Na Veronica Romwald, Dar es Salaam
TAASISI ya Saratani Ocean Road itapatiwa kiasi cha Sh bilioni
14.5 katika mwaka ujao wa fedha ili iweze kununua mashine ya kisasa ya Pet Scan
yenye uwezo wa kutibu magonjwa ya saratani.
Hayo yalielezwa Dar es Salaam jana na Naibu Waziri wa Wizara ya
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile
alipofanya ziara katika Taasisi hiyo.
“Nimeridhika huduma ni nzuri wanazotoa, tunakusudia katika mwaka
ujao wa fedha kuwaongezea bajeti, ttutawapa kiasi hicho cha fedha ili wanunue
mashine hiyo kusudi matibabu ya kibingwa dhidi ya magonjwa ya saratani
yapatikane hapa hapa nchini,” alisema.
Alisema tayari hospitali hiyo ilipatiwa fedha imenunua mashine ya CT
simulator Linac ambayo nayo inatibu kwa kiwango cha kisasa na kibingwa magonjwa
ya saratani.
“Tuliwapatia zaidi ya Sh. bilioni 9.5 kununua mashine hiyo,
hatua hii inaifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza Barani Afrika kuwa na mashine
hiyo yenye uwezo wa juu katika kutibu magonjwa ya saratani,” alisema.
Aliongeza “Tunataka ifikapo April, mwaka huu mitambo hii iwe
imekamilika ili ianze kutoa huduma, nimeridhika pia na hali ya majengo
wamejitahidi mno vile vile hali ya upatikanaji dawa ni nzuri.
“Lakini kwa upande wa tiba ya mionzi kuna changamoto, mashine
moja imeharibika na wamesema kifaa kimefika, nimeagiza ndani ya wiki hii
itengenezwe ili ifanye kazi kuondoa msongamano uliopo wa wagonjwa,” alisema.
Aliwataka ORCI kukusanya takwimu za wagonjwa wa saratani nchi
nzima ili serikali iweze kujua idadi yao, wapi walipo na aina gani ya satatani
wanaugua.
“Tunataka tuwatambue hiyo itatusaidi serikali tuwe thabiti
kuweza kuwahudumia wagonjwa hawa,” amesisitiza.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa ORCI, Dk. Julius Mwaiselage alisema hivi
sasa mafundi wa taasisi hiyo wanaendelea na shughuli ya ufungaji mashine hiyo.
Chapisha Maoni