Gari ikiwa imeharibika vibaya baada ya ajali kutokea, picha na mtandao
NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM
AJALI za barabarani ni janga si tu Tanzania bali
duniani kwa ujumla, Shirika la Afya Duniani (WHO) linakadiria kila mwaka watu
milioni 1.25 hufariki duniani kwa ajali za barabarani.
Kulingana na Shirika hilo, idadi hiyo ni sawa na
vifo vya watu 3,400 kila siku, takwimu za WHO zinaonesha ajali za barabarani
zinashika nafasi ya pili miongoni mwa mambo yanayosababisha vifo duniani.
Inakadiriwa asilimia 90 ya ajali hutokea katika
nchi zinazoendelea ikilinganishwa na nchi zilizoendelea huku ajali zikionekana
kusababisha vifo vingi kuliko hata maambukizi ya virusi vya ukimwi, kifua kikuu
na malaria.
Shirika hilo linaeleza kundi linaloathirika zaidi
na ajali za barabarani ni watu wenye umri wa kuanzia miaka 15 hadi 29.
Aidha, wengi wao huwa ni watumiaji wengine wa
barabara ikiwamo watembea kwa miguu, waendesha pikipiki, baiskeli.
Kwa mujibu wa WHO ajali za barabarani hutokana na
sababu mbalimbali hasa za makosa ya kibinadamu kama vile ulevi, mwendokasi,
kutokuzingatia sheria za usalama barabarani, kutokuvaa kofia ngumu na
kutokufunga mikanda.
Inaelezwa kati ya watu wanne wanaopata ajali kila
siku duniani watatu huwa ni wanaume.
Shirika hilo linakadiria nchini Tanzania kila mwaka
watu wapatao 16,000 hupoteza maisha kwa ajali za barabarani.
Shirika hilo linazionya nchi zote kwamba ikiwa
hatua hazitachukuliwa huenda hali itakuwa mbaya zaidi ifikapo 2030 kuliko
ilivyo sasa.
Nimekuwa nikiandika habari za afya kwa muda wa
zaidi ya miaka mitano sasa, hiyo imeniwezesha kushuhudia na kuzungumza moja kwa
moja (wodini) na watu mbalimbali walioathiriwa na matukio ya ajali.
Wengi wao huwa ni vijana huwa nakutana nao katika Taasisi
ya Mifupa Muhimbili (MOI) ambako hufikishwa kwa matibabu.
Nakumbuka vema tukio la ajali ya gongo la mboto
ambayo ilihusisha gari la mafuta ambalo lilianguka wakati likijaribu kupisha
gari iliyokuwa ikija mbele yake ikiwa mwendo kasi.
Wakati dereva yule akijitahidi kupishana na gari
lile lilimshinda akajipata gari yake ikiangukia mtoni, wananchi wakakimbilia
kwenda kuchota mafuta na hatimaye baadae yalilipuka na kusababisha maafa.
Niliwaona majeruhi wa ajali ile, akiwamo utingo wa
ile gari, nilibahatika kufanya naye mahojiano.. alikuwa na maumivu makali mno.
Kimsingi ajali nyingi hutokea kwa uzembe, maisha ya
watu wale yalibadilika tangu pale, wapo waliopoteza viungo vyao na wengine
walipoteza kabisa maisha yao.
Mzigo mkubwa kwa familia na Taifa, nguvu kazi
zimepotea kutokana na uzembe wa mtu mmoja aliyedaiwa kuwa katika mwendo kasi.
Na ndipo hapo linapokuja wazo la kudhibiti mwendo
kasi wa madereva, Jeshi la Polisi kwa namna moja au nyingine linajitahidi mno
kutekeleza wajibu wake katika hilo, kwa kutumia ‘tochi’ za usalama barabarani.
Hivi karibuni nilisafiri kutoka Dar es Salaam hadi
Morogoro kwa hakika nilifurahia safari yangu, zamani nilikuwa nikisafiri nakuwa
na shaka na wasiwasi wa kule ninapokwenda, Je nitafika salama.
Hali imebadilika, angalau sasa ‘wazembe’
wanadhibitiwa hata hivyo haitoshi kusema kwamba tumeweza kubadili tabia.
Nadhani kampeni ya paza sauti ‘imeleta matunda’
lakini bado tunapaswa kuendelea kuelimisha jamii yaani madereva na abiria
umuhimu wa kuzingatia alama za usalama barabarani.
Tukifuata kwa hakika alama za usalama barabarani
itatusaidia kuepuka ajali zinazoweza kuepukika na hivyo kwa pamoja tukawa
tumeokoa maisha ya watu wengi.
Ingawa changamoto inabaki kwa wenzetu wa bodaboda
ambao wengi hujifunza vichochoroni na kuingia barabarani.
Hawa huwa hawajali hii ni njia ya abiria waenda kwa
miguu au hapa natakiwa kusimama kwa sababu taa iliyowaka ni nyekundu na si ya
kijani.
Huwa wanapita tu popote ni haki yao, lakini ndio
hao ambao wengi huishia kuletwa MOI huku wakiwa viungo vyao vimeharibika vibaya
na hivyo kulazimu madaktari kukata viungo vyao kama sehemu ya matibabu.
Lazima jamii ibadilike na kuheshimu alama za
usalama barabarani ili tuepuke ajali za barabarani.
Makala haya kwa mara ya kwanza yametoka leo (Juni 4, 2018) kwenye gazeti la MTANZANIA ambalo nalitumikia
Chapisha Maoni