Picha inayoonesha mfumo wa uzazi wa mwanamume
Na Veronica Romwald, Dar es
Salaam
SI jambo rahisi hata kidogo kukaa
ndani ya chumba cha upasuaji na kushuhudia jinsi ambavyo madaktari wanafanya upasuaji
kumtibu mgonjwa aliyelazwa mbele yao.
Kama una ‘roho nyepesi’ lazima utatamani
au utaomba kabisa kutoka nje ya chumba hicho tena hasa hasa ikiwa ni mara yako
ya kwanza kuingia ndani ya chumba hicho.
Hivi karibuni, nikiwa pamoja na
waandishi wenzangu wa vyombo vingine vya habari tulipata fursa ya kuingia
katika chumba namba mbili cha upasuaji katika Hospitali ya Taifa Muhimbili
(MNH).
Katika chumba hicho madaktari
bingwa wa upasuaji wa watoto wa Muhimbili na wenzao wa Hospitali ya King Faisal
ya nchini Saudi Arabia walikuwa wanafanya upasuaji kwa njia ya matundu (laparoscopic).
Niliona baadhi wakiogopa kutazama
kilichokuwa kikiendelea binafsi nilijipa moyo konde na kushuhudia yote
yaliyokuwa yakifanyika humo kwa zaidi ya saa mbili.
Baada ya madaktari kumuandaa mgonjwa,
mmoja alisoma orodha ya wanaoshiriki upasuaji huo kisha daktari aliyekuwa
akiongoza upasuaji huo alifanya sala, wote wakaitikia amina. Ni utaratibu ulionivutia.
Upasuaji huu ulifanyika kwa siku
kuanzia Februari 20 hadi 23, mwaka huu kwa watoto sita waliokuwa na matatizo
mbalimbali.
Kati yao kuna ambaye alifanyiwa
upasuaji wa kurudisha ndani utumbo wake ambao ulikuwa unatoka nje kila
alipokuwa akijisaidia haja kubwa.
Wapo waliofanyiwa upasuaji wa kushusha
kokwa za korodani, kufungua njia ya haja kubwa, katika makala haya nitagusia tatizo
la kutoshuka kwa kokwa za korodani.
Unapozungumzia viungo muhimu
katika mwili wa mwanamume basi huwezi kuacha kutaja korodani. Hiki ni kiungo
cha kipekee ambacho kazi yake kuu ni kuzalisha mbegu za kiume na homoni za
kiume iitwayo testosterone.
Korodani inaposhindwa kufanya
kazi yake sawa sawa hushindwa kuzalisha mbegu pamoja na homoni za kiume na
matokeo yake mwanamume hushindwa kutungisha mimba.
Kawaida mwanamume anazo korodani
mbili, moja katika upande wa kushoto na nyingine upande wake wa kulia. Korodani hutengenezwa tumboni na baadae hushuka
hadi katika vifuko vyake vilivyoko nje ya mwili wa mwanaume.
Jinsi zinavyotengenezwa
Daktari Bingwa wa Mfumo wa Njia
ya Mkojo (Urolojia) wa Muhimbili, Ryuba Nyamsogoro anasema hutengenezwa ndani
ya tumbo la mtoto wa kiume, wakati mimba ikiwa katika kipindi cha kati ya mwezi
wa sita na saba tangu ilipotungwa.
Anasema baada ya korodani kutengenezwa
katika kipindi hicho tumboni mwa mama wakati wa ujauzito, huanza kushuka
kuelekea kwenye vifuko vyake kupitia mrija wake wa Gubanakulamu.
Anasema hata hivyo muda wa
korodani kushuka kutoka tumboni mwa mtoto kuelekea katika vifuko vyake hivyo
unapofika kuna wakati mwingine hutokea zikawa
hazijashuka kutokana na matatizo mbalimbali.
“Hali hiyo huitwa korodani
zisizoshuka, Wanaume wengi hujikuta
wakiwa na korodani moja isiyoshuka ingawa wakati mwingine huweza kutokea zote
mbili zisishuke ila hii huwa ni mara chache mno,” anasema.
Daktari huyo anasema tafiti
mbalimbali zinaonesha kwamba katika vizazi hai 100 vya watoto wa kiume kila
mwaka ulimwenguni wanne huzaliwa wakiwa na tatizo hilo.
Sababu za kutoshuka korodani
Dk. Nyamsogoro anasema hata
hivyo hakuna dalili zozote ambazo mjamzito anaweza kuziona ili kujua kuwa mtoto
aliyembeba tumboni atazaliwa akiwa na tatizo hilo. Isipokuwa zipo sababu mbalimbali ambazo huweza
kuchangia mtoto kupata tatizo la korodani kutoshuka.
Mashine ambayo madaktari huitumia kufanya upasuaji wa kutoboa matundu
“Sababu moja wapo ni uchache wa
homoni za kiume kwa mtoto iitwayo androgen.
Homoni hii ya androgen ni ya muhimu
mno kwa ajili ya viungo mbalimbali vya mwanamume sasa inapotokea zikapungua
kwenye mwili wa mtoto husababisha hitilafu kwa viungo vyake mbalimbali ikiwamo
korodani,” anasema.
Anataja sababu nyingine ni
hitilafu ya korodani yenyewe pamoja na mrija wake uitwao ‘gubanakulamu’ambapo
hitilafu hiyo hupunguza uwezo wa kushuka kwa korodani husika.
“Sababu nyingine ni mgandamizo
mdogo tumboni kwa mtoto husika. Ili korodani ishuke kutoka tumboni na kwenda
kwenye mfuko wake huhitajika kuwapo kwa msukumo ‘pressure’ ya kutosha kutoka
ndani ya tumbo. Sasa ikiwa msukumo
uliopo hautoshi, husababisha
korodani kutoshuka. Mgandamizo huo hutokana na kuwapo kwa viungo vya kawaida
vya mwili kama vile figo, ini, utumbo na vinginevyo,” anasema.
Daktari Bingwa wa Upasuaji wa
Watoto, Zaituni Bokhary anasema katika idara hiyo kila mwezi hupokea watoto wawili
hadi watatu wenye tatizo hilo.
Zikibaki tumboni, hazai
“Kimsingi kokwa zinapaswa
kushuka na kukaa katika vifuko vyake vya korodani ambavyo vipo nje ya mwili wa
mwanamume. Inapotokea zimebaki ndani ya tumbo ni hatari,” anasema.
Anasema mtoto ambaye kokwa zake
hazijashuka kwenye vifuko vya korodani huwa katika hatari ya kushindwa
kuzalisha pindi atakapofikia umri wa kuzaa.
“Uwezekano wa mtoto ambaye kokwa
zake zimebaki tumboni kushindwa kuzalisha ni mkubwa mno ikilinganishwa na
wengine ambao kokwa zao zimeshuka kwenye vifuko ipasavyo,” anasema.
Anasema iwapo kokwa hazijashuka
mahala pake mtoto huhitaji kufanyiwa upasuaji wa mapema ili kuzishusha kumuepusha
na hali hiyo.
“Ndiyo maana tuliwafanyia
upasuaji watoto hawa ili kuzishusha kokwa zao, upasuaji huo ulifanyika kwa njia
ya kisasa ya matundu madogo.
“Upasuaji huo uitwao kitaalamu (Laparoscopic)
huu ni tofauti na ule wa kufungua tumbo (open surgery), hapa tunakuwa tunatumia
vifaa maalumu kutoboa matundu kufikia eneo ambalo tunalihitaji na kuanza
kufanya upasuaji,” anasema.
Anasema mmoja wa watoto hao ana
umri wa miaka minane ambaye mwishoni mwa mwaka jana alifanyiwa upasuaji wa
awali wa kuzisogeza kokwa zake karibu zaidi na korodani.
“Huyu kokwa zake zilikuwa mbali
mno tukazisogeza hivyo tumekamilisha upasuaji huo na tayari tumezishusha kokwa
kwenye korodani na hivyo kumtoa katika hatari hiyo,” anasema.
Daktari huyo anasema kufanikiwa
kwa upasuaji huo ni hatua kubwa kwa hospitali hiyo ambayo sasa inatara
mkubwa kufanyika katika hospitali hiyo ambayo
inatarajia kufanya mageuzi makubwa ya kimatibabu.
Utajuaje kokwa hazijashuka
Dk. Nyamsogoro anasema mara
nyingi huwa wanaweza kutambua tatizo
hilo la kutokushuka kwa korodani kwa kutumia njia kuu mbili.
Anataja njia hizo kuwa ni kuona
na kugusa, kwa kuona huwa wanabaini tatizo kwa kuzitazama tofauti iliyopo
kwenye ngozi ya mfuko wa korodani.
“Ukitazama vifuko vya korodani
ya mtoto mwenye tatizo utaona ngozi ya upande ambao haijashuka ipo tofauti na
ile ambayo imeshuka. Ile ambayo haijashuka utaona ngozi yake haijakomaa sawa
sawa na iwapo utaigusa utakuta haipo kabisa.
“Wakati mwingine unaweza kukuta
ipo katika sehemu ya juu eneo la tumboni au kwenye ‘kinena’ na au kwa ndani ya
tumbo lakini siwashauri wazazi kuwagusa watoto kwa sababu wanaweza kuwaumiza ni
vyema wawalete hospitalini tuwachunguze,” anasema.
Daktari huyo anasema hiyo ni kwa
sababu wakati mwingine pamoja na kutumia njia hizo za kuona na kugusa huwa ni
vigumu kuweza kubaini tatizo hadi wanapokwenda kuchunguza kwa kutumia vipimo
maalumu.
“Hivyo mara nyingi huwa
tunatumia vipimo vya MRI na Ultra sound. MRI ni kipimo kizuri zaidi kwani ina
uwezo wa kutubainishia hadi mahala ambako korodani imejificha,” anasema.
Anasema hata hivyo mara nyingi
huwa wanawashauri wakunga kuhakikisha wanawachunguza watoto punde tu baada ya
kuzaliwa kwani huwa rahisi kubaini kama watakuwa wana tatizo hilo.
“Huwa pia tunawashauri wazazi na
walezi wanaowalea watoto wachanga kuwa wanawachunguza maana ni rahisi na wao
kuweza kuona kama kuna tofauti kati ya korodani moja na nyingine na iwapo
watazibaini basi wawapeleke hospitalini,” anasema.
Hugeuka kuwa saratani.
Dk. Nyamsogoro anasema katika
kliniki yao ya Ulorojia wamekuwa wakipokea hadi watu wazima wanaosumbuliwa na
tatizo hilo la korodani kutoshuka.
“Wengi wao wapo katika umri wa
kati ya miaka 25 hadi 30. Lakini kwa kuwa wanakuwa wamechelewa mno kuja
hospitali matibabu yao huwa ni magumu mno,” anasema.
Anasema kutokana na ugumu wa
matibabu hayo matokeo yake hulazimika kufanyiwa upasujia wa kuiondoa korodani
husika kwani iwapo itaachwa huko ndani ilikojificha madhara makubwa huweza
kutokea siku za usoni za maisha yake.
Madhara yenyewe
Daktari huyo anasema iwapo
korodani hiyo itaendelea kubakia huko ndani ya tumbo husababisha maji yaliyoko
tumboni kuteremka chini kupitia mrija wa korodani hali ambayo baadae
husababisha tatizo la ngiri maji (henia).
“Tumboni kuna maji maji mfano wa
mate, korodani isiposhuka kupitia mrija wake matokeo yake ni kwamba mlango wa
kuipitisha ili ikae kwenye sehemu yake huendelea kubakia wazi ukisubiri ishuke.
“Kwa hiyo maji maji hayo hutumia
uwazi huo kushuka ndipo inatoke tatizo la ngiri maji (henia) na wakati mwingine
mnaona watoto wanapata hadi tatizo la busha,” anafafanua DK. Nyamsogoro.
Anasema hata hivyo wakati
mwingine huweza kutokea korodani ya mtoto ikashuka lakini bado mlango huo
ukabaki wazi na ndio maana upo umuhimu wa kwenda kumpima afya ya korodani zake
kila baada ya kipindi fulani.
Athari zaidi
Dk. Nyamsogoro anasema athari
nyingine inayoweza kutokea iwapo korodani husika itaendelea kubakia ndani ya
tumbo ni kugeuka kuwa saratani.
Anasema korodani isiyoshuka ina
uwezekano mkubwa wa kugeuka kuwa saratani ingawa si mara zote na ndio maana
hulazimika kuishusha na iwapo itagoma kabisa huwa tunaiondoa kwa njia ya
upasuaji.
“Korodani isiyoshuka mara nyingi
huwa kuna uwezekano wa kugeuka kuwa saratani kuliko ile iliyoshuka, ikiwa
imebaki tumboni huwa tunajaribu kuishusha lakini ikishindikana tunaiondoa kwa
upasuaji,” anasema.
Anasema ile iliyogoma kushuka
hulazimika kuondolewa kwa njia ya upasujia haraka kwani ikiendelea kubakia huko
ndani husababisha matatizo makubwa kwa mwanaume husika.
“Ingawa na ile ambayo tunaweza
kufanikiwa kuishusha inaweza akupata saratani lakini ikiwa nje pale kwenye
mfuko wake huwa rahisi kuitibia na wakati mwingine kupona kabisa kuliko ikiwa
ndani ya mwili hapo huwa tunaiondoa kwa upasuaji,” anasema.
“Na ndio maana nahimiza watu
wawahi hospitalini hasa wale wenye watoto wa kiume wenye tatizo ili tuwasaidie
kuishusha kwa njia ya upasuaji iwe kwenye sehemu yake inayotakiwa ili hata
itakapotokea ikataka kugeuka kuwa saratani iwe rahisi kuitibu kwani inapona,”
anasema.
Kila kinachofanyika lazima kiandikwe
Anaongeza hata hivyo matibabu
hayo huwa yanafanyika kwa watoto waliotimiza umri wa miezi sita hadi mwaka
mmoja na nusu kwani kama alizaliwa zikiwa hazijashuka huweza kushuka katika
kipindi hicho.
“Wakiwahi mapema katika kipindi
hicho huwa wakati mwingine si lazima wafanyiwe upasujia badala yake huwa kuna
dawa tunawapatia za kihomoni ambazo huwasaidia kuzishusha,” anasema.
“Hata hivyo dawa hizo
zikishindwa kumsaidia kuzishusha ndipo huwa tunamfanyia upasuaji... huwa rahisi
kwa mtoto mdogo kuliko mtu mzima kwani viungo vyake vinakuwa vimekomaa.
“Lakini nawashauri wanaume wenye
umri mkubwa nao waende hospitali kuchunguza afya zao ili kama watakuwa na
tatizo waweze kusaidia kwa kuindoa korodani hiyo kabla haijaleta madhara ikiwa
huko ndani ya tumbo,” anatoa rai.
Mimi na matatizo ya korodani kuto kushuka sasa nifanyeje
JibuFutaPole rafiki, tunakushauri uende hospitalini ili kufanyiwa uchunguzi wa kina na wataalamu
FutaChapisha Maoni