Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement
NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM
MTIZAMO kwamba ulaji mayai ni hatari kwa afya ya binadamu umekuwako katika jamii nyingi duniani hasa ziishizo katika Bara la Afrika tangu enzi za kale.
Wengi huaminika ulaji wa mayai ni hatari kwa afya kwani huweza kumsababishia mlaji kuishia kupata magonjwa mbalimbali hasa ya moyo baadae katika maisha yake.
Lakini huenda matokeo ya utafiti uliofanyika nchini China hivi karibuni uliohusisha watu 500,000 yakabadili mtizamo huo walionao watu wengi.
Utafiti huo unaeleza, ulaji wa mayai una faida lukuki kwa afya ya mwili wa binadamu na husaidia kumkinga mtu dhidi ya magonjwa mengi ikiwamo hayo ya moyo, saratani na kiharusi.
Kwa mujibu wa watafiti waliofanya utafiti huo wanasema mayai yana virutubisho vingi muhimu ambavyo huhitajika katika mwili wa binadamu.
Wanasema mayai yana ‘utajiri’ mkubwa wa Vitamin A, B, B2, B5, B9, B12 na D pia yana kiwango cha juu cha protini na madini ya lutein na zeaxanthin.
Wanasisitiza kwamba ili mtu apate virutubisho vilivyopo kwenye mayai ili awe na lishe bora na yenye afya ni lazima ale mayai yaliyondaliwa katika namna inayofaa.
“Mtu anaweza kufikiria zaidi kuhusu tahadhari ambazo zimekuwa zikitolea na wataalamu wa lishe na kilichobainika kwamba ulaji wa angalau yai moja kwa siku hakuongezi hatari ya kupata magonjwa ya moyo badala yake kuna faida,” anasema Profesa Nita Forouhi wa Chuo Kikuu cha Cambridge.

Matokeo ya utafiti huo, yamechapishwa katika jarida la masuala ya moyo la Heart, ulifanywa baada ya miaka mingi ya watu kuonyesha dhidi ya ulaji mayai.
Mwaka 2007 wakfu wa Moyo Uingereza (BHF) uliondoa ushauri wake wa kuwataka watu wasile mayai zaidi ya matatu kwa wiki kutokana na kutokea kwa utafiti mpya kuhusu cholesterol.
Kwa mujibu wa ushauri wa Huduma ya Taifa ya Afya Uingereza (NHS), "ingawa mayai yana cholesterol, kiwango cha mafuta kutoka kwa mafuta na vyakula vingine tunavyovila huathiri zaidi kiwango cha chorestrol kwenye damu kuliko kinavyoathirika kutokana na ulaji wa mayai."
Kwa mujibu wa watafiti inaelezwa, kimsingi mayai si chanzo cha matatizo ya kuwepo na kiwango cha juu cha chorestrol kwenye damu bali yale mafuta tunayoyatumia.
Kwa mujibu wa Heart UK, yai la kawaida (58g; 2oz) huwa na mafuta 4.6g na ni robo pekee ya mafuta hayo huwa mafuta mabaya, yaani yale yanayoongeza kiwango cha chorestrol.
Wataalamu wa lishe
Daktari Frankie Phillips wa Chama cha Wataalamu wa Lishe Uingereza anasema “Yai moja au hata mawili kwa siku hutosha kwa mahitaji ya mwili na kwamba watu hawapaswi tena kuwa na wasiwasi juu ya ulaji mayai.
Dkt Phillips anasema onyo pekee watu wanafaa kuzingatia ni kwamba kula chakula cha aina moja pekee kwa wingi kutapelekea miili yao kukosa  madini na virutubisho vingine ambavyo hupatikana kutoka kwenye vyakula hivyo vingine mbali na mayai.
“Kwa sababu ingawa mayai yana protini, lakini mwili hupata pia protini kutoka katika vyakula vingine, jambo la kuzingatia pia ni kwamba ulaji wa vyakula vyenye protini kupindukia vinaweza kupelekea ‘kuwa mzigo kwa figo’.
Kwa kuangazia jinsi tunavyopika mayai, mayai ya kuchemshwa ndiyo bora zaidi.
Wataalamu wengi wa lishe hupinga kukaangwa kwa mayai kwa sababu mara nyingi mafuta hutumiwa na hivyo kiwango cha cholesterol anachokula mtu huongezeka.
Wanasema mayai mabichi au yalivyopikwa kidogo tu pia ni sawa, mradi tu yawe yalitokana kwenye mazingira safi.
Wanasema mayai yaliyopikwa ndiyo njia bora zaidi ya kujikinga na maambukizi na kwamba si vema kununua mayai ambayo yamevunjika kwani yanaweza kuwa yameingiwa uchafu au bakteria.
“Wengi bado wanakumbuka jinsi ya kutumia maji kwenye bakuli kubaini iwapo yai limeharibika au la.
Iwapo litazama, ni bora na lisipozama limeharibika,” wanabainisha.
Wanasema mayai mengi huwa katika kiwango kizuri kwa siku 28 tangu yanapotagwa.
Daktari
Pedro Pallangyo ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) anasema mayai pia yana madini ya zinc, selenium, iodine na phosphorus.
Anasema vitamin hizo huwa na kazi tofauti tofauti katika mwili wa binadamu ambapo vitamin A husaidia mwili wake huhusika kwa upande wa macho kumuwezesha kuona.
“Vitamin D yenyewe huhusika kwenye mifupa, B zina kazi nyingi kwenye vimenyeng’aji mbalimbali ndani ya mwili.
“Mtu akila yai moja maana yake anapata mjumuisho wote wa vitamin na madini muhimu yanayohitajika mwilini,” anasema.
Anasema ule weupe wa yai umerutubishwa kwa kiwango cha juu na protin na kile kiini chake kina mafuta hali inayowafanya wengi kuamini yana cholesterol nyingi.
Anasema kitaalamu mayai yanahusishwa na kuufanya mwili kuwa na afya njema pia huusaidia kujikinga dhidi ya magonjwa mbalimbali.
Kinga saratani ya kizazi
Anasema upo utafiti uliowahi kufanyika nchini Marekani ambao ulionesha mayai yana uwezo mkubwa wa kuwakinga wanawake dhidi ya saratani ya kizazi.
“Utafiti huo ulionesha wanawake wanaokula mayai sita kwa wastani kila wiki, walikuwa na uwezekano mdogo wa kupata saratani ya kizazi kwa kiwango cha asilimia 40 kushuka chini ikilinganishwa na wale wasiokula,” anasema.
Kiharusi
Anasema ulaji wa mayai mara kwa mara husaidia kumkinga mtu dhidi ya kiharusi.
“Kiharusi kimegawanyika katika aina mbili, kuna kile ambacho husababisha kuvilia kwa damu kwenye ubongo, na kile ambacho damu huwa haivilii kwenye ubongo.
“Utafiti ule ulionesha kwa asilimia 26 mayai humsaidia mtu kumkinga dhidi ya kiharusi cha kuvilia damu kwenye ubongo,” anasema.
Moyo na mfumo wa fahamu
Anaongeza “Upo utafiti pia uliowahi kufanyika na 1kuonesha mayai humkinga kwa asilimia 18 muhusika dhidi ya magonjwa ya moyo kuliko wale wasiokula.

Anasema mayai yana madini mengine muhimu ambayo husaidia kuilinda mifupa ya binadamu na kulinda ule mfumo wa fahamu.
“Hasa kipindi ambacho mtu anafikia uzee, mara nyingi hupata ugonjwa wa kutetemeka mwili na kusahau, wale wanaokula mayai mara kwa mara huwa na afya njema na nzuri ya ubongo kuliko wale wasiokula,” anasema.
Afya ya kucha, nywele
Daktari huyo ambaye pia ni mbobezi katika kufanya tafiti mbalimbali anasema ulaji wa mayai pia unahusishwa na kusaidia kuimarisha afya ya nywele na kucha.
“Tafiti zimewahi kuonesha watu wanaokula mayai mara kwa mara wanakuwa na uwezekano mdogo wa kupoteza (kunyonyoka) nywele zao pamoja na kucha wakifikia umri wa utu uzima,” anasema.
Anasema kwa watu wanaougua saratani mara nyingi hupoteza nywele zao hasa wale wanaopata tiba ya mionzi, ikiwa watakula mayai mara kwa mara watapokea ile protin ambayo huhipoteza kutokana na ugonjwa huo.
Unavyopaswa kuyaandaa 
Dk. Pallangyo anasema pamoja na kwamba mayai yana virutubisho hivyo muhimu hata hivyo suala la uandaaji wake ni jambo la kuzingatiwa ili mtu aweze kuvipata vyote.
Anasema kitendo cha kutumia moto mkali au kupika yai kwa muda mrefu kunaua ile protin iliyopo na hivyo kulifanya lisiwe na faida kwa mwili.
Anasema yai likipikwa mno jikoni husababisha kupoteza vile virutubisho vyote muhimu na kulifanya lisiwe na ‘thamani’.
“Kimsingi ikiwa mtu anataka kupata vile virutubisho vyote muhimu ni vizuri akila yai likiwa bichi kabisa, pale vinakuwa havijabadilishwa, lakini likiwekwa jikoni huvipoteza kadiri linavyokuwa linazidi kupikwa,” anasema.
Anafafanua “Yaani yai ambalo linakuwa halijapikwa muda mrefu jikoni ndilo linakuwa limebaki na vile virutubisho kuliko lile lililopikwa kwa muda mrefu.
Anasema tafiti zinaonesha kula wastani wa mayai matano hadi sita kwa wiki moja ni vema, au kula mawili hadi matatu inawezxa kukufanya ukapata kiwango kikubwa cha colestro.
Anasema yai halina madhara lakini madhara hutokea pale linapoandaliwa isivyofaa hasa ule ukaangaji, aidha yai bora zaidi ni lile lililochemshwa kuliko lile lililokaangwa.
“Ikiwa litakaangwa linapaswa kukaangwa na mafuta ya mimea tena ya alzeti na yawekwe kwa kiwango kidogo kwani ya kwake yanajitosheleza na si kukaanga kwa kutumia mafuta ya wanyama,” anasema.
Makala haya kwa mara ya kwanza yametoka leo katika gazeti la MTANZANIA ambalo nalitumikia

1 Maoni

  1. Yapi mayai mazuri kwa lishe ya kienyeji au haya mengineyo?

    JibuFuta

Chapisha Maoni

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement