NA VERONICA ROMWALD - DAR ES SALAAM
UTAFITI
uliofanywa na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) umeonesha watoto wengi
wenye saratani ya jicho wanaopokelewa hospitalini hapo wanatoka katika
maeneo ya Kanda ya Ziwa.
Hayo
yalielezwa Dar es Salaam jana na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Saratani
kwa Watoto wa Muhimbili, Anna Sanyiwa alipozungumza mbele ya Mganga
Mkuu wa Serikali walipotoa tamko kuhusu Maadhimisho ya Wiki ya Kuongeza
Uelewa kuhusu Saratani ya Jicho (Retinoblastoma).
"Mwaka
2007 tulifanya utafiti ulionesha hali hiyo na hivi karibuni, mwaka huu
tumefanya tena utafiti bado wagonjwa wengi tunapokea kutoka ukanda huo, "
alisema.
Alisema wagonjwa wengi wanatoka maeneo ya vijijini mno hasa mkoa wa Mwanza, Tabora, Rukwa tena kutoka jamii masikini.
"Hatujajua
sababu hasa ni nini lakini mara nyingi saratani hii inatokana na
hitilafu ya vinasaba, tunadhani labda pengine na changamoto za mazingira
zinachangia, hilo bado hatujajua, " alisema.
Alisema
pamoja na hayo utafiti huo mpya umeonesha matumaini kidogo kuliko ule
wa mwaka 2007 kwamba angalau wazazi wameanza kuwahishwa watoto
hospitalini.
"Awali
walifikishwa wakiwa wamechelewa mno, lakini siku hizi wanaletwa wakiwa
na miezi mitano, sita na kuendelea, hata hivyo bado asilimia 85 wanakuja
wakiwa wamechelewa kwa asilimia 40 hupona na vifo ni asilimia 50,"
alisema.
Alisema katika nchi zilizoendelea asilimia 90 ya wagonjwa hupona kwani huwahishwa hospitalini.
"Inabidi
tujitahidi kuhamasisha jamii walete watoto tuwachunguze mapema dawa
zipo, vifaa vipo na wakiwahi matibabu wanapona, " alisema.
Akizungumza,
Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Mohamed Kambi alisema Retinoblastoma
ni saratani inayotokea mara nyingi watoto wakiwa na umri wa mwaka mmoja
hadi miaka mitano.
"Ni
tatizo la Kitaifa, hutokea kwenye pazia la fahamu la jicho, inaweza
kuathiri jicho moja ama yote mawili iwapo lililoathirika huachwa bila
kutibiwa, " alisema.
Alisema hiyo huharibu jicho lote na kulazimisha jicho kutolewa amazing kuleta kifo baada ya kusambaa katika hatua za mwisho.
"Kati
ya vizazi hai 16,000 hadi 18,000 duniani asilimia moja huwa na saratani
ya Retina, huchangia asilimia tatu ya saratani za watoto duniani kote
na kwa Afrika huchangia asilimia 10 hadi 15 ya saratani zote za watoto,
idadi ipo sawa kwa wavulana na wasichana, " alisema.
Alisema takwimu nchini zinaonesha watoto 137 wenye saratani hiyo walionwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya mwaka jana.
Alisema
watoto wanaopewa rufaa na kufika Muhimbili ni wastani wa watoto 80 hadi
100 kila mwaka, wengi hutibiwa Hospitali ya KCMC Moshi.
Alisema
maadhimisho ya Wiki ya Saratani ya Retina kwa mwaka 2018 yamebebwa na
kauli mbiu isemayo 'Mboni Nyeupe kwenye Jicho la Mtoto ' inaweza kuwa
Saratani ya Retinoblastoma.
Habari hii imetoka leo katika gazeti la MTANZANIA ambalo nalitumikia.
Chapisha Maoni