Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement


*Mfumo huo wanaongeza makusanyo, upatikanaji wa damu salama

*Mgonjwa anayehitaji huongezewa bila ndugu kuitwa kujitolea

*Anaporuhusiwa huwa balozi wa uhamasishaji kwenye jamii

*Utaratibu huo waondoa kero ya kukosekana kwa damu salama

NA Veronica Mrema – Mtwara

KUKUSANYA damu kutoka kwa wachangiaji wa ndugu wa mgonjwa aliyelazwa wodini ni miongoni mwa mbinu zinazotumika katika maeneo mengi nchini ili kuweza kupata damu kwa ajili ya kusaidia wale wanaokuwa na uhitaji kuweza kuokoa maisha yao.

Tathmini ya Mpango wa Taifa wa Damu Salama Tanzania (NBTS) zinaonesha pia kwamba zaidi ya asilimia 80 ya wachangiaji damu ni wanafunzi na wanavyuo.

Hata hivyo, mambo ni tofauti katika Ukanda wa Kusini ambako kuna Kanda ya NBTS, kwenyewe kiwango kikubwa cha damu salama kinakusanywa kutoka kwa wachangiaji wa hiyari.

Wachangiaji wa hiyari kutoka moja kwa moja kwenye jamii katika maeneo mengine wapo lakini si kwa kiwango kikubwa kama ambavyo Kanda ya Kusini imefanikiwa kufikia.

Hatua ambayo Meneja wa Mpango huo unaosimamiwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wa Kanda hiyo, Dk. Pendael Sifuel anasema imewawezesha kuondoa kero na malalamiko ya ukosefu wa damu hata wakati wa mapambano dhidi ya Janga la Corona.

Namna gani Kanda hiyo imeweza kufanikisha jambo hilo?

“Mgonjwa yeyote aliyelazwa wodini katika Kanda hii ya Kusini ya NBTS, ambapo tunahudumia mikoa mitatu, , Lindi, Mtwara na Ruvuma pamoja na Halmashauri za Wilaya ya Tunduru na Namtumbo, akihitaji damu, huku hatulazimishi ndugu, jamaa na marafiki waje wachangie, wajitolee damu.

“Tulishaachana na utaratibu huo, tulichofanya ni kwamba mgonjwa husika anapatiwa damu iliyopo, akishapata huduma na kupona, anaporuhusiwa kurudi kijijini, lazima aende akaripoti kwa uongozi kwamba alisaidiwa kupatiwa damu alipokuwa wodini,” anasema.

Anaongeza “Kwa hiyo, yule ambaye tulimpa huduma ya damu salama, sasa anakuwa sehemu ya uhamasishaji katika jamii yake, tunapokwenda kukusanya damu, anakuwapo na kutoa ushuhuda.

“Jamii inahamasika kujitolea damu, tuliamua kwenda moja kwa moja vijijini kwa sababu eneo hili (Kanda) ni dogo kulinganisha na Kanda nyinginezo, sisi hapa tumewekeza zaidi kukusanya damu vijijini kwa sababu hata shule zilizopo hapa ni chache, wakati mwingine huwa zinafungwa au kunakuwa na mitihani.

“Lakini kule vijijini ndiko waliko wananchi wanapata huduma zetu hospitalini, hivyo tuliona bora kupeleka elimu kule kule vijijini,” anasema.

Mtaalamu wa Maabara wa NBTS Kanda ya Kusini, Kassim Mmera akionesha mazao ya damu yaliyohifadhiwa kwenye friji zilizopo ndani ya maabara hiyo.

JINSI WALIVYOANZA

Dk. Sifuel anasema walianza kwa kuwashirikisha wazo hilo viongozi wa Serikali za mitaa na vijiji kwamba kila mtu anayepatiwa huduma ya damu salama hospitalini, anaporuhusiwa na kurudi kijijini kwanza lazima aripoti kwa uongozi wa kijiji husika.

“Tulikubaliana kwamba mgonjwa akifika kwa daktari, ikihitajika kuongezewa damu atapatiwa huduma pasipo kuambiwa kitu chochote, hatatakiwa kuleta ndugu zake kumchangia.

“Ataongezewa ile iliyokusanywa na kuandaliwa tayari kusaidia wahitaji, lakini akirudi kijijini lazima akaelezee kwamba amepatiwa huduma ya damu bure, anakuwa balozi wetu anasaidia kwenye uhamasishaji,” anasema.

Anaongeza “Hili limetusaidia mno kuongeza hamasa kwa wananchi baada ya kuona huduma kweli inatolewa bure na hakuna usumbufu wa kulazimika kuleta ndugu wala nini.

“Tukifika kule vijijini, wenyeviti na watendaji wanatueleza endapo wanapata wagonjwa ili tuhakikishe wanapata huduma,” anasisitiza.

UMILIKI KWA WANANCHI

“Kwa hiyo wananchi hapa wanamiliki mpango wa damu salama, wao ndiyo wanapanga tufanye nini, sisi tunafanya nao kazi, mwitiko ni mkubwa na mafanikio tuliyopata pia ni makubwa,” anasema Dk. Sifuel.

Anaongeza “Hii imetusaidia pia hata lilipokuja janga la maambukizi ya Virusi vya Corona (COVID – 19), sisi tulijiwekea kauli mbiu yetu tukisema damu salama Kanda ya Kusini, Corona haituwezi.

“Tulihakikisha tunafuata miongozo iliyotolewa na Wizara kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi hivyo wakati wa kutoa huduma kwa wananchi.

“Kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni, kutumia sanitizers (vitakasa mikono), vitanda pia tunaweka kwa kuzingatia umbali wa mita moja, wataalamu wetu wanazingatia mbinu zote za kujikinga na kuwakinga wale wanaokuja kujitolea kuchangia damu, tuliamini Corona haituwezi na tumefanikiwa kupigana nayo," anabainisha.

Dk. Sifuel anasema hapo kabla hawajaanza kufuata utaratibu huo (wa mfumo wananchi 'kumiliki benki ya damu) wagonjwa walipolazimika kuleta ndugu wa kuwachangia damu, walikuwa wakipata ndugu watano pekee.

“Lakini kwa kufuata utaratibu huu mpya tuliojiwekea, kwa mgonjwa mmoja anapohamasisha, tunapokwenda kijijini tunakusanya chupa 25 hadi 50,” anabainisha.

Mkuu wa Maabara wa NBTS Kanda ya Kusini, Hamis Mohamed akifafanua jinsi wanavyotumia mfumo wa kulebo mazao ya damu

WANAKIJIJI WALIUMIA

Anaongeza “Utaratibu wa zamani tuliona ulikuwa unawaumiza wagonjwa na hata ile kauli kwamba huduma hii ni bure, wengi wao walikuwa hawaoni maana yake.

“Kwa mfano kama mtu amepanga, hana ndugu hapa mjini atapataje hao ndugu wa kumchangia damu ilia pate huduma,!?,” anahoji.

Anasema kwa hiyo kwa utaratibu mpya, akilazwa anapewa damu akitoka anakwenda kuhamasisha, kule kwenye jamii ndiko tunapopata wachangiaji wa hiyari wengi.

“Kuliko kutegemea ndugu wa mgonjwa aliyelazwa wodini ambapo pia tulibaini kwamba wengi wanapopona huwa hawaoni tena umuhimu wa kurudi kuchangia damu, sasa kwa mfano kama watakaa miaka mitano hadi 10 hawajapata mgonjwa, hautawapata kuja kuchangia,” anasema.

Daktari huyo anaongeza “Lakini akipewa mgonjwa mmoja, akienda akihamasisha tunapata wachangiaji wa hiyari wengi, kwa hiyo sasa kila mtu anamiliki damu salama.

MAHITAJI YA KANDA

Anasema kwa siku ni wastani wa chupa 100 ikiwa hakuna mahitaji ya dharura na kwamba endapo dharura inatokea huweza kutuka chupa kati ya 120 hadi 150 kwa siku.

“Kwa siku mahitaji yetu si makubwa, damu tunayokusanya inatosheleza, kwa mfano kwa Hospitali ya Mkoa mahitaji yao kwa mwezi ni chupa 300, si matumizi makubwa sana,” anabainisha.

WAJAWAZITO WAONGOZA

Anasema katika Kanda hiyo kundi linaloongoza kwa matumizi ya damu salama ni lile la wajawazito kwa zaidi ya asilimia 60 hasa katika kipindi cha kujifungua likifuatiliwa na kundi la watoto kwa asilimia 20.

“Kundi jingine ni la majeruhi wa ajali na wale wanaokabiliwa na magonjwa mengine mbalimbali. Ndiyo maana tunasema tusiwasumbue hasa hawa wakina mama, wakija kujifungua, wanahudumiwa, wanaenda nyumbani, wakienda huko wanatusaidia kuhamasisha jamii,” anasema.

Anaongeza “Tunakusanya na kusambaza hata kwa hospitali binafsi na zile za ‘misheni’ zilizopo kwenye kanda hii ikiwa wanahitaji na si kwa hospitali za Serikali pekee.


UWEZO WA MAABARA

Dk. Sifuel (pichani) anasema NBTS katika Kanda hiyo ilianzishwa mwaka 2007 wakati huo ikiwa chini ya CDC na kwamba ilifanya kazi vizuri hadi mwaka 2015 wafadhili hao walipoondoka na kuchukuliwa rasmi na Serikali chini ya Wizara hiyo.

“Tangu hapo utendaji kazi kwa asilimia 100 unatekelezwa chini ya Serikali, tangu ilipochukuliwa na Serikali hadi sasa tumepata mafanikio mengi ikiwamo hiyo ya kuongezeka kwa hamasa ya wananchi,” anasema.

Anaongeza “Aidha, kiwango cha ukusanyaji damu nacho kimekuwa kikiongezeka, mwaka 2017/18 tulikusanya chupa za damu 6,444, mwaka 2018/19 tulikusanya chupa 9,510 na mwaka 2019/20 kufikia sasa tumekusanya chupa 11,500.

“Hii ni sawa na ongezeko la asilimia 113, tumevuka lengo kwa sababu tumeweza kukusanya zaidi ya asilimia moja ya wakazi (population), ushirikiano tunapata kule vijijini, idadi ya wachangiaji inaongezeka mwaka hadi mwaka.

Anasema hata katika Halmashauri wanazoshirikiana nazo kwa mwaka jana ziliweza kuvuka lengo ambapo zilikusanya chupa za damu 24,780 sawa na 112% ya malengo waliyojiwekea.

“Tunafanya vizuri tunaishukuru Serikali kwa sababu imekuwa ikisimamia vizuri, tumepata mashine za kisasa za upimaji kwa makundi ya damu na magonjwa manne (Ukimwi, Homa ya Ini B na C na Kaswende).

“Kwa mashine tulizokuwa nazo awali majibu yalikuwa yanatoka ndani ya siku tatu tangu tulipopokea sampuli na kuzichunguza, kwa mashine hizi mpya sasa tuna uwezo wa kutoa majibu ndani ya siku moja,” anabainisha.

Anaongeza “Ikiwa kuna dharura, kwa mfano labda Halmashauri inahitaji haraka, kwa mashine tulizonazo sasa tunao uwezo wa kuzifanyia kazi sampuli tulizopokea na kutoa majibu ndani ya saa tatu na kuwarudishia.

“Uwasilishaji wa matokeo ya majibu ya sampuli tulizopokea unafanyika kupitia mfumo maalum na mashine hizi zina uwezo wa kuchunguza zaidi ya sampuli 100 kwa saa moja na dk. 10,” anasisitiza Mkuu wa Maabara hiyo, Hamis Mohamed.

Anasema wanao uwezo pia ndani ya maabara hiyo kuchakata mazao ya damu na kwamba plasma na chembe hai nyekundu ndizo ambazo hutumika kwa wingi kuliko chembe sahani katika Kanda hiyo.

“Hata hivyo, chembe sahani huwa tunatengeneza kwa oda maalum kutoka kwa daktari kwa sababu huwa zina uwezo wa kukaa ndani ya saa moja hadi nane ziwe zimetumika, vinginevyo inaharibika, haifai tena kwa matumizi,” anabainisha.

Anaongeza “Kwa upande wa plasma zenyewe huweza kukaa hadi miezi 11 tangu imetengenezwa ndipo inaharibika, ndani ya dakika 14 hadi 20 tuna uwezo wa kupata pakiti nne za damu na kuzihifadhi kwenye friza katika kiwango cha baridi kinachoshauriwa kitaalamu tayari kwa matumizi.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement