NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM
MIRATHI ni utaratibu unaotumika kugawa mali zilizoachwa
duniani na marehemu katika jamii nyingi za kiafrika linapofika suala la kugawa
mirathi matatizo mengi huibuka.
Baadhi ya watu huanza kugombea mali za marehemu,
mzozo huwa mkubwa na mgumu kuutatua hasa pale inapotokea kwamba marehemu
hakuacha wosia.
Wakati mwingine hata anapokuwa ameandika na kuacha
wosia ikiwa hakufuata taratibu zinazotakiwa wosia huo hushindwa kutambulika kisheria
na hivyo bado huacha matatizo mengi.
Inaelezwa watu wengi hawajui jinsi ya kuandika
wosia unaotambulika kisheria ingawa kuna changamoto kwamba wapo wanaoogopa
kuandika kwa hofu ya kujichuria kifo.
Pamoja na hayo, MATUKIO NA MAISHA imezungumza na Wakili wa Mahakama Kuu Tanzania, Maulid
Kikondo ambaye hapa anaeleza kwa kina kuhusu
umuhimu wa wosia na suala zima la mirathi.
Anasema ingawa bado jamii haina uelewa na mwamko wa
kutosha katika kuandika wosia na mirathi wapo baadhi ambao huzingatia umuhimu
wa mambo hayo hata hivyo bado kuna changamoto.
“Wakati mwingine hata marehemu anapokuwa ameacha
wosia na akaandika mirathi yake bado kuna watu wengine hujitokeza na kuyakataa
maoni yaliyoachwa na marehemu,” anasema.
Anaongeza “Labda unakuta katika hiyo jamii,
walikuwa wakiishi na marehemu kwa mizozo, migogoro inapofika suala la kufuata
kile alichokiandika wakati wa uhai wake hawakizingatii.
“Yaani inapotokea amefariki unaweza kukuta hata
wale watoto wake ambao labda waligombana naye enzi za uhai wake wanakuja na
kuanza kugombea mali za marehemu na unakuta wanataka kuchukua kila kitu chake,”
anasema.
Anasema wakati mwingine watu hujitokeza kudai mali
za marehemu ingawa enzi za uhai wake walikuwa hawamjali au hata hawaongei naye.
“Ni tofauti kabisa na jamii za nchi zilizoendelea
kwamba mtu anapofariki watoto wake wanajua wazi kama walikuwa hawaelewani wanaachana
na mali zake.
“Inabidi na sisi kama jamii inabidi tufike mahala
tuchague, wakati fulani unaishi na wazazi wako mnakuwa na mizozo mikubwa mara
nyingine hata hamtembeleani, hamsalimiani kwa muda mrefu.
“Lakini anapofariki wewe ndiyo wa kwanza kwenda
kugombani mali, matokeo yake hata wale wachache ambao waliamua kumsaidia mzazi
wako kufanya kila jambo,” anasema Wakili Msomi Kikondo (pichani).
Changamoto
Anasema hali hiyo huzua ‘tafrani’ hasa ikiwa
marehemu anakuwa amechagua watu na kuwaandika katika andiko lake la
wosia/mirathi kuwagawia mali zake.
“Labda ndiyo waliomsaidia alipokuwa hai anaamua
kuwataja ili wagawiwe mali zake ikiwa ni sehemu ya shukran zake kwao, lakini
anakuja mtu ambaye hakushiriki chochote naye anataka apatiwe mali, mizozo
huanzia hapo,” anabainisha.
Anasema kwa kawaida mizozo huwa mingi kulingana na
jinsi jamii inakosa ule uwelewa wa kutosha kuhusu masuala ya kisheria.
“Ukiangalia Sheria ya Usimamizi wa Mirathi Sura 352 inaeleza taratibu zote
za usimamizi wa mirathi kuanzia pale mtu anapofariki na jinsi gani ya kufanya
lakini ni watu wachache mno wanafahamu.
“Kimsingi inapotokea mtu amefariki jambo la kwanza
kujiuliza ni je ameacha wosia au la, ikiwa imetokea wanasema ameacha wosia,
swali la pili litakuwa je huo wosia unakubalika kisheria, kwamba taratibu za
kuandika zilizingatiwa katika huo wosia au la,” anasema.
Anasema taratibu hizo hutegemea aina ya wosia
unaoandikwa, kwa mfano ikiwa anayeandika anajua kusoma na kuandika wakati
anauandika huo wosia anatakiwa kuhakikisha unashuhudiwa na watu wawili wazima
wenye akili timamu.
Anasema wakati muhusika akiandika na kuusaini wosia
huo ni lazima watu hao wamshuhudie akiusaini wosia huo.
Hata hivyo, Wakili Kikondo ambaye amebobea zaidi katika masuala ya sheria ya matibabu anasema mara
nyingi hushuhudia watu wakiandika wosia wodini wakiwa hoi kitandani.
“Wengi nimeona waandika wosia wakiwa hoi kitandani
na wakati mwingine unakuta shahidi anakuwa mkewe au ndugu yake wa karibu,
kimsingi mke hapaswi kuwa sehemu ya shahidi.
“Matokeo yake, wengi wanapofariki unakuta hakuna
mtu anayejua kwamba aliacha wosia au wanapokwenda mahakamani wale mashahidi
wanaotajwa wakiulizwa iwapo walishuhudia akiusaini wanasema hawakuwepo,”
anasema.
Anaongeza “Kisheria hapo tayari ni utata na
mahakama inaweza kuamuru kwamba kwa kuwa wosia huo haukufuata taratibu
hautambuliki kisheria ingawa unaweza kukubaliwa iwapo ndugu na wanafamilia
watakubaliana kuuheshimu wosia husika.
“Lakini huwa ni ngumu mno kwa sababu siku zote kwenye
jamii zetu tunapoandika wosia tayari humo ndani kuna fukuto unakuta mtu labda
amezaa watoto wengi kwa mama tofauti sasa anahofia mizozo itakayotokea anaamua
kuandika wosia.
“Wosia wa namna hiyo usipofuata taratibu tayari
kuna pande mbili, tatu au zaidi unakuta zinavutana au hata ukoo nao unavutana,”
anasema.
Anaongeza “Wosia ukikosewa japo kidogo, lile kosa
dogo hukuzwa na kuwa kubwa, inapofika hapo ule wosia hautakubalika mahakamani
na itachukuliwa mtu huyo alikufa bila kuacha wosia.
“Kwa uzoefu wangu inapotokea mwanaume amezaa na
mwanamke zaidi ya mmoja unakuta kila mama anataka mtoto wake apate urithi zaidi
ya mwingine.
“Hata wale waliozaliwa wengi kwa mama mmoja wakati
mwingine changamoto hujitokeza, unakuta wametofautiana kielimu, kiuchumi na
mambo mengine mengi, ugomvi huwa mkubwa katika baadhi ya familia juu ya mali za
marehemu.
“Au kuna baadhi ya makabila, ukoo unaona ni heri
mali za marehemu zilithiwe na kaka au mdogo wa marehemu kwamba iendelee kubaki
kwenye ukoo kuliko ikirithiwa na watoto wa marehemu wakihofia zitapotea,”
anasema.
Hatua
za kuchukua
Anasema ikitokea bahati mbaya mirathi inakuwa na
shida inabidi familia ya marehemu itumie taratibu zinazotambulika kisheria
kudai haki yao.
“Kumbuka ule wosia unaweza kukubalika au
kukataliwa, ukikataliwa itachukuliwa ni sawa na mtu yule alifariki bila kuacha
wosia, lakini yule anayeandika wosia ni muhimu akumbuke kuandika msimamizi wa
mirathi yake.
“Katika kuteua msimamizi wa mirathi inahitaji
umakini, inabidi ateue mtu ambaye ni mwadilifu kweli kweli, Ingawa hata
asipoteua haibatilishi ule wosia anaouandika,” anabainisha.
Ufunguzi
wa kesi
Wakili Kikondo anasema ikiwa marehemu aliacha wosia
na katika wosia huo akataja msimamizi wa mirathi yake bado wosia huo unakuwa
haufanyi kazi hadi pale unapopelekwa mahakamani.
“Hauwezi kufanya kazi ‘automatic’, lazima kesi
ifunguliwe mahakamani, itasikilizwa na mahakama itatoa hukumu yake, yaani
haiwezekani yule msimamizi wa mali za marehemu ‘kujitapa’ kwamba ndiye
msimamizi ikiwa kesi haijapelekwa mahakamani,” anasema.
Anaongeza “Lazima upitiwe mahakamani, na apitishwe
kwamba ndiye msimamizi wa mali hizo kwa sababu baada ya hapo kuna mambo ya
msingi ya kufanya juu ya mali hizo.
Hubatilishwa
Wakili Kikondo anasema wosia huweza kubatilishwa
lakini muhusika anapoubatilisha ni lazima aandike kwamba anaubatilisha ule wa
kwanza aliouandika.
“Inahitaji umakini wa hali ya juu wakati
unapoandika wosia na kuuhifadhi, ukizagaa zagaa si jambo zuri na umakini
huhitajika pia katika kutafsiri sheria,” anasema.
Anasema mtu
anapoandika wosia ni muhimu kubaki na nakala na kwamba huwa unahifadhiwa ama
mahakama Kuu, kwa wakili au katika taasisi mbalimbali zinazotambulika kisheria.
“Kwa mfano Tanzania tunaweza kuhifadhi katika RITA lakini unaopeleka huko kuhifadhi
lazima mtu (shahidi) wako ajue ili unapofariki aweze kutoa taarifa kule
ulipohifadhi kusudi hatua zianze kuchukuliwa,” anasema.
Anaongeza “Ikitokea wosia umebatilishwa na mahakama
ile familia ya marehemu hutakiwa kwenda kukaa kikao na ukoo kisha wataandaka
muhtasari wa kikao hicho.
“Katika muhtasari huo watatakiwa kutaja mali zote
za marehemu na warithi wake pia watateua msimamizi wa mirathi hiyo, lakini kuna
tofauti kubwa ya kurithisha na kugawa mirathi.
Madeni
ya marehemu
“Kwa mfano marehemu ikiwa aliacha madeni msimamizi
wa mirathi anayeteuliwa hapo huwajibika kulipa madeni yote yaliyoachwa na
marehemu.
“Mnapotua msimamizi mteue mtu mwadilifu ingawa zipo
sheria zinazosimamia iwapo atachakachua mali za marehemu atahukumiwa kama
wanavyohukumiwa wahalifu wengine,” anasema.
Anasema msimamizi wa mirathi anapoteuliwa wanafamilia
ni lazima warudi mahakamani ambako hupewa fomu namba moja na kuijaza kuomba
usimamizi wa mirathi husika.
“Hapo watalipia gharama za faili na wataambatanisha
fomu hiyo na cheti cha kifo au kiapo cha kifo cha marehemu, kisha
wataambatanisha ule muhtasari wa kikao,” anasema.
Anasema watatakiwa kutoa tangazo katika gazeti
lolote ndani ya siku 90 ili kutoa nafasi kwa wale wanaotilia shaka kuwasilisha
malalamiko yao mahakamani.
“Kama hakuna malalamiko mahakama itampitisha yule
aliyeteuliwa kusimamia mirathi husika lakini kabla hajagawa mali hizo lazima
alipe madeni yote yaliyoachwa na marehemu,” anasisitiza.
Anasema hata hivyo wengi husahau kulipa madeni ya
marehemu mara baada ya kukubaliwa kusimamia mirathi.
“Wanapopewa kibali tu huenda kugawa mali na kuwasahau
kabisa wale waliokuwa wakimdai marehemu, ni makosa makubwa kisheria,” anasema.
Sheria
mbadala
Anasema wakati mwingine sheria ya kidini hasa ya
kiislamu huweza kutumika katika suala la usimamizi wa mirathi au sheria ya
kimila.
“Lakini ili itumike sheria ya kiislamu ni lazima
iwe marehemu alikuwa akiyaishi maisha ya dini hiyo vinginevyo hamuwezi
kuitumia, au sheria ya kimila lazima wote wawili wawe wametoka katika kabila
moja.
“Lakini ikiwa wameowana kutoka kabila tofauti hapo
sheria ya kimila haiwezi kufanya kazi katika kugawa mali za marehemu hata hivyo
katika miaka ya hivi karibuni sheria ya kimila imekuwa ikikosa nguvu kwani
mambo mengi yanakwenda kinyume na haki za binadamu,” anabainisha.
Maulid Kikondo ni Daktari na Wakili wa Mahakama Kuu Tanzania anapatikana kwa nambari, +255 713 304 149, Unaweza kuwasiliana naye ikiwa unahitaji msaada wa kisheria yupo tayari kukusikiliza.
Chapisha Maoni