Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement
Picha na mtandao

NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

MACHI nane, kila mwaka dunia huadhimisha mambo makubwa mawili ambayo ni Siku ya Wanawake Duniani na Siku ya Figo Duniani.

Maadhimisho ya Siku ya Figo Duniani mwaka huu yamepewa kauli mbiu isemayo 'Figo na  Wanawake, Tuwashirikishe, Tuwaheshimu na Tuwawezeshe'.

MATUKIO NA MAISHA imefanya mahojiano ya kina na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Vincent Tarimo.

Anasema magonjwa ya figo kwa wanawake yanaweza kuwekwa katika makundi makubwa mawili.

Anasema yapo magonjwa ambayo yanahusiana na ujauzito yanayoweza kuchangia kuua figo na yapo ambayo hayahusiani na ujauzito yanayoweza pia kuchangia kuua figo.

"Katika haya yanayohusiana na ujauzito, upo ugonjwa wa 'Severe pre eclampsia', huu ni ugonjwa ambao husababishwa na shinikizo la damu na iwapo mjamzito haudhurii kliniki kufuatiliwa hali yake, shinikizo la damu huendelea kuongezeka na kuwa kali (la juu) zaidi.

"Ikiendelea zaidi huleta athari nyingi mwilini ikiwamo kifafa cha mimba, huathiri figo kidogo kidogo na akichelewa matibabu figo zake hufa kabisa," anasema.

Anasema huweza pia kusababisha kutokwa na damu nyingi wakati wa kujifungua au kondo la nyuma kukatika na kuachia kabla ya uchungu wa uzazi kuanza au njia ya uzazi kufunguka.

"Damu hutoka kwa wingi, kutokana na hali hiyo yale mapigo na usambazaji wa damu kwenda kwenye figo kupungua.
"Ikiwa huyu mjamzito hatawahishwa hospitalini mapema na kuhudumiwa haraka anaweza kupoteza figo zake (hufa)" anasisitiza.
 Related image
Hali halisi MNH

Daktari huyo anasema mara nyingi tatizo la shinikizo la juu la  damu huchangia kondo la nyuma ingawa si kwa wajawazito wote.
 
"Yaani wapo wajawazito ambao kondo huweza kuachia kutokana na  sababu nyinginezo bill kuwa na shinikizo la juu la damu.

"Katika 'adimission' ya wanaolazwa  hapa Muhimbili wodi namba 35 ambayo ni maalum kwa wagonjwa wenye shinikizo la juu la damu kwa siku huwa ni wastani wa mtu mmoja hadi watano," anabainisha.

Wengi huchelewa

Anasema ni rahisi kukabili tatizo hilo ikiwa mjamzito atawahi kliniki mapema kwani wataalamu watafuatilia kwa ukaribu hali yake.

Anasema hata hivyo, changamoto ni kwamba wengi hufika wakiwa wamechelewa.

"Unakuta tayari zile  athari zinakuwa zimeanza kujitokeza ikiwamo huko 'kupachuka' kwa kondo la nyuma," anasema.

Anasema ni muhimu mjamzito kuwahi hospitalini au kituo cha afya haraka hasa anapoona damu inatoka ukeni.

"Si dalili nzuri kwani damu huendelea kuvuja ndani kwa ndani, akiwahishwa atatibiwa haraka ili figo zake pia zisiathirike ila akichelewa maana yake zitaathirika na hatimaye kufa," anasema.

Nini husababisha

Dk. Tarimo anasema mwanamke anaweza kupata shinikizo la juu la damu kwa kurithi kwenye familia au kutokana na uzazi.

"Kuna vitu vingine vinafikirika kwa mfano mama kubadili mume wengine hupata tatizo hilo, kitaalamu tunasema anapata tatizo la 'auto immune' hivyo mwili wake unajikuta 'una-react'.

"Pia unaweza kukuta mwingine mimba ya kwanza hakuwa na tatizo lakini likajitokeza katika mimba ya pili, ya tatu na kuendelea," anasema.

Daktari huyo anasema wapo pia ambao hupata tatizo bila kuwapo sababu yoyote na wapo wanaopata kutokana na sababu za kimaumbile.

"Zipo tafiti ambazo zinaeleza hayo lakini bado huwezi kusema moja jumlisha moja ni mbili, yaani huwezi kusema hasa kwamba hii ndiyo kisababishi.

"Kwa mfano zipo tafiti zinaeleza kukaa maeneo ya ukanda wa Pwani ambako kuna mbu wengi husababisha malaria na kifafa cha mimba na ukiangalia sana magonjwa ya kifafa cha mimba yanavyosababisha na tatizo hilo yapo sana ukanda wa Pwani.

"Lakini katika maeneo yenye baridi, Kilimanjaro, Kagera na kwingineko kiwango kipo chini sana, hivyo wanajaribu kufikiria kwanini ukanda wa Pwani tatizo lipo juu," anasema.

Anasema tatizo hilo huweza kuathiri viungo vingine vya mwili ikiwamo macho, husababisha ugonjwa wa kiharusi, moyo na hata mapafu kujaa maji.
 Human Kidney Canvas Print - Human Kidneys by Sciepro
Madhara zaidi

Anasema tatizo hilo huweza humsababishia mama kupata tatizo jingine la kuvuruga siku za hedhi, mimba kuharibika au kushindwa kabisa kushika mimba.

"Ili kuokoa figo za mama kama amekaribia kujifungua tunamsaidia kumkomaza mtoto aliye-tumboni na kumzalisha (njiti).

Maamuzi magumu

Dk. Tarimo anasema wakati mwingine iwapo mjamzito anakuwa amefikishwa hospitalini akiwa na hali mbaya huwalazimu kuharibu mimba  ili kuokoa maisha yao.

"Tunapotoa huduma kipaumbele chetu huwa mama na mtoto, nia yetu ni kuhakikisha tunawafikisha salama wote wawili.

"Lakini ikifika lazima tuchague mmoja abaki, huwa tunalazimika kumchagua mama kwa sababu tukichagua mtoto na mama akafa, lazima ujiulize huyu mtoto atalelewa na nani!

"Hivyo tukiona ugonjwa unaelekea kumuathiri mama na hajakaribia kujifungua inatulazimu kuitoa mimba hiyo ili tuokoe maisha ya mama.

"Kumbuka awali nimesema 'pressure' kali inaweza kusababisha matatizo mengine ikiwamo kifafa cha mimba na hata kuua figo za mama," anasisitiza.Image result for dk tarimo muhimbili hospital
Dk. Tarimo (pichani) anaongeza "Ujauzito pekee huongeza athari katika mwili wa mama, katika kipindi hicho mwili wake hutengeneza maji mengi.

"Ndiyo maana wengi huvimba mwili, kwa sababu ya mwili hutengeneza maji mengi, sasa kama mama ana tatizo la figo maana yake ile volume ya maji huwa kubwa zaidi mwilini halafu haitoki, hivyo huongeza uwezekano wa kuiua zaidi zile figo.

"Kutokana na hali hiyo wengi ambao wanakabiliwa na magonjwa ya figo huwa tunawashauri wasishike ujauzito kwa wakati huo kwani madhara huongezeka zaidi, ni muhimu watibiwe kwanza hadi watakapopona ndipo washike ujauzito," anasema. 

Magonjwa mengine

Anasema yapo magonjwa mengine ambayo hayahusiani na ujauzito yabayosababisha tatizo la figo kwa wanawake ikiwamo saratani ya shingo ya kizazi.

"Asilimia 30 hadi 40 ya wagonjwa waliopo wodini hapa Muhimbili idara ya kinamama ni wa saratani ya shingo ya kizazi, saratani hii inapozidi kuenea huenda kuathiri mirija ya mkojo, hushindwa kushuka kwenye kibofu, mkojo unaporudi nyuma huathiri zile figo na kufa," anasema.

Anaongeza "Kina mama wanakufa si kwa sababu ya saratani bali wanakufa kutokana na ile sumu kuwa nyingi mwilini na figo kufa.

Changamoto

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Figo Muhimbili, Jaqueline Shoo anasema hata baada ya kusaidiwa kujifungua wengi hujipata figo zao zimeumia kwa sehemu kubwa.

"Kila wiki tunapokea angalau mama mmoja katika Idara ya Magonjwa ya figo ambaye amepata athari kutokana na mambo mbalimbali ikiwamo tatizo la shinikizo la damu na ajali za mimba," anabainisha.

Dk. Shoo anasema iwapo mama hatapata matibabu sahihi kwa wakati hujipata viungo vyake vingine vya mwili navyo vikiathirika.

"Akiwahi matibabu anapona kabisa lakini wapo ambao tunawapokea tatizo limekuwa kubwa... Tayari unakuta ini limeathirika, mapafu, ubongo na hivyo kupoteza maisha.
"Tunajitahidi kuwafanyia huduma ya 'dialysis' (kuchuja damu) lakini bado unakuta wamebaki na figo zenye majeraha," anasema.

Anaongeza 'Asilimia kubwa ya wanawake wanaofanyiwa huduma hii wanapata changamoto ya kushika ujauzito na hata wakishika mimba huwa 'zinaporomoka'.

Anasema kutokana na hali hiyo wengi huhitaji kufanyiwa huduma ya upandikizaji figo.

"Hata hivyo kuna changamoto si tu Tanzania bali duniani kote, inaonesha wanawake huwa hawapati wachangia figo kama ilivyo  kwa wanaume, bado haijulikani sababu hasa ni nini.

"Hata hapa nchini katika watu 250 waliopandikizwa figo, wengi ni wanaume ingawa wanawake ndiyo ambao hujitolea mno kuchangia figo," anabainisha.


Dalili za tatizo

Dk. Shoo anasema mara nyingi hufanana na dalili za magonjwa mengine ikiwamo malaria.

"Ndiyo maana tunashauri watu wafanye uchunguzi wa afya mara kwa mara ni muhimu pia kupimwa mkojo kama kuna tatizo ni rahisi kubaini kwani mtaalamu ataona umeanza kuwa na chembe-chembe za damu," anasema.

Anataja dalili zingine ni kuhisi kichefuchefu, kuwashwa na kuvimba mwili hasa miguuni, kukojoa mara kwa mara hasa nyakati za usiku kuliko asubuhi, aliyejifungua ataona kiwango cha mkojo wake kimepungua.

VVU na homa ya ini

Anasema magonjwa ya maambukizi hasa VVU yanapogundulika mapema na mgonjwa kupata matibabu husaidia kumwepusha virusi hivyo kusambaa na kuathiri figo zake.

"Virusi Vya Ukimwi vinaweza kusafiri hadi kwenye figo eneo la glomerular (vichujio) na kushambulia," anabainisha.

Anasema virusi vya homa ya ini navyo vinaweza kushambulia figo.
 
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Figo wa Muhimbili Jaqueline Shoo akifafanua jambo mbele ya waandishi wa habari hivi karibuni kuhusu upasuaji wa kwanza waliofanya wa kupandikiza figo.

 Huathiri saikolojia

Dk. Shoo anasema magonjwa ya figo ni janga duniani husababisha athari za kisaikolojia, jamii na kiuchumi.

"Tunashauri watu wajenge utamaduni wa kupima afya zao, wakate bima ya afya kwani matibabu ni gharama kubwa pia serikali isogeze huduma za 'dialysis' karibu zaidi na wananchi," anasema.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement