Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement

Mwanasayansi wa maabara wa histopathologia BMH, Elisha Mgoji, akiwa katika 'Tissue Machine', hii ni miongoni mwa vifaa tiba vilivyomo ndani ya maabara hiyo ya kisasa (Picha kwa hisani ya BMH).

Na Veronica Mrema – Aliyekuwa Dodoma

Wataalamu wa Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) sasa wanao uwezo wa kuchunguza saratani kwa wagonjwa wanaowapokea kwenye kliniki zao kwa kuchukua sampuli za seli (tishu) kwa kutumia sindano, pasipo kulazimika kuwafanyia upasuaji wowote.

Yalibainishwa hayo hivi karibuni na Afisa Mteknolojia Maabara wa BMH (Histotechnologist), Michael Mazoya, katika mahojiano maalum na MATUKIO NA MAISHA BLOG kuhusu  idara hiyo muhimu katika masuala ya tiba ya magonjwa ya saratani namna inavyotoa huduma.

Mazoya alisema BMH imekuwa ikiimarisha huduma za uchunguzi wa magonjwa ya saratani na kwamba tayari wagonjwa wapatao 46 wamenufaika na huduma hiyo.

"Endapo huduma hizi zisingepatikana hapa BMH wagonjwa wote wangelazimika kusubiri majibu yatoke Dar es Salaam. sampuli nyingi za wagonjwa wa saratani tunazopokea ni za  mkoa wa Dodoma," alisema.

Mteknolojia Maabara huyo wa BMH alisema vile vile walipata sampuli kutoka mikoa mingine ukiwamo Tabora, Singida, Iringa, Mara, Morogoro na Manyara," alisema.

“Kuna uwekezaji mkubwa umefanywa na Serikali hapa BMH katika maabara ya pathlogy, tunao uwezo wa kubaini vimelea vya saratani kwa kutumia seli (tishu) za mwili wa binadamu.

“Tuna kliniki hapa BMH siku za jumatano na jumamosi, ambapo tunatumia sindano kupata sampuli kutoka kwenye kivimbe, hatufanyi upasuaji,” alisema.

Alifafanua “Tukishamchunguza mgonjwa na kukuta kuna uvimbe sehemu fulani, badala ya kukata, tunatumia sindano kwa kuchoma pale pale na kuchukua sampuli kwenda nazo maabara kwa uchunguzi.

“Huwa tunachukua seli moja kwa moja, katika kuchukua seli zile kuna wagonjwa wanaokuja vimbe zimejaa usaha, wengine zimejaa maji na wapo ambao ndani ya vimbe kuna seli tu ambazo zinakuwa kama nyama.

“Tunaingiza sindano, tunatoa kile tunachokipata ndicho tunakwenda kukifanyia uchunguzi na kubaini kile kinachomsumbua mgonjwa ni nini, uvimbe umetokana na nini? 

“Maana zipo vimbe nyingine ambazo zinatokea lakini si saratani, unakuta ni bakteria tu wameshambulia eneo husika na mara nyingi huwa ni zile ambazo tunakuta kuna usaha tu,” alibainisha.

Alisema kwenye maabara hiyo wana huduma tofauti tofauti, ikiwa ni pamoja na hiyo.

"Pia tunao uwezo wa kuchunguza  saratani kwa kutumia choo ndogo (mkojo), kwa kutumia makohozi na kutumia kwa majimaji yote yanayopatikana kwenye mwili wa binadamu.

“Kuna majimaji yanayopatikana kwenye uti wa mgongo, tumboni, moyo, mapafu na kwengineko, tunapima,” alisisitiza.

Alisema pia wanafanya uchunguzi wa awali wa magonjwa ya saratani kwa mfano za matiti, shingo ya kizazi na tezidume kwenye idara hiyo.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement