NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM
EBOLA ni miongoni mwa magonjwa ya
mlipuko yanayotishia uhai wa viumbe hai hasa binadamu waishio katika Ukanda wa
Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Mtandao wa Wikipedia unaeleza ugonjwa
huo kwamba husababishwa na virusi vya Ebola ambavyo hupelekea tatizo la damu
kutoganda na unaua.
Ni ugonjwa hatari ambao husababisha kuvuja
kwa damu ndani ya mwili na kutoka kupitia matundu mbalimbali ya nje ikiwamo
mdomoni, sikioni, puani na hatimaye kifo.
Inaelezwa kwamba huweza kusambaa kwa
haraka kupitia kwa maji maji ya mwili na dalili zake hazitambuliwi kwa urahisi.
Virusi vya Ebola viligunduliwa
katika miaka ya nyuma mnamo 1976 katika milipuko miwili ambapo watu 151 walifariki
katika enoe la Nzara, Sudan kusini na watu 280 waliofariki katika eneo la
Yambuku karibu na mto Ebola uliopewa jina kutokana na ugonjwa huo.
Mlipuko wa Ebola wa mwaka 2014-16
Afrika uliowaua watu 11,300 ulikuwa mbaya zaidi, ulisamba kwenda miji mikuu ya
nchi za Guinea, Sierra Leone na Liberia.
Inakadiriwa kati ya watu 10 wanaopata
virusi vya Ebola wastani wa watano hadi tisa kati yao hufariki dunia.
Mtu hupata ugonjwa huo kwa kugusa damu
au majimaji ambayo yanakuwa yametoka kwa mtu mwenye maambukizi ya ugonjwa huo.
Ama kwa kugusa maiti ya mtu aliyekufa kwa ugonjwa huo, kugusa
wanyama (mizoga na wanyama wazima) walioambukizwa kama vile sokwe na swala wa
msituni.
April 4, mwaka huu Shirika la Afya Duniani (WHO) ilitangaza kuzuka
tena kwa ugonjwa huo huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Viliripotiwa visa 30, watu
wapatao 18 wamefariki dunia licha ya kwamba ni visa viwili tu ndivyo
vilivyothibitishwa kimaabara kwamba vilitokana na Ebola.
Ugonjwa huo uliripotiwa kutokea huko katika mji wa Biroko
ulioko jimbo la Equator ambapo takriban mwaka mmoja uliopita ulitokea mlipuko
mwingine ambao ulisababisha vifo vya watu wanne.
Mei 17, mwaka huu, ugonjwa huo uliripotiwa
kuanza kusambaa katika eneo jingine jingine nchini humo, Waziri wa afya wa
Kongo, Oly Ilunga Kalenga, alithibitisha kisa kimoja huko mjini Mbandaka.
Mji huo unatajwa kuwa na wakazi wengi
kiasi cha milioni moja, upo kilomita 130 kutoka eneo ambapo kisa cha kwanza
kilithibitishwa mapema mwezi huu.
Mji huo ni muhimu kwa usafiri ukiwa na
barabara zinazoelekea mji mkuu Kinshasa, hofu inazidi kuenea wapi kwengine
ugonjwa huo utazuka.
Ofisa wa cheo cha juu wa WHO, Peter
Salama, alinukuliwa akisema kuanza kusambaa kwa Ebola kwenda Mbandaka kuna-maanisha
kuwa huenda kukawa na visa vingine vya milipuko ya ugonjwa huo.
Visa vilivyothibitishwa vya ugonjwa huo
vimerekodiwa sehemu tatu kwenye mkoa wa Equateus, kwa mujibu wa WHO.
Wafanyakazi wa afya wametambua watu 430
ambao huenda wakikaribiana na ugonjwa huo na wanajaribu kuwatafuta wengine 4000
ambao wametawanyika kwenda kaskazini magharibi mwa Kongo.
Siku ya Jumatano chanjo kwa ajili ya
majaribio dhidi ya ugonjwa wa ebola
iliyotumwa na WHO iliwasili nchini humo huku nyingine ikitarajiwa kuwasili hivi
karibuni.
Mkurugenzi wa WHO, Tedros
Adhanom (pichani) alitembelea katika mji wa Bikoro kaskazini magharibi mwa nchi hiyo,
kujionea hali halisi na kufanya tathmini namna ya kudhibiti maambukizi ya
ugonjwa huo.
WHO hivi sasa inafuatilia kwa
ukaribu mlipuko huo wa ugonjwa ambao unaambukizwa kwa njia ya kugusa majimaji
yaliyotoka kwa mgonjwa.
Hofu iliyopo sasa ni wapi
pengine ugonjwa huo utazuka na kuathiri maeneo mengine duniani, hivyo WHO
tayari mashirika mengine yanayofanya kazi nchini humo na yale ya Umoja wa
Mataifa yameanza kutuma timu ya waangalizi wao nchini humo ili kufuatilia na
kudhibiti usienee.
Kila nchi inapaswa kuhakikisha
inafuatilia kwa ukaribu ugonjwa huo na kuimarisha mifumo yake ya ukaguzi wa
wageni hasa katika maeneo ya mipakani na viwanja vya ndege ili kuudhibiti.
Waziri wa Afya, Maendleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,
Ummy Mwalimu anasema tayari wamechukua hatua juu ya hilo.
“Ebola ni kati ya magonjwa yenye hatari ya kusambaa kwa kasi
na kuleta madhara makubwa kiafya duniani. Ingawa hadi sasa Tanzania hakuna
mgonjwa yeyote aliyehisiwa au kuthibitishwa kuwa na virusi vya ebola, nchi yetu
inapata na Kongo na ipo hatarini kuambukizwa kutokana na mwingiliano wa watu
wanaosafiri, wanaotoka na kuingia.
“Kwa sababu hizi, tahadhari lazima zichukuliwe, hivyo Wizara
inapenda kutahadharisha wananchi juu ya ugonjwa huu katika mikoa yote hasa
iliyoko mpakani mwa Kongo ikiwamo Mwanza, Kagera, Kigoma, Katavi, Rukwa na
Songwe,” anasema.
Anasema katika mikoa hiyo serikali imeweka uangalizi zaidi
kwani ndiko ambako kuna muingiliano mkubwa wa watu hadi kupitia njia ya majini.
“Ingawa kuna changamoto tunaiona hasa kuwapo njia za panya
ambazo baadhi ya watu wasio waaminifu huweza kuzitumia lakini pia kuna
wahamiaji haramu, lakini tunashirikiana kwa ukaribu na nchi zingine kuudhibiti
tukiongozwa na Sheria ya Kimataifa ya Afya (IHR) kila nchi inawajibika,”
alisema.
Ramani inaonesha maeneo yaliyopo hatarini kupata maambukizi ya ugonjwa huo.
Dalili
Anasema huanza kuonekana kwa mtu aliyeambukizwa baada ya siku
mbili hadi 21 tangu alipoambukizwa.
“Hupata homa ya ghafla, hulegea mwili, hupata maumivu ya
misuli, kuumwa kichwa na vidonda kooni, mara nyingi dalili hizi hufuatiwa na
kutapika, kuharisha, vipele vya ngozi na pia figo na ini hushindwa kufanya
kazi,” anasema.
Waziri Ummy anasema ugonjwa huo unaweza kuzuilika kwa mtu
kujikinga kwa kuepuka kugusa au kuingiwa na mate, damu, mkojo, jasho, kinyesi,
machozi na majimaji mengine yanayotoka mwilini kwa mtu mwenye dalili.
“Kwa kuepuka kushughulikia maiti ya mtu aliyekufa akiwa na
dalili za ebola, badala yake watoe taarifa kwa uongozi wa kituo cha huduma za
afya kwa ushauri.
“Wananchi waepuke mila na desturi zinazoweza kucheleweha
kupata huduma muhimu na kuzidi kueneza ugonjwa huu,” anasema.
Anasema wanapaswa kuzingatia usafi wa mwili, kutoa taarifa
mapema kwa viongozi wa serikali na wa huduma za afya katika ngazi zote pale
anapotokea mtu mwenye dalili za ebola.
Anasema njia nyingine ya
kuubidhiti ugonjwa huo ni kufuatilia kwa ukaribu na kuwatenga wale
wanaogundulika kuwa na maambukizi hayo na kuwaweka katika mpango wa ufuatiliaji.
“Yeyote anayekuwa kwenye hatari
ya kuambukizwa anafuatiliwa kwa siku 21 na maziko hufanyika kwa uangalizi ili
kuudhibiti,” anasema.
Aidha, dunia haiwezi kusahau
janga la Afrika magharibi mnamo 2014-16 lililozuka katika kijiji kimoja cha
mpakani nchini Guinea, na muathiriwa wa kwanza anadhaniwa kuwa mtoto wa kiume
mwenye umri wa miaka miwili aliyefariki duniani mnamo 2013.
Kuhusu chanjo
Waziri Ummy (pichani) anasema bado wanasubiri kupokea
taarifa rasmi ya WHO na kusisitiza hadi sasa hakuna mtu aliyehisiwa kuwa na
ugonjwa huo nchini.
“Tumeimarisha mfumo wa
ufuatiliaji magonjwa, kila siku tunapokea taarifa kuhusu wagonjwa nchi nzima,
hadi sasa hakuna taarifa ya mtu aliyehisiwa kuwa na Ebola, tupo salama,” anasema
Waziri Ummy.
Ni janga
Magonjwa ya mlipuko sasa ni janga linalotesa nchi
zinazoendelea hasa zilizopo kusini mwa Jangwa la Sahara ambako jamii nyingi
zinaishi katika ‘dimbwi’ la umasikini.
Pamoja na magonjwa hayo, majanga mengine yanayozikumba nchi
hizo ni ya kiasili kama vile ukame, mafuriko na zipo zenye migogoro ya kisiasa.
Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Afya Duniani (WHO-Kenya), Dk.
James Kojo anasema kati ya majanga ya dharura 100 ya dharura yanayotajwa kila
mwaka katika Ukanda huu, mengi ni yale ambayo huusisha magonjwa ya mlipuko
ambayo huhitaji ufumbuzi wa haraka.
Kulingana na WHO, kipindupindu ndiyo ugonjwa wa mlipuko
unaoonekana kuwa tishio zaidi huchukua kiasi cha asilimia 23 kila mwaka.
WHO inaeleza ni tatizo linalokabili nchi nyingi na kwamba majanga
ya asili ni asilimia 17 na asilimia tano huwa ni majanga mengineyo ukiwamo
Ebola.
Rai kwa
waandishi
Kojo anasema Serikali pekee kupitia wizara ya afya haziwezi
kufanya kazi peke yake kukabili magonjwa na kwamba waandishi wa habari wana
nafasi kubwa kushirikiana nao kuhakikisha wanatoa taarifa sahihi ili kusaidia
jamii.
“Sisi (WHO na Wizara) kazi yetu ni kutoa takwimu lakini
hatuwezi kusimulia habari. Ninyi mnao uwezo huo lakini ni muhimu kuhakikisha
mnakusanya taarifa kutoka kwa vyanzo sahihi ili kuisaidia jamii hasa jinsi ya
kuepuka magonjwa haya,” anatoa rai.
Chapisha Maoni