Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement
RIPOTI MAALUM

NA VERONICA ROMWALD – ALIYEKUWA MOROGORO

Mei 5, mwaka huu Tanzania iliungana na mataifa mengine duniani kusherehekea Maadhimisho ya Siku ya Wakunga Duniani ambayo kwa mwaka huu yalipewa Kauli mbiu isemayo 'Wakunga ni Chachu  katika Utoaji Huduma bora kwa mama na mtoto'.

Tanzania iliadhimisha siku hii ya pekee, maadhimisho hayo yalifanyika huko mkoani Morogoro katika viwanja vya sabasaba.

Upo msemo wa wahenga usemao, usitukane wakunga na uzazi ungalipo, msemo huu unalenga kuhamasisha jamii kumthamini mkunga kulingana na nafasi yake ‘nyeti’ aliyonayo.

Mkunga ni mtu muhimu mno katika kusaidia kufanikisha kuanza kwa safari ya mwanadamu duniani, huhitajika katika kusaidia na kufuatilia hali ya mama tangu anapogundulika kuwa mjamzito, kipindi cha ujauzito na hadi kujifungua.

Hata baada ya mama kujifungua mkunga huendelea kufuatilia hali yake na mtoto au watoto waliozaliwa hadi wanapofikisha kipindi cha umri wa miaka mitano.

Ili kufanikisha safari hiyo salama mama anapaswa kuanza kuhudhuria kliniki pindi tu anapojihisi kuwa ni mjamzito, ili afya yake na maendeleo ya mtoto aliyepo tumboni ifuatiliwe kwa ukaribu na watumishi wenye ujuzi.

Wapo ambao wanaufananisha uhai wa mwanadamu na ‘bidhaa adimu’ ambayo kamwe mtu hawezi kuipata popote duniani akainunua.

Ni zawadi maalum na ya pekee ambayo Mwenyezi Mungu humjalia kila mmoja kwa mapenzi yake.

Kibaiolojia wataalamu wa afya wanasema uhai wa mwanadamu huanza rasmi pale tu mbegu ya baba inaposafiri hadi kukutana na yai la mama na kutunga mimba, baada ya kujamiiana.

Wanasema suala la uzazi linahusisha jinsi zote mbili (ya kike na kiume) lakini kujifungua mtoto au watoto ni jukumu la msingi la mama, ni haki ya msingi pia ya kila mwanamke duniani.

Wanasema pamoja na hilo siku hizi wengine huweza kutumia njia ya kupandikiza (IVF) kitaalamu na kupata mtoto au watoto hasa wale wanaokabiliwa na matatizo ya uzazi, hayo ni matokeo ya kukua kwa sayansi na teknolojia.

Lakini kiasili, baada ya mbegu na yai kutunga mimba ndani ya mfuko wa uzazi wa mama, mimba hiyo hukua na kuishi humo kwa muda wa miezi tisa.

Inapotimia miezi hiyo tisa mama hujifungua na mtoto au watoto hao huanza rasmi ‘safari’ yao ya maisha hapa duniani, ni tukio la kipekee.

Pamoja na hayo, wanasisitiza afya ya mama na mtoto ni jambo la msingi kuzingatiwa kwani kadiri mtoto anavyokuwa na afya njema ndivyo ambavyo naye atakuwa na uwezo mzuri wa kuzaa (wa kike) au kuzalisha (wa kiume).

Zamani mabibi zetu walilazimika kujifungua kwa msaada wa wakunga wa jadi ingawa hadi sasa bado zipo jamii ambazo hujifungua kwa wakunga hao hata hivyo kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia wengi leo hii wanajifungua kwa msaada wa wakunga wataalamu.

Pamoja na umuhimu huo wa wakunga kwa miaka ya hivi karibuni baadhi yao wamekuwa wakilalamikiwa na wananchi (wajawazito) na hata jamii kwa ujumla kwamba wanatenda kazi bila kuzingatia misingi ya taaluma yao.

Wapo ambao wanatuhumiwa kuwatolea lugha zisizofaa wajawazito wakati wanapokuwa wakiwahudumia huko kliniki au katika vyumba vya kujifungua (labour).

Simulizi ya Frida

Frida Eliud Mkazi wa Morogoro ni mama wa watoto wawili, anasema mtoto wake wa kwanza alijifungulia katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro mwaka 1998.

Anasema wakati wa ujauzito wake huo wa kwanza alipatwa wasiwasi mwingi wa kuanza kuhudhuria kliniki hasa alipokuwa akikumbuka simulizi alizosimuliwa na wanawake wenzake kuhusu lugha zinazotolewa huko kliniki.

“Walikuwa wakinisimulia jinsi walivyopokelewa katika hospitali walizokwenda kwamba baadhi ya wakunga na wauguzi wanatoa lugha za kuudhi, lakini ilifika mahali nikasema wacha niende tu kwa sababu sina jinsi na lazima nifuatilie maendeleo ya hali yangu na mtoto wangu aliye tumboni.

“Nilianza kuhudhuria kliniki, sitasahau siku ile ya kwanza, muuguzi aliyenipokea hakuwa na lugha nzuri, hata siku nilipokwenda kujifungua mkunga aliyenisaidia naye hakuwa na lugha nzuri, kusema ukweli wapo wanaofanya vema lakini kuna wengine wanawaangusha kwa kufanya yasiyofaa,” anasema.

Anaongeza “Mkunga yule kila nilipomuita aje anisaidie alikuwa akiniambia nisimsumbue, kwamba kuna wengine pia waliokuwa wakihitaji kusaidiwa na yeye hakuwa na uwezo wa kujigawa atusaidie wote.

“Nilipelekwa pale hospitalini usiku sikujifungua hadi ikafika asubuhi, mume wangu alikuja nikamsimulia kilichokuwa kikiendelea, alisikitika mno.

“Lakini hakuwa na jinsi ilibidi wasubiri hadi nilipojifungua majira ya saa nne hivi, tukarudi nyumbani, ujauzito wangu wa pili nilikwenda tena hospitali nyingine ya serikali,” anasema.
Anaongeza “Nilipokelewa na mkunga wa kiume, nilichelewa kujifungua lakini aliendelea kunihudumia kwa upendo na kwa kunithamini mno.

“Alikuwa na lugha nzuri, muda wote alikuwa akija kuniangalia na kunitia moyo kwamba nisiogope, nitajifungua salama kwa kweli nilistaajabu, nikajifungua salama nikarudi nyumbani kwangu na furaha,” anasema.

Anasema hivi sasa ana ujauzito mwingine na kwamba anatamani kwenda kujifungua kwenye hospitali hiyo na anatamani akifika huko apokewe na mkunga wa kiume na si wa kike.

Mama mwingine

Mariam James (50) Mkazi wa Morogoro Mjini ni mama wa watoto watatu, anasema awali alikuwa akiishi Jijini Dar es Salaam eneo la Sinza kwa Remmy.

Anasema alipojihisi kuwa ni mjamzito mnamo mwaka 1990  aliamua kufanya uchunguzi hospitali ipi itamfaa kwa huduma ya kliniki.

“Wanawake wenzangu walishanisimulia changamoto walizokumbana nazo katika hospitali mbalimbali, lakini nikasema kwa kuwa ninahisi ni mjamzito nifanye uchunguzi kwanza hospitali ipi itanifaa nianze kliniki.

“Basi nilikwenda kwanza Hospitali ya Tandale, nikakaa kwenye benchi nikaangalia namna ambavyo wauguzi na wakunga walivyokuwa wakipokea wagonjwa na kuzungumza nao,” anasema.

Anasema hakuridhishwa na watumishi wa hospitali hiyo, hivyo aliondoka tena hadi Hospitali ya Mwananyamala  akakaa kwenye benchi na kufanya tena uchunguzi wake.

“Hapo napo sikuridhika na huduma, nikaondoka hadi Hospitali ya Mnazi Mmoja nikafanya hivyo hivyo, kidogo hapo niliridhishwa na huduma, kulikuwa na wauguzi na wakunga wenye umri wa utu uzima tofauti na kule nilipokwenda awali, walikuwa wakipokea watu kwa kauli nzuri mno.

“Lakini nikasema ngoja niende na Hospitali ya Taifa Muhimbili nikaangalie huduma zilivyo,  huko sikuridhishwa, nikaamua kurudi Mnazi Mmoja wale watumishi wakaniambia muda ulikuwa umekwisha, ilikuwa siku ya ijumaa basi wakanishauri niwahi mapema asubuhi nianze kliniki,” anasema.

Mariam anasema aliondoka akiwa na furaha na kwamba aliwahi mapema jumatatu hospitalini hapo na kuanza kliniki ya uzazi.

“Wale watumishi walikuwa wakiongea nasi kwa lugha nzuri, walikuwa wanahudumia kwa upendo, wanafariji na wanabembelea mtu unajisikia amani muda wote tofauti na wale watumishi wa hospitali zingine ambazo nilikwenda walikuwa wakizungumza vibaya na wagonjwa,” anasema.

Anaongeza “Niliendelea kuhudhuria kliniki Mnazi Mmoja lakini nilipofikia kujifungua walinishauri nitafute hospitali nyingine kwa sababu wakati ule pale walikuwa hawana huduma ya kujifungua bali ya kliniki tu.

“Ingawa nilitamani kujifungulia pale lakini sikuwa na jinsi ilibidi nirudi Mwananyamala nikajifungulia hapo, kusema ukweli jinsi wauguzi na wakunga wenye umri wa utu uzima walivyokuwa wanahudumia ilikuwa tofauti kabisa na wale wenye umri wa ujana wakati huo,” anabainisha.

Anasema hadi sasa anaona kuna utofauti mkubwa kati ya watumishi wenye umri mkubwa jinsi wanavyohudumia wagonjwa na wale watumishi wenye umri mdogo.

“Wenye umri mkubwa wana hudumia kwa upendo zaidi kuliko hawa wenye umri mdogo (wa ujana), kwa msingi huo, ikiwa inawezekana basi naishauri serikali iangalie hii kazi ya uuguzi na ukunga ifanywe na watu wenye umri wa utu uzima kuliko vijana,” anashauri.

Ukweli wa mambo

Pamoja na umuhimu wa kada hii katika sekta ya afya hata hivyo kwa muda mrefu sasa yamekuwako malalamiko kutoka kwa jamii wakidai baadhi yao wamekuwa wakizungumza lugha zisizofaa (za kejeli au matusi) kwa wajawazito hasa wanapokwenda kujifungua.

Itaendelea

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement