpango wa chanjo Taifa,
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Dafrosa Liymo.
Anaongeza
"Inazuilika kwa kutumia chanjo maalum ya HPV ambayo huchanjwa wasichana
ambao bado hawajaanza kushiriki ngono.
"Serikali
inatarajia kuanza utekelezaji wa mpango wa chanjo hii kuanzia April 25, mwaka
huu, kwa mwaka huu watachanjwa wasichana wenye umri wa miaka 14, lakini kuanzia
mwakani watachanjwa kuanzia miaka tisa hadi 14," anasema.
Anasema
lengo ni kukabiliana ili kupunguza idadi ya vifo vitokanavyo na saratani hiyo
pia kuzipunguzia familia na serikali mzigo mkubwa wa gharama za matibabu.
Zipoje?
Waziri wa
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu anasema
serikali hugharamia kiasi cha Sh milioni 5.5 kumtibu mgonjwa mmoja wa saratani
kila mwaka ORCI.
"Ni
gharama kubwa mno tunatumia kutibu lakini kumkinga msichana mmoja tutatumia Sh
30,000 tu, hivyo tunaona ni muhimu mno kuwakinga," anasisitiza.
Anaongeza
"Tuliwasilisha andiko katika Shirika Gavi la Chanjo Duniani na
likakubaliwa, wametufadhili pia serikali imewekeza kiasi cha Sh milioni
800 katika mpango huu.
Kuhusu
usalama/ubora
Anasema katika mwaka 2014 jumla ya wasichana 135,700 mkoani
Kilimanjaro walichanjwa na kwamba imeonesha mafanikio kwa kiwango cha zaidi ya
asilimia 70.
"Maandalizi ya kuanza rasmi awamu ya kwanza ya chanjo
yamekamilika, dozi hutolewa kwa awamu mbili tunakusudia kuwafikia wasichana
616,734 wenye umri wa miaka 14.
Je watawajuaje?
Ni swali ambalo wengi wanajiuliza, kwamba watajuaje wasichana
ambao hawajaanza kushiriki ngono, je watawakagua au watatumia mbinu gani?.
Dk. Maguha anasema hawatawakagua kama wengi wanavyodhani na
wanaamini wasichana wengi katika umri huo bado hawajaanza kushiriki ngono.
"Tutashirikiana kwa ukaribu na walimu na wazazi wao
katika utoaji wa chanjo hii, tutawapatia wasichana wote walio katika umri huo
ili kuwakinga dhidi ya saratani hii," anasema.
Wito
Waziri Ummy anawasihi wananchi kutokuwa na hofu juu ya chanjo hi
kwani WHO na Mamlaka ya Udhibiti wa Chakula na Dawa Tanzania (TFDA)
imeithibitisha ni salama na haina madhara kwa binadamu.
"Mimi nitakuwa wa kwanza kumchanja mwanangu siku
hiyo," anasema.
Kauli ya WHO
Mwakilishi wa WHO Tanzania, Ritha Njau anaipongeza serikali kwa
hatua hiyo na kusisitiza kwamba Shirika hilo litaendelea kushirikiana nayo bega
kwa bega katika utekelezaji wa mpango huo.
Chapisha Maoni