Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement


Na Veronica Mrema – Dar es Salaam

Kipo kisa halisi cha mtoto (jina na umri vinahifadhiwa), ambaye anadaiwa kubakwa kwa zaidi ya miaka mitatu mfululizo na baba yake mzazi, Jijini Dar es Salaam.

Mama yake mzazi alitengana na mumewe tangu mtoto huyo  alipokuwa na umri mdogo, aliachwa kwa baba yake.

Baba huyo baadae alioa mke mwingine ambaye alikuwa akifanya kazi katika moja ya vituo vya mafuta (sheli) jijini humo, alikuwa akiienda zamu usiku.

Inadaiwa ni katika nyakati hizo za usiku wakati mama mlezi alipokuwa zamu kazini, mtoto alibaki nyumbani na baba yake ni hapo alipoanza kumuingilia kimwili tangu akiwa elimu ya awali (chekechekea).

Kisa hiki cha kusikitisha ni miongoni mwa visa vilivyoripotiwa katika Kituo cha One Stop Center kinachotoa msaada wa moja kwa moja kwa wahanga wa vitendo vya ukatili wa kijinsia na kingono, kilichopo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala, Dar es Salaam.

Katika mahojiano maalum na MATUKIO NA MAISHA BLOG,  Ofisa Ustawi wa Jamii wa kituo hicho, Asia Mkini anasimulia zaidi, ilidaiwa baba alikuwa akimbaka mtoto wake huyo wa kumzaa akimuahidi kumsomesha afike mbali ki-elimu.

“Alitumia vitisho kwamba endapo atasema kwa watu atamsitishia huduma zote anazompa ikiwamo kumlipia ada shuleni, hivyo safari yake ya masomo itaishia njiani.

“Kwa kuwa wazazi wake walikuwa wametengana na inaonesha mama mlezi hakuwa akimfuatilia kwa ukaribu mtoto huyu, hakuna aliyeweza kubaini mapema juu ya vitendo alivyokuwa akifanyiwa,” anasimulia.

Anasema ni hadi pale alipofika darasa la tatu ilipobainika na kisa hicho kufikishwa kituoni hapo ikiwa imepita takriban miaka minne tangu alipoanza kuingiliwa kimwili.

Anasema mwalimu wake ndiye alimbaini kupitia rafiki wa shuleni ambaye naye aliambiwa na mdogo ‘mtu’ aliyeshuhudia siku moja, baba yao alipokuwa akimbaka dada yake nyumbani kwao.

“Yule mdogo alitunza siri kwenye moyo wake hatimaye alishindiwa na kumsimulia rafiki yake wa shuleni ambaye alikwenda kumueleza mwalimu.

“Mwalimu alichukua hatua kumleta kituoni, baada ya vipimo tulibaini kweli alikuwa akiingiliwa, tulijitahidi mno kufuatilia kisa hiki, tulikuwa tunaendelea vizuri na ufuatiliaji wake, yule baba alikana, alikuwa mkali, alitishia kusitisha huduma zote alizokuwa akimpa mtoto, hapo ndipo changamoto ilipokuja.

KIPATO DUNI

“Mama wa mtoto alitaka limalizwe kifamilia, kwamba ikiwa baba atafungwa, yeye hataweza tena kumuhudumia mtoto kwa sababu uwezo wake kiuchumi si mzuri, ndoto zake za kielimu zitakuwa zimeishia njiani, jambo ambalo alidai hatamani litokee,” anasema.

Anaongeza “Makubaliano ya kifamilia yalipelekea mtoto yule kukosa haki yake kwa sababu kesi haikuweza kuendelea kama ambavyo tulitamani iwe.

Asia anasema huo ni mfano wa kisa kimoja kinachosikitisha  kilichokwama kufikia tamati, haki ya mtoto ipatikane kwa sababu tu ya makubaliano ya kifamilia.

“Ni utamaduni ambao bado upo kwenye jamii na kikwazo katika kupatikana kwa haki za watoto wanaofanyiwa vitendo vya ukatili hasa wa kingono (ubakaji na ulawiti),” anasisitiza.

Afisa Ustawi wa Jamii wa Kituo cha One Stop Center kilichopo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala (mwenye tisheti nyeupe na kofia) akizungumza na wanafunzi hivi karibuni (pichani na Veronica Mrema).

VITISHO

Afisa Ustawi wa Jamii huyo anasema vitisho hutumiwa na wabakaji kwa kiasi kikubwa ‘kuwafumba mdomo’ watoto wasiseme vitendo vya kikatili wa kijinsia na kingono wanavyofanyiwa.

“Mara nyingi wanapoletwa hapa kituoni, tunapowahoji baadhi ya watoto hukataa kuwataja waliowafanyia ukatili, kwa sababu wengi wanaowafanyia ama kwa kuwabaka au kulawitiwa unakuta ni wakubwa waliowazidi umri.

“Huwa wanatumia vitisho mbalimbali, wapo baadhi ya watoto tunapofanikiwa kuwahoji hutueleza walishikiwa visu, walifungwa mdomo au kuambiwa wazi wazi wakisema tu mama au baba  yake atauwawa.

“Wengine hutueleza, wale wanaowafanyia ukatili kama ni baba mzazi anakuwa amemtishia kutokumlipia ada ya masomo yake shuleni,” anabainisha.

Anasema kwa kuwa wana mbinu nyingi kituoni hapo za kuweza kuwashawishi watoto kuwataja wale waliowafanyia ukatili, huzitumia ipasavyo, hatimaye kupata undani wa kile ambacho mtoto husika amefanyiwa.

“Kwa wale wenye umri mdogo, tuna vifaa vya kumpatia kuchezea au tunamunulia vitu vya kutafuna - tafuna, tunamuweka karibu zaidi anatuzoea na anatuweka wazi kila kitu.

“Wapo wanaotueleza wazi kwamba, kwa mfano aliyenibaka ni mzazi, mjomba, mtu wa karibu lakini alinitisha nisisema," anabainisha.

anaongeza "Kiujumla jamii inaonekana haipo karibu na watoto ndiyo maana wanapofanyiwa vitendo vya kikatili na watu wasio wema huchelewa kugundulika, inabidi kubadilika.

USHAHIDI HUPOTEA

Asia anasema katika mazingira hayo ya mtoto kuchelewa kuweka wazi aliyemfanyia ukatili hasa wa kingono wakati mwingine ushahidi hupotea na hii ni changamoto nyingine katika ufuatiliaji wa kupata haki.

“Siku ambapo mnakuja kujua kwamba mtoto anafanyiwa kitendo hicho tayari ushahidi umepotea, kwa mfano mtoto anaweza kusema amekuwa akilawitiwa kwa miaka mitatu mfululizo.

“Sasa ukiangalia hili, inasikitisha lakini unakuta tayari mtoto ameshaharibika,” anasema.

Koplo Salome Izina wa Kituo cha Polisi OysterBay ambaye ndiye anayesimamia katika dawati la polisi ndani ya One Stop Center, hospitalini hapo anasema ndani ya saa 72 tangu mtu alipofanyiwa ukatili wa kingono au kijinsia ushahidi unapaswa kukusanywa.

“Inapaswa kukusanywa mapema kwa sababu, kwa mfano, ikiwa mtu amebakwa, akichelewa kufishwa kituoni ndani ya muda huo ni rahisi kupoteza ushahidi hasa endapo atanawa kwa maji katika sehemu zake za siri.

“Anapaswa kuwahishwa kituoni ili ushahidi ule ukusanywe kabla hajanawa maji, vivyo hivyo kwa mtu aliyefanyiwa ukatili mathalani wa kupigwa,” anasema Koplo Salome.

Anaongeza “Ndiyo maana lilikuja wazo la kuwa na kituo cha moja kwa moja ili kusaidia wananchi waliofanyiwa ukatili hapa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala, ndani ya kituo anapatiwa huduma ya kuona na ofisa afisa ustawi wa jamii, daktari, muguzi na polisi.

“Huduma hizi hupatiwa haraka kwa kuonana na afisa ustawi wa jamii, daktari ambaye atamfanyia vipimo ndani ya muda, haraka na kwa wepesi na askari atahakikisha anamsimamia, anamsindikiza kupata huduma hizo.

“Hii inasaidia kuepusha kupoteza muda na hata kuweka ‘mwanya’ wa kufikia makubaliano ya kifamilia au ya kijamii dhidi ya mtuhumiwa na hatimaye haki ya muhusika aliyetendewa ukatili kuweza kupatikana kwa wakati,” anasema.

‘KICHAKA CHA WEMA’

Koplo Salome anasema wapo baadhi ya watu wanaofanya vitendo hivyo hujificha katika wema na hata kuwasindikiza waathirika kituoni hapo.

“Kuna kisa kimoja, mbakaji alimleta mwenyewe aliyembaka, alikuwa mtoto, tayari alikuwa amemtishia asiseme ukweli, lakini sisi tuna mbinu zetu tunazozitumia, mtoto alitueleza aliyembaka ndiye huyo huyo aliyemleta kituoni, tulimkamata, ushahidi ulipokamilika alifikishwa mahakamani na haki ya mtoto ilipatikana,” anabainisha.

Anaongeza hapa kituoni kila huduma inatolewa kwa wakati ikiwa ni pamoja na Pf3 badala ya muathiriwa kwenda kuzunguka huku na kule ili aipate fomu hii na hivyo kuziba 'mwanya' wa kupoteza ushahidi na majadiliano kukubaliana na kuyamaliza kijamii.

“Tukishamuhudumia aliyefanyiwa vitendo vya ukatili, askari wa kituo anahakikisha faili limefunguliwa na maelezo yameandikwa kisha anakwenda kupata namba ya jalada la kesi kituo cha polisi kinachohusika katika eneo ukatili ulipofanyika.

“Kwa mfano Kinondoni, atapelekwa huko atapatiwa mpelelezi, jalada litapelekwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kisha mahakamani kwa ajili ya kesi kusikilizwa na kutolewa maamuzi ili haki ipatikane,” anabainisha.

Anasema katika kesi wanazopokea asilimia 87 ni za watoto na wanawake na kwa upande wa wanaume ni asilimia chache.

Afisa Ustawi wa Jamii wa Kituo cha One Stop Center kilichopo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala (mwenye tisheti nyeupe) na Koplo Salome Izina wa Oyster Bay na Kituo hicho, wakizungumza na mzazi hivi karibuni (picha na Veronica Mrema).

HATUA ZA MWANANYAMALA

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala, Dk. Daniel Nkungu anasema huduma hiyo jumuishi (One Stop Center) kwa waathirika wa vitendo vya ukatili imekuwa msaada mkubwa kwa wananchi.

“Data zetu ambazo tumezichakata hivi karibuni zimetuonesha watu zaidi ya 105 wamepita na kupata huduma katika kituo hiki katika kipindi cha mwaka 2018 tulipoanzisha hadi kufikia sasa (Novemba), 2020,” anabainisha.

Dk. Nkungu anaongeza “Kabla ya kuanzisha huduma hii jumuishi tulikuwa tunapokea watu wengi walioathiriwa na vitendo vya ukatili wa kijinsia na kingono kupitia mifumo yetu ya hospitali lakini walipoondoka baadhi yao tulishindwa kufuatilia taarifa zao kwani hawakurejea tena hospitalini.

“Vile vile, wapo ambao walikuwa wanafika hospitalini wakati ushahidi ukiwa umekwisha kupotea, unakuta mtu amezunguka huku na kule, kwa mfano kutafuta Pf3, bila kujua kwamba muda wa kukusanya ushahidi unakwisha na unaweza kupotea,” anasema.

Anasema bado jamii haina uelewa kwamba katika hospitali hiyo kunatolewa msaada kupitia huduma hiyo jumuishi.

“Tunazidi kutoa elimu ili wajue pale Mwananyamala huduma hizi zinapatikana kupitia njia mbalimbali kwa mfano hivi karibuni tulishiriki katika Wiki ya Kitaifa ya Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa Yasiyoambukiza yaliyofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam.

“Maofisa wote walioko ndani ya kituo hiki jumuishi walikuwapo uwanjani kuelimisha jamii kuhusu huduma hii,” anasema.

Anaongeza “Kwa sababu katika kipindi hicho cha mwaka 2018/20 ingawa watu 105 walipatiwa msaada katika kituo bado kuna watu zaidi ya 200 walipita katika mifumo ya ndani ya hospitali.

“Utaona ni idadi ndogo ambayo ilipita kituoni bado idadi kubwa ilipita kwenye mifumo yetu ndani ya hospitali, sisi tunatamani wote hawa wangepita kwenye mfumo wa kituo ili kupata msaada wa haraka zaidi na kuweza kupata haki.

“Lakini tunashukuru kwamba jitihada za kusaidia jamii tumeweza kuwafikia hawa 105 waliopita kituoni kwa sababu pengine kama kisingekuwepo huenda tusingewapata kabisa hata katika mifumo yetu ya hospitali,” anasisitiza.

Dk. Nkungu anaongeza “Kesi nyingi zinazorekodiwa kulingana na ripoti zetu ni za ubakaji na wengi waliokumbana na jambo hilo ni wa mabinti walio katika rika balehe kati ya miaka 13 hadi 18, kwa upande wa watoto wa kiume wanaolawitiwa pia zimerekodiwa ingawa si nyingi kama za watoto wa kike.

“Migogoro ya kifamilia si mingi, ikiwa kesi inafika mahakamani daktari wetu anahusika moja kwa moja kwenda kutoa ushahidi wa kimaabara na daktari anayemuhudumia mwathirika ni mmoja ili kuweza kufuatilia kwa ukaribu mwenendo wake wa matibabu.

“Tofauti na akija kwenye mfumo wa hospitali ambako leo atakutana na daktari huyu aliyepo kliniki, kesho au siku nyingine akirudi anakutana na daktari mwengine kliniki,” anasema.

Anasongeza “Kwa ujumla huduma zote zinazotolewa ndani ya kituo hiki zinamsaidia mwathirika kutokuzunguka mno pasipo kupata ufumbuzi wa changamoto aliyokumbana nayo.

UKATILI HAUKUBALIKI

Novemba 20, kila mwaka Tanzania huungana na nchi nyingine duniani kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Haki ya Mtoto ambayo 2020 yamepewa kauli mbiu isemayo "Dunia Salama kwa kila Mtoto Inawezekana: Chukua Hatua".

Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazopambana kujenga Familia Bora, Taifa Imara kuelekea 2030 ambapo Malengo Endelevu ya Dunia (SDGs) ya Umoja wa Mataifa (UN) yamekusudia nchi wanachama kutimiza.

Kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii kwa kushirikiana na wadau mbalimbali likiwamo Jeshi la Polisi Tanzania wamechukua hatua mbalimbali ili kuweza kuisaidia jamii dhidi ya vitendo vya ukatili hususan wa kijinsia na kingono.

Jamii imekuwa ikipatiwa elimu kuhusu haki za wanawake na watoto, mijadala nayo ikiibuliwa kupitia makongamano yanayoandaliwa yanayowaleta pamoja wadau tofauti tofauti kujadiliana ili kupata maoni yao kusaidia kuongeza nguvu za kukabili vitendo vya ukatili nchini.

Kampeni mbalimbali nazo huandaliwa na kufanyika nchini ili kuifikia jamii kwa ukubwa zaidi kuielimisha kwa mfano kampeni ya hivi karibuni iliyopewa jina 'Twende Pamoja, Ukatili Tanzania sasa Basi'.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Idara ya Maendeleo ya Jamii, Dk. John Jingu anasema jitihada zote hizo zinafanyika kwa sababu vitendo vya ukatili kwenye jamii hasa kwa watoto na wanawake nchini kamwe haviwezi kukubalika.

Anasema Serikali imefanya mambo mbalimbali katika kuhakikisha vitendo vya ukatili wa kijinsia na kingono vinatokomezwa kwenye jamii.

Anataja mambo hayo ni pamoja na uanzishwaji wa Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto, uanzishwaji wa Kamati za Ulinzi za Wanawake na Watoto, uanzishwaji madawati ya Polisi ya Jinsia na Watoto na kuhamasisha jamii kwa kutoa elimu ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Dk. Jingu anasisitiza pamoja na jitihada hizo, uwepo wa makazi bora katika jamii ni moja ya njia ya kupunguza vitendo vya ukatili wa kijinsia hasa dhidi ya wanawake, watoto na wazee.

"Ni jukumu letu jamii kuwalinda na kuwatunza wanawake, watoto na wazee dhidi ya vitendo vya ukatili vinavyoweza kuwakabili," anasema.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement