Katika sehemu ya pili tumeona namna ambavyo gharama za matibabu ni changamoto kwa wagonjwa wa moyo na figo, katika makala haya nitagusia gharama za matibabu dhidi ya saratani na mambo mengine mengi... endelea.
Na Veronica Romwald, Dar es Salaam
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,
Ummy Mwalimu anasema kwa upande wa matibabu ya saratani serikali hutumia
wastani wa Sh. milioni 5.5 kila mwaka kumtibu mgonjwa mmoja wa saratani Ocean Road.
“Ni gharama kubwa mno, zinatumika lakini hatuwezi kuacha kulipa
kumtibu Mtanzania, lazima tumtibu, lakini tunaona ni vema tujikite katika
kukinga wananchi wasipate magonjwa haya ambayo mengi yanaweza kuepukwa kwa watu
kuviepuka vile vihatarishi,” anasema.
Mzigo kwa serikali
Gharama za matibabu hasa kwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza licha
ya kuwa ni mzigo kwa jamii sasa zinaonekana wazi kuielemea Serikali.
Sasa imeanza kuchukua hatua na kuwekeza nguvu kubwa katika
kuielimisha jamii jinsi ya kuepukana na magonjwa hayo.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza wa
Wizara hiyo, Dk. Sarah Maongezi anasema hata
hivyo inahitajika nguvu ya pamoja kufikia lengo hilo.
“Serikali tunahitaji kushirikiana bega kwa bega na wadau
mbalimbali wa masuala ya afya wakiwamo waandishi wa habari hasa katika
kuelimisha jamii namna ya kuepukana na magonjwa haya,” anasema.
Waziri Ummy anasema matibabu dhidi ya magonjwa
hayo yamegawanyika katika makundi makuu mawili, kwamba kuna wagonjwa ambao
hutibiwa kwa dawa maalum na wengine huhitaji upasuaji.
“Kwa mfano wa saratani wale hutibiwa kwa dawa
na mionzi pamoja na wanaougua kisukari lakini kwa wagonjwa wa moyo, figo na
maradhi mengineyo matibabu yao ukijumuisha dawa huwa pia wanatibiwa kwa
kufanyiwa upasuaji,” anabainisha.
Anaongeza “Kwa matibabu ya saratani pekee
tunatumia takriban Sh. bilioni saba kwa ajili ya kununua dawa kila mwaka, hapo
hatujajumuisha gharama zingine za watumishi, umeme, maji na nyinginezo.
“Kumtibu mgonjwa mmoja wa moyo tulilazimika
kutumia zaidi ya Sh. milioni 80 mgonjwa mmoja anayehitaji upasuaji wa kutibu
ugonjwa wa moyo nje ya nchi.
“Ndiyo maana serikali iliamua kuwekeza Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ili kuokoa fedha nyingi ambazo zilikuwa
zikitumika kutibu wagonjwa nje ya nchi,” anasema.
Sera ya
msamaha ‘kikwazo’
Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Profesa Mohamed Janabi anasema pamoja
na mafanikio ambayo Taasisi hiyo ya umma inayochunguza na kutibu magonjwa ya
moyo imeyapata, sera ya msamaha inawapa changamoto kubwa.
Anasema miongoni mwa wagonjwa wanaopokelewa kliniki asilimia 38 hutibiwa
kwa bima, asilimia 17 huchangia huduma na kwamba asilimia tano pekee hutibiwa
kwa kulipia gharama (cash).
“Kati ya wagonjwa wote tunaowatibu, asilimia 40 huwa ni wagonjwa
wa msamaha, kusema ukweli huu ni mzigo mkubwa kwa hospitali na serikali kwa
ujumla.
“Kwa sababu, uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo ni
gharama kubwa mno hasa pale tunapohitaji vifaa kwa mfano vile vya kupandikiza
(pacemaker), huwa tunavinunua kwa kuagiza nje ya nchi ambako vinauzwa gharama
kubwa mno,” anasema.
Ushauri
Dk. Pallangyo anasema kulingana na
matokeo ya utafiti waliofanya wanaishauri Wizara na wadau mbalimbali wa sekta
ya afya nchini kutafuta mbinu zitakazosaidia kuhakikisha wananchi wanakuwa na
bima ya afya.
“Ifike mahali bima ya afya iwe ni haki
ya msingi kwa kila mwananchi badala ya wachache tu kuwa nayo, maana kwa matokeo
haya inaonesha wazi kwamba mtu akiwa na bima ya afya anakuwa hana ‘stress’ za
jinsi gani atamudu gharama za matibabu na dawa,” anasema.
Dk. Pallangyo anaongeza “Lakini pia
itafakari jinsi gani kila atakayekata bima ya afya atakuwa analipa kwa sababu
sisi wafanyakazi tunakatwa kwenye mshahara lakini kuna kundi la watu ambao
wamejiajiri wenyewe katika ajira ambazo si rasmi.
“Tunaona pia kuna haja zaidi ya
kuwapatia elimu wananchi kuhusu umuhimu wa kukata bima ya afya na kuzingatia
matumizi ya dawa kulingana na walivyoelekezwa na wataalamu wa afya katika
kutibu magonjwa mbalimbali,” anasema Daktari huyo.
Kauli ya serikali
Waziri Ummy anakiri kwamba sera hiyo ni changamoto hasa katika
utekelezaji wake kwani kwa wastani asilimia 40 ya wagonjwa wanaotibiwa katika
taasisi zake ni wa msamaha.
“Tunajumuisha makundi maalum pia wakiwamo wajawazito, watoto
wenye umri wa chini ya miaka mitano na wazee wasiojiweza, hivyo tunalazimika
kuhakikisha tunapeleka bajeti ya dawa na baadhi ya vifaa tiba katika taasisi
zetu.
“Lakini, kweli mzigo unakuwa mkubwa, kwa msingi huo kwenye sekta
ya afya tunakusudia kuja na mkakati wa kugharamia huduma za afya (Health Sector
Financing), ambao utabainisha vyanzo mbalimbali vya mapato vitakavyogharamia
huduma za afya nchini,” anasema.
Vyanzo vyenyewe
Anataja chanzo kimoja wapo ni bima ya afya kwa kila Mtanzania na
kwamba hilo litakapopitishwa na Bunge itamlazimu kila mmoja kuwa nayo.
“Tulichoamua kufanya ni kwamba ndani ya huo mkakati kuna
mapendekezo ambayo yanayohusu Wizara ya Fedha (Hazina) na mengine yatahusu
wananchi moja kwa moja hasa kuchangia gharama kabla ya kupata matibabu yaani
kukata bima ya afya.
“Tunakusudia April, mwaka huu tutafanya kikao huko mjini Dodoma na
wabunge pamoja na wadau wa maendeleo kutoka Benki ya Dunia (WB) ili sasa waweze
kuupitia mkakati wetu tulioandaa na wao watoe maoni yao ili baada ya hapo
tuuwasilishe katika Baraza la Mawaziri kabla haujaenda tena Bungeni,” anasema.
Anaongeza “Katika uandaaji wa mkakati huu, tuliangalia mfano
katika nchi zingine ikiwamo Ghana ambao wao katika ile VAT (Kodi ya Ongezeko la
Thamani) kuna asilimia fulani ambayo hiyo ni lazima iingizwe katika kuchangia
huduma za afya.
“Afrika Kusini wenzetu wana mfumo wanauita ‘sin-taxes’ yaani kwa
zile bidhaa na huduma ambazo kwa namna moja au nyingine zina athari kwa
binadamu kwa mfano sukari, disko, sigara, vilevi na nyingine za namna hiyo kuna
kiasi fulani cha fedha kupitia kodi kinakatwa na kwenda kuchangia huduma za
afya,” anabainisha.
Chanzo kingine
“Sasa hivi ukienda pale Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI)
takriban asilimia 50 ya wagonjwa wanaopokelewa na kutibiwa wengi ni wa ajali
hasa za bodaboda na zile za magari.
“Kwa hiyo, hivyo tumeona chanzo kingine ambacho tunaweza kupata
fedha ya kuchangia huduma za afya, ikiwa wenzetu watakubaliana nasi, ni
kutokana na kodi za leseni.
“Kwa kuwa watu hukata leseni na huwa zinalipiwa basi kiasi
fulani cha fedha kipelekwe katika huduma za afya,” anasema.
Hali halisi..... Itaendelea
Chapisha Maoni