Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement

Na WAMJW- Dom.

Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imesikitishwa na kitendo askari wa ulinzi (SUMA - JKT) kumpiga ndugu wa mgonjwa aliefika kumjulia hali mama yake katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga. 

Hayo yamesemwa leo na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi (pichani) pindi akiongea na Maafisa habari wa Wizara ya Afya katika Ofisi za Wizara hiyo katika jengo la Bima ya Afya Jijini Dodoma. 

"Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imesikitishwa na inalaani sana kitendo hicho kilichofanywa na mlinzi wa SUMA - JKT" amesema Prof. Makubi. 

Akielezea juu ya tukio hilo Prof. Makubi amesema kuwa, Mnamo Januari 22, 2021 Ijumaa jioni askari wa kujenga taifa (SUMA-JKT) alionekana akimpiga ndugu wa mgonjwa katika maeneo ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga jambo ambalo ni kinyume na maadili na taratibu za kazi.

Aidha, Prof. Makubi amesema kuwa, Wizara kwa kushirikiana na ofisi ya mkuu wa Mkoa wa Shinyanga kupitia Mkuu wa Wilaya imeelekeza mlinzi huyo atolewe kwenye kituo hicho cha kazi na kurudishwa makao makuu ya kanda ya jeshi hilo kwaajili ya hatua za kinidhamu kulingana na taratibu za jeshi hilo. 

Hata hivyo, Prof. Makubi ameeleza kuwa, Katibu Mkuu (Afya) Prof. Mabula Mchembe ameelekeza kupata maelezo kutoka kwa uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga wa jinsi tukio hilo lilivotokea, mazingira yake na hatua zilizochukuliwa na uongozi wa Hospitali hiyo. 

Pia, ufanyike uchaguzi kama kulikuwa na uzembe wa utekelezaji wa mfumo na mwongozo wa utoaji huduma kwa mteja (customer care)ambao ulitolewa na Wizara kwa vituo vyote vya kutolea huduma za Afya ili kuona kama kulikuwa na udhaifu mpaka tukio hili kutozuilika, huku akisisitiza baada ya uchunguzi huo hatua stahiki zitachukuliwa. 

Mbali na hayo, Prof. Makubi ametoa rai kwa wananchi kuwa watulivu wakati hatua zikiendelea kuchukuliwa, huku akiwaasa wananchi kuendelea kupata huduma za Afya bila wasiwasi kwani Serikali imejipanga kuhakikisha suala hili halijirudii tena.

"Rai ya Wizara, tunaomba wananchi wawe watulivu wakati suala hili linafanyiwa kazi, na Jamii iendelee kupata huduma katika vituo vyote vya kutolea huduma za Afya nchini bila wasiwasi wowote, kwani Serikali imejipanga kuhakikisha suala hili halijirudii," amesema Prof. Makubi. 

Wakati huo huo, Prof. Makubi ametoa wito kwa wananchi kufuata na kuzingatia taratibu zilizowekwa za muda wa kuingia na kuona wagonjwa katika vituo vyote vya kutolea huduma za Afya nchini. 

Pamoja na hilo, Prof. Makubi amewataka wananchi kutumia vizuri mifumo ya Mawasiliano ambayo imewekwa sehemu mbali mbali ikiwa ni pamoja na kupiga namba 199 bila malipo na za viongozi ili kuwasilisha malalamiko ili kufikia maamuzi sahihi ya migogoro. 

Pia, amewataka Viongozi na Watumishi wote kuendelea kusimamia vizuri huduma bora za afya kwa wananchi wanaowahudumia, kisha kuwakumbusha kusimamia vizuri miongozo ya huduma kwa wateja ambayo ilishatolewa na Wizara. 

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement