Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement

Picha (na mtandao) inaonesha dalili za ugonjwa huo.

*Ni ugonjwa usiojulikana chanzo chake, hauna tiba

*Huweza kusababisha kuharibika mimba

NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

KWA kawaida kinga za mwili humlinda mtu husika dhidi ya magonjwa mbalimbali, hata hivyo wapo baadhi ambao hujipata kinga zao zikishambulia mwili badala ya kuulinda.

Ugonjwa huo kitaalamu huitwa ‘System Lupus Erythematosus (SLE), hadi sasa bado wataalamu wa afya hawajabaini nini hasa husababisha kutokea kwake.

May 3, 2018, Onesmo Mhehwa aliyekuwa Daktari Bingwa wa Usingizi kwa Watoto na Wagonjwa mahututi katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) alifariki dunia kutokana na ugonjwa huo.

Simulizi ya mgonjwa

Meneja Utawala, Huduma za Hospitali (HR) katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI), Costansia Lima anasema mwaka 2015 alianza kujihisi vibaya hasa sehemu za kichwa.

“Nilianza kuhisi pia sehemu ya tumbo (eneo la chini) lilianza kuuma, nikaenda kuonana na Medical Director wa Muhimbili nikamueleza, akanipatia daktari wa Neurology, akanichunguza kwa vipimo mbalimbali ikiwamo MRI lakini hakuona tatizo.

“Siku zilivyoenda hali yangu ilizidi kubadilika, nikaanza kupata reaction kwenye ngozi, nikawa napata mabaka meusi, nywele zikaanza kunyofoka nikichana, nikabadilika sura, nilikuwa na hali mbaya.

“Mkurugenzi wa Muhimbili akasema kama imeshindikana kugundulika wanipe rufaa nikapelekwa India, kule nilipata nimonia kali, lakini Mungu alinisaidia nikapata matibabu na nikapata nafuu, nikarejea nyumbani nikapewa dawa za kunisaidia.

“Sikuweza kuzungumza na wale madaktari nilikuwa na hali mbaya, nipo nchini naendelea na matibabu hapa nyumbani, ni wakati sasa jamii ielezwe kwa kina kuhusu ugonjwa huu, inawezekana wanaumwa lakini hawajui kama ni ugonjwa, mimi ilichukua muda mrefu kugundulika,” anasema Lima huku akitokwa machozi.

Mgonjwa mwingine

Tangu mwaka 2007 hadi sasa, Irene Kilumanga ambaye ni mke wa Balozi Chabaka Kilumanga anaishi akisumbuliwa na ugonjwa huo na kwamba dalili zake zinafanana na za malaria, kuhisi homa homa.

Mumewe, Balozi Kilumanga anasema watu wanaougua ugonjwa huo unaweza kuona wanafanya makusudi kutokana na kuugua kwa muda fulani na muda mwingine kuoneka akiwa mzima.

“Kwa mtu ambaye hana imani anaweza kudhani amerogwa kwa sababu anaweza kuwa mzima na ghafla akajikuta ameanguka, mwili unaanza kuishiwa nguvu na anapata maumivu,” anasema.

Anaongeza “Sisi tulimpeleka hospitalini akawa akitibiwa baada ya muda tena anaumwa, tukimrudisha ikawa madaktari wanajaribu kuchunguza kila aina ya ugonwja lakini hawakuweza kubaini kilichokuwa kinamsumbua.
 Image result for dk. mhehwa jkci
Daktari

Kifo cha Dk. Mhehwa (pichani) kimeipa ‘pigo’ JKCI kwani ndiye alikuwa pekee kwa upande wa matibabu ya watoto.

Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Profesa Mohamed Janabi anasema pamoja na kutojulikana chanzo cha ugonjwa huo hauna tiba.

Anasema hata dalili zake bado hazijathibitika na kwamba hufanana kwa ukaribu na dalili za magonjwa mengine kama vile malaria.

“Wataalamu hata sayansi haijaweza kujua, ile system ya mwili inaugeuka mwili wenyewe, ghafla inaanza kuushambulia kila mahali, kwenye figo, moyo, tumbo chochote wenyewe unadhani ni adui.

“Hauna tiba, mgonjwa akija hospitalini kama anasumbuliwa na bakteria tunampa antibiotics, ikiwa ni virusi nitakupa dawa ya virusi, lakini kwa kawaida mtu anapolalamika kuumwa moja kwa moja tunaangalia labda amepata malaria.

“Lakini akipimwa malaria haionekani, typhoid hana, hapo inabidi achunguzwe zaidi kuliko vipimo vilivyozoeleka na ndipo tunapogundua nini kinamsumbua.
“Tafiti zinaonesha wanawake ndiyo huathiriwa zaidi kuliko wanaume, imefika wakati sisi madaktari tubadili mtazamo wetu tulionao kwa sababu si kila homa ni malaria, tuanze kuchunguza zaidi ya hapo,” anasema Profesa Janabi (Pichani).

Utafiti

Kulingana na mtandao wa Medical News Today, inaelezwa Lupus ni miongoni mwa magonjwa sugu, ambapo kinga za mwili wa binadamu badala ya kumlinda hugeuka na kuanza kumshambulia.

Hali hiyo inapotokea muhusika huhisi maumivu makali, huvimba mwili, homa za mara kwa mara, na baadae viungo vyake vya ndani ikiwamo moyo, figo na mapafu navyo huathiriwa.

Mtandao huo unaeleza, kwa kawaida mfumo wa kinga hutengeneza protin iitwayo ‘antibodies’ ambayo hulinda na kupigana dhidi ya ‘antigens’ kama vile virusi na bakteria.

Lakini, kwa mtu mwenye Lupus mambo huwa kinyume, yaani ule mfumo wake wa kinga wa mwili hushindwa kutofautisha kati ya ‘antigens’ na tishu zilizo bora.

Hali hiyo husababisha mfumo wa kinga kuziamuru ‘antibodies’ kuzishambulia tishu zilizo bora badala ya ‘antigens’ kama inavyopaswa.

Kwa mujibu wa mtandao huo, kitendo hicho ndicho ambacho hupelekea muhusika kupata maumivu makali, uvimbe na kuathirika kwa viungo vyake.

Inaelezwa ugonjwa huo si wa kuambukiza na kwamba umegawanyika katika aina mbalimbali ikiwamo Lupus Erythematosus (SLE) na Lupus Discoid (Cutaneous).
 Related image
Celena Gomez ni msanii mkubwa anayesumbuliwa na ugonjwa huo, 

Mtandao huo unaeleza, Kulingana na Shirika la Lupus la nchini Amerika, watu wapatao milioni 1.5 hadi mbili nchini humo wanakabiliwa na aina mojawapo ya Lupus.

Inaelezwa asilimia 72 ya wamarekani wenye umri wa miaka kati ya 18 hadi 34 hawaufahamu kwa kina ugonjwa huo.

Mtandao huo unaeleza zaidi ya asilimia 90 ya wagonjwa wa Lupus ni wanawake na kwa kawaida huwapata watu walio kati ya umri wa miaka 15 hadi 45.

Dalili zingine

Kulingana na mtandao wa Heath line, watu wenye Lupus figo zao huvimba hali iitwayo kitaalamu ‘nephritis’ huzifanya zishindwe kuchuja taka mwili na kujikuta wakipoteza damu.

Mtandao huo unaeleza, kwa mujibu wa Shirika la Lupus la Amerika, nephritis huanza kujitokeza ndani ya kipindi cha miaka mitano tangu mtu apate ugonjwa huo.

Unaeeleza mtu mwenye Lupus ambaye figo zake zimeanza kushindwa kufanya kazi huvimba miguu, hupata shinikizo la damu, huona chembe chembe za damu kwenye mkojo wake.

Unaeleza wakati mwingine mkojo huonekana kuwa wa rangi nyeusi, huenda haja ndogo mara kwa mara hasa nyakati za usiku na hupata maumivu wakati wa kujisaidia haja ndogo.

Wakati mwingine, mtu mwenye Lupus huugua homa ya matumbo ingawa si wote na wapo ambao hupata ukavu wa midomo au macho na kunyonyoka nywele.

Kwa mujibu wa mtandao huo, wagonjwa wengi wa Lupus upata vipele usoni unaozunguka (butterfly rash).
 Image result for lupus
Kwanini wanawake?

Mtandao huo wa Health Line unaeleza wanawake wanaokabiliwa na ugonjwa huo huonesha dalili pia kipindi cha hedhi na ujauzito.

Hali hiyo inawafanya wanasayansi kuamini kwamba huenda linachochewa zaidi na homoni ya kike (Estrogen) hata hivyo bado tafiti zinahitajika kuthibitisha ukweli wa mtazamo huo.

Mtandao wa Medicine Net unaeleza mjamzito mwenye tatizo la Lupus hupaswa kufuatiliwa hali yake kwa ukaribu zaidi kwani tatizo hilo huweza kupeleka kuharibika kwa mimba.

Visababishi

Pamoja na kuwa bado chanzo chake hakijulikani wala tiba yake haijulikani, hata hivyo wataalamu wa afya wanaamini kwamba huenda ugonjwa huo unatokana na sababu za mabadiliko ya vinasaba na za kimazingira.

Inadhaniwa vitu ambavyo huchangia mtu kupata Lupus ni pamoja na msongo wa mawazo, miale ya jua, matumizi ya dawa za kulevya, maambukizi ya virusi vya Epstein-Barr (kwa watoto) na yale yatokanayo na baadhi ya kemikali, mwanga wa ‘ultraviolet’, matumizi ya sigara na dawa za kutuliza maumivu (antibiotics).

Changamoto zingine

Mtandao wa Health Line unaeleza wagonjwa wa Lupus hukabiliwa pia na tatizo la kushindwa kuganda kwa damu, kuvimba mishipa ya damu, mabadiliko ya tabia, kushindwa kutunza kumbukumbuku, kuvimba mapafu, moyo na hatimaye kiharusi.

Kwa mujibu wa mtandao huo, tafiti zinaonesha watu wanaokabiliwa na ugonjwa huo huweza kuishi nao kwa miaka 40 ikiwa watapata matibabu sahihi.

Mkakati

Dk. Mhehwa (marehemu) amekuwa chanzo cha watu wengi kuanza kuujua ugonjwa huu baada ya kufariki na ndipo nilipoona Profesa  Janabi akiizungumzia nikaona nimtafute ili tushirikiane kuutangaza,” anasema Dk. Kilumanga.

Anasema wanakusudia kuanzisha taasisi ambayo itakuwa ikijishughulisha kutoa elimu kwa umma juu ya ugonjwa huo.

Anasema katika nchi zilizoendelea wanaujua ugonjwa huo wa SLE ambapo kuna siku maalumu ya kuadhimisha ambayo ni May 10 kila mwaka.

“Anasema matibabu dhidi ya ugonjwa huo ni ghali na kwamba vidonge anavyopatiwa mgonjwa si tiba bali humsaidia tu kupunguza yale maumivu anayoyapata ili ugonjwa huo usifikie hatua za juu (acute stage) na kusababisha viungo vyake vya mwili kuanza kushambulia.

Ombi kwa serikali

Balozi Kilumanga anaishauri serikali ianze kuandaa wataalamu watakaobobea kutibu ugonjwa huo tofauti na ilivyo sasa.

Aidha, anaishauri kununua vifaa vya kupimia ugonjwa huo ili watu waweze kugundulika mapema tofauti na ilivyo sasa ambapo wanaenda kugundulika nje ya nchi.

Balozi Chabaka Kilumanga pia anaiomba serikali, kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kuangalia kwa undani suala hili ikiwa ni pamoja na kuanzisha kitengo kitakachoangalia ugonjwa huu.

“Aidha, pamoja na kuanzisha kitengo hicho ni muhimu pia kuangalia namna ya kuwapata wataalamu ambapo wataushughulikia ugonjwa huu,” anatoa rai.

Makala haya kwa mara ya kwanza yametoka Mei 31, 2018 katika gazeti la MTANZANIA ambalo nalitumikia.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement