Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement

NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

MWAKA 1987 wanafunzi wanne kati 200 waliokuwa wakisoma katika Shule ya Msingi Kipampa iliyopo huko Ujiji mkoani Kigoma walichaguliwa kujiunga na masomo ya sekondari.

Maulid Kikondo alikuwa miongoni mwa wanafunzi hao waliochaguliwa na serikali kuendelea na masomo ya sekondari.

“Nilipelekwa Kilosa Agricultural Secondary School iliyoko huko mkoani Morogoro ambako nilisoma kwa miaka minne na nikahitimu kidato cha nne.

“Baada ya hapo nilibahatika tena kuchaguliwa kuingia kidato cha tano katika Shule ya Sekondari Pugu hiyo ilikuwa 1992 nilisoma Fizikia, Kemia na Biolojia (CBG) mwaka 1994 nilihitimu,” anasema.

Kikondo anasema mwaka 1995 alifanikiwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Tiba na Sayansi Shirikishi Muhimbili wakati huo kilikuwa bado ni tawi la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

“Nilifanikiwa kusoma masomo ya radiolojia (elimu ya uchunguzi wa magonjwa kwa njia ya mionzi) nilihitimu mwaka 1998,” anasema.

Anasema baadae alijiendeleza kusoma katika Ultra sound, baada ya kumaliza masomo Muhimbili alipata ajira katika Hospitali ya Shiu Hindu Mandal ambako alifanya kazi mwaka 1999 hadi 2002.

Anasema mwaka 2002 aliajiriwa katika Hospitali ya regency idara ya radiolojia ambayo wakati huo ilikuwa ndiyo hospitali pekee iliyokuwa na kipimo cha CT Scan.

Anasema alifanya kazi katika hospitali hiyo hadi Juni, 2003 alipoajiriwa katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI).

“Nikiwa MOI nilichaguliwa kuwa miongoni mwa wataalamu 24 ambao tulitakiwa kuanzisha Taasisi ya Magonjwa ya Moyo, tulipelekwa nchini India mwaka 2005 kujifunza na tulirudi nchini mwaka 2007,” anasema.
Anaongeza “Lakini kabla ya huko kote nilipomaliza elimu yangu ya radiolojia kwa sababu nilikuwa napenda sheria tangu nikiwa sekondari, mwaka 2000 nilianza kujipanga kusoma sheria.

“Nilijiunga pale Chuo Kikuu Huria mwaka 2001 nikaanza masomo na nilihitimu mwaka 2004, nilifaulu vizuri masomo yangu na nilihitimu kwa heshima mwaka 2005 nilifanya mafunzo ya vitendo kazini kama inavyotakiwa katika sheria ndipo nikaenda India,” anasema.

Anasema waliporudi mwaka 2007 aliomba kufanya mitihani ya uwakili ili aweze kufanya kazi hiyo, mwaka 2008 alifanya mtihani wake na Juni, mwaka huo huo  aliapishwa kuwa Wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
“Hivyo tangu mwaka huo nimekuwa nikifanya kazi kama wakili, baada ya hapo 2009 nilienda kusoma Ubelgiji, huko nilienda kujiendelea katika taaluma ya radiolojia nilifanya ‘Advance Study’ katika mambo ya ultra sound,” anasema.

Wakili Kikondo anasema mnamo mwaka 2011 alijiunga na Chuo cha Diplomasia ambako alisoma kozi ya Diplomasia ya Uchumi.

“Wakati nikiwa chuoni hapo nilisoma lugha ya Ki-Hispaniola ambayo kila mmoja wetu alipaswa kuisoma, na kabla ya kwenda India niliwahi kusoma pia Kifaransa pale Alliance France,” anasema.

Anaongeza “Hiyo ilinisaidia kwani nilipokwenda Ubelgiji sikusumbuliwa mno na lugha.

Wakili Kikondo anasema alipokuwa nchini India pia alijifunza kozi mbalimbali za komputa

“Mwaka 2014 nilianza kusoma Shahada ya Umahiri katika Usimamizi na Sheria za Fedha katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na nilihitimu mwaka 2016 nikiwa na alama nzuri,” anasema.

Kwanini udaktari kisha sheria

“Wakati sisi tunasoma kuliwa na sera iliyoelekeza wale ambao wanafanya vizuri katika masomo ya sayansi lazima waendelezwe kulingana na masomo hayo.

“Sasa mimi nilikuwa nafanya vizuri katika masomo yote ya sayansi na sanaa, nilikuwa na uwezo mkubwa wa kuzungumza lugha ya kingereza, nilikuwa mwenyekiti wa mdahalo shuleni kwetu na nilikuwa Waziri wa Elimu.

“Kulingana na sera iliyokuwepo wakati ule, ilinilazimu kusoma masomo hayo na ilikuwa vigumu kubadili mchepuo wakati ule,” anasema.

Anasema ameendelea kufanya vema katika ngazi hiyo ya afya hasa katika upande huo wa vipimo vya mionzi hususan Ultra sound.

“Tulifundishwa vizuri mno na sasa nawasaidia watanzania,” anasema.

Anamudu vipi?

“Binafsi naamini ‘The hard way is the only way’ yaani unapoamua kufanya jambo lazima uendelee kung’ang’ania hapo hapo na ndiyo maana niliendelea kung’ang’ania hadi nilipotimiza ndoto yangu ya kuwa mwanasheria,” anasema.

Anaongeza “Hivi sasa mimi ni mtaalamu wa uchunguzi wa magonjwa ya moyo kwa kutumia ultra sound na ni mtaalamu wa kuchunguza magonjwa kwa vipimo vya radiolojia.

“Nimekuwa nikifanya kazi hii tangu mwaka 1999, ninaweza kumudu kazi zote ingawa nalazimika kupangilia muda wangu na kuutumia vema, namshukuru Mwenyezi Mungu ananiwezesha.

“Uzuri ni kwamba katika dunia ya sasa ya sayansi na teknolojia unaweza kufanya jambo lolote kwa kutumia komputa yako.

“Chochote unachohitaji unaweza kukitafuta mtandaoni mradi ujali muda, nasoma mno kupata ‘refference’ mbalimbali kwa njia ya mtandao.

“Inawezekana, ndiyo maana unakuta mtu ni profesa wa uchumi na wakati huo huo profesa wa sheria, wakati ule nasoma niligundua kuna matatizo mengi watu wanapata hasa katika wakati wa kupata matibabu.

“Tatizo naona wengi wanadhani kupata huduma ya matibabu ni kama vile ‘favour’ lakini kumbe ni haki yao, inapotokea amepata matatizo wengi hawajui pa kupata haki zao.

“Ndiyo maana niliamua kubobea zaidi katika sheria ya matibabu ili kuwasaidia hata kwa ushauri, hivyo utaona imekuwa rahisi kwangu kwani tayari ni daktari na wakili sasa nimebobea upande huo wa sheria ya matibabu ili kuwasaidia watu,” anasema.

Anasema hata diplomasia ya uchumi aliyoisoma inamsaidia katika maisha yake kwani amekuwa akitoa ushauri kwa watu mbalimbali pindi wanapotaka kusaini mikataba hasa ile mikubwa.

“Elimu yangu hiyo naitumia hata katika maisha yangu ya kila siku,” anasema Wakili Kikondo.

Kikondo ni nani?

Ni mtoto wa pili kati ya watoto tisa waliozaliwa katika familia ya Mohamed Kikondo na Rukia Maulid yenye makazi yake huko Ujiji mkoani Kigoma. 

Anasema alizaliwa mnamo mwaka 1974 na kwamba katika familia yao hiyo watoto wa kiume walizaliwa sita na wa kike watatu.

Maulid anasema ndoto yake tangu akiwa mdogo ilikuwa kuja kuwa mwanasheria mbobezi.

Sasa ni daktari bingwa wa uchunguzi wa magonjwa ya moyo, na wakili aliyebobea katika upande wa sheria ya matibabu.

Anapatikana kwa simu namba +255 713 304 149 yupo tayari kukusikiliza na kukushauri kisheria.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement