Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement

Wasichana hao wakiwa na baba yao, Prof. Makani na mwandishi wa makala haya hivi karibuni.

Na Veronica Mrema – Dar es Salaam 

Mazingira waliyoishi wakishuhudia na kusikia mazungumzo mengi kwenye jamii kuhusu ugonjwa (wagonjwa) wa siko seli na imani potofu walizonazo wanajamii, ni suala ‘lililowasukuma’, kuamua kujikita zaidi katika kuufahamu ugonjwa huo kwa undani wake.

Wasichana watatu waliokulia maeneo tofauti tofauti, kabla ya kukutana pamoja darasani, Shule ya Sekondari Zanaki, jijini hapa, Valentina Rwegasira (18), Zuwena Ismail (18) na Zainab Mohamed (19) sasa wametia nia ya kuwa madaktari bingwa wa magonjwa ya damu hususan upande wa siko seli.

Hivi karibuni MATUKIO NA MAISHA BLOG ilifanya mahojiano maalum na wasichana hao ambao walikuwa miongoni mwa washiriki wa kongamano la kisayansi lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), ambapo wataalamu walijadili maendeleo ya Mpango wa Taifa wa Damu Salama (NBTS) na changamoto za magonjwa ya damu Tanzania.

WOTE NI ‘VIPANGA’

Ni wasichana walio tayari kuhakikisha wanapambania ndoto yao hiyo, wakijidhatiti vema katika upande wa masomo yao tangu wakiwa kidato cha pili na hadi katika matokeo yao ya mtihani wa ‘Mock’ wa kidato cha nne mwaka 2020, matokeo yao yanadhihirisha hilo.

Katika mahojiano na mwandishi wa Makala haya wanabainisha kwamba wote watatu wamefanya vema kidato cha pili kwa kupata daraja la kwanza, vivyo hivyo kwa upande wa kidato cha nne katika matokeo ya Mock’

“Matokeo ya kidato cha pili, nilipata I:7 na matokeo ya kidato cha nne ya mtihani wa mock nilipata I: 9,” anabainisha Valentina.

Zuwena anasema kwa upande wake kidato cha pili alipata I:10 na kidato cha nne katika mtihani wa ‘Mock’ alipata I:13.

Zainab naye anabainisha kidato cha pili alipata I:9 na katika ‘Mock’ kidato cha nne alipata I:13.

“Tukiwa kidato cha pili, mwalimu wetu wa taaluma aliagiza kila mtu afikirie ‘project’ ya kufanya ikiwa ni sehemu ya masomo na mafunzo darasani.

“Hapo ndipo tulipojikuta tuna wazo linalofanana na kuamua kuungana ili tutekeleze ‘project’ hiyo tuliyokuwa tumekusudia ,” anasema Valentina.

WAZO LILIANZIA MBALI

“Tulijikuta wote watatu tukifikiria kuhusu kufanya ‘project’ kwa upande wa ugonjwa wa siko seli, mwalimu akatuambia tulifanye kwa pamoja,” anabainisha Zainab.

Valentine anaongeza “Binafsi nimekuwa nikitamani kujua ugonjwa huu kwa undani miaka mingi, mara kadhaa nikiwa na umri mdogo (nikiwa najitambua), nimekuwa nikiambatana na baba yangu mzazi ambaye ni mtaalamu wa maabara kwenda naye kazini kwake.

“Huko nimekuwa nikishuhudia jinsi anavyosaidia wagonjwa ambao baadae alikuja kunieleza wanakabiliwa na ugonjwa wa siko seli, alikuwa akichukua sampuli za vipimo na kwenda kuzichunguza maabara.

“Nimekuwa pia nikishuhudia jinsi wagonjwa hao wanavyopatiwa matibabu kule hospitalini, hata hivyo bado kuna imani potofu nyingi juu ya ugonjwa huu, hicho ndicho kilinisukuma zaidi kujifunza ili siku moja na mimi niweze kuja kusaidia jamii yangu,” anasema.

ALITOA KIZAZI

Zuwena anasimulia kwamba kwa upande wake alijikuta akitamani kusoma udaktari wa magonjwa ya siko seli ili kusaidia jamii kutokana na kisa alichowahi kushuhudia kwenye mtaa anakoishi jijini hapa juu ya jirani yao mmoja.

“Kuna mama mmoja alikuwa akiugua siko seli, alitoa kizazi kwa sababu iliaminika kwamba ndicho kimemsababishia tatizo, hivyo hakuwahi kuwa na watoto, nilimuuliza mama yangu iwapo anafahamu alipohamia mwanamke huyo lakini hakuna anayejua aliko hivi sasa,” anasema.

Anaongeza “Hata hivyo, nilipokuja kufanya hii ‘project’ ya kidato cha pili nikajifunza mengi kwamba kuwa na siko seli haina maana kwamba mtu hastahili kuzaa tena, nimejifunza kuna imani potofu nyingi juu ya ugonjwa huu, nikaamua kujikita zaidi kwenye masomo ya sayansi.

“Nimeamua kusoma udaktari Mwenyezi Mungu atakaponijalia kufika huko elimu ya juu, siku moja nitaisaidia jamii yangu kuelewa kuhusu ugonjwa huo n ahata kuepusha changamoto kama hizo zinazoweza kujitokeza kutokana na kukosa ufahamu,” anasema.

Zainab anasema yeye aliwahi kuwa na jamaa yake ambaye alikuwa akikabiliwa na ugonjwa huo, alishuhudia namna anavyoteseka kujitibia, wakati mwingine akitengwa, sasa ana imani atakapojifunza zaidi ataweza kusaidia wengi.

PROF. MAKANI 'AWATABIRIA' 

Profesa Julie Makani (mwenye suti nyekundu pichani) ni miongoni mwa Madaktari na Watafiti waliojikita kwa zaidi ya miaka 20 kufanya tafiti juu ya magonjwa ya damu hasa kwa upande wa siko seli nchini, anasema amevutiwa na wito walionao wasichana hao.

“Wapo wengine ambao nawafahamu wenye nia ndani ya mioyo yao ya kuja kuwa wabobezi upande wa sikoseli, ni jambo la kuwatia moyo kwamba wanaweza kufikia ndoto hiyo, ni miongoni mwa wasichana wachache walioamua kujitoa kimasomaso,” anasema.

Anapngeza “Valentina baba yake nafanya naye kazi upande wa maabara, aliponishirikisha kuhusu ‘project’ waliyokuwa wameichagua, nilimwambia waje, walikuja.

“Wana nia ya dhati ya kujifunza, nilivutiwa zaidi namna walivyofanya vema kwenye matokeo yao ya kidato cha pili na yeye (Valentina) alifanya vizuri kiasi cha kupewa zawadi shuleni kwao.

“Matokeo yao ya kidato cha nne katika mtihani wa ‘Mock’ nayo ni mazuri, ‘nawatia moyo’ wasichana wengine kwamba wasikimbie sayansi, wasikimbie hesabu, inawezekana kabisa kuwa wataalamu wabobezi, wakiweka nia watafika mbali, watafikia ndoto zao,” anasema.

Prof. Makani anasema nafasi ya mzazi (wazazi) nayo ni muhimu katika kuhakikisha mtoto (watoto) wanafikia ndoto zao na malengo yao waliyojiwekea, wasiwaache, wawasaidie.

MWANZO WA HATUA

Wasichana hao wanasema Prof. Makani amekuwa nao karibu akiwasisitiza kutokukata tamaa kufikia malengo yao siku moja kwenye maisha yao watakapojaliwa na Mwenyezi Mungu.

“Walimu wetu hatuwezi kuwasahau katika hili, wamekuwa karibu nasi pia, wakituhasa kuzingatia masomo na kutokuta tamaa, tusonge mbele ipo siku tutafika,” anasema Zuwena.

Zainab anasema kongamano walilohudhuria ni la kwanza tangu walipoweka malengo hayo na kwamba wamejifunza mambo mengi na kuongeza maarifa katika kile wanachotamani kuwa.

Valentine anaongeza “Wazazi ‘wanawape moyo’ watoto wao waweze kusoma sayansi na watoto nao ‘watie imani’ kusoma sayansi kwa bidii, wasifikiri ni ngumu, ni nyepesi kama ‘wakiwa na moyo’ wa kujifunza.

“Pale Zanaki vifaa vipo kila kitu kwa ajili ya kujifunza lakini pia mwanafunzi lazima afanye kwa vitendo si tu kwa kutegemea shule, lazima utafute na sehemu nyingine ili kupata ujuzi zaidi,” anasema.

‘NILIPANDA MBEGU NJEMA’

Gracian Rwegasira (pichani akiwa na wasichana hao) ambaye ni baba mzazi wa Valentina ambaye ni mtaalamu wa maabara ya pathologia na Idara ya vimelea vya malaria Muhimbili, anasema anajisikia fahari juu ya wasichana hao akiwamo mwanawe.

“Nafanya kazi idara ya pathology na idara ya vimelea vya malaria pamoja na Prof. Makani, pia ninawahudumia wagonjwa wa siko seli kwa upande wa vipimo ili wapate tiba sahihi na kwa ufasaha zaidi,” anasema.

Anaongeza “Mwanangu amekuwa akiona jinsi ambavyo huwa nafanya, nilikuwa nakuja naye tangu alipokuwa mdogo, aliona jinsi nilivyokuwa natoa huduma, wakati ule alikuwa anashangaa wale wanaugua nini!?.

“Nikiwa ‘on-call’ nilikuwa nakaa naye ofisini wakati fulani, wakati mwingine anabaki na wenzangu ofisini mimi naenda maabara, hivyo amekua katika mazingira hayo, hata alipokuwa likizo nilikuwa naambatana naye ofisini.

“Akiwa darasa la tano, kila alipokwenda shule alikuwa akikua na kujiuliza hawa ni wagonjwa wa aina gani, kadri alivyokua nilianza kumueleza kuhusu magonjwa ya damu na wagonjwa aliokuwa akiona nawahudumia walikuwa wakikabiliwa na ugonjwa gani?

“Nyumbani pia alikuwa akiniuliza maswali mengi, nilikuwa namuelewesha nini kinatokea hadi mtoto kuwa na siko seli na matibabu gani anapewa.

“Kwenye jamii wakati mwingine nilikuwa ‘nawa – identify’ wagonjwa kwa kuwaangalia wengi nawaleta kliniki, wapo ambao mtaani walidai ni ndondocha (wagonjwa wa akili).

“Nililazimika na nazimika kuwafuata na kuwaelewesha wazazi na kuwasihi kuwaleta watoto wao kliniki kwa uchunguzi, wapo ambao huwaleta na hatimaye wale wanaokutwa na siko seli wanaanzishiwa matibabu mara moja.

Anaongeza “Tunawasaidia wazazi kuelewa ugonjwa huu na jinsi gani ya kuishi na watoto wao, watoto pia wanakua wakijitambua hali zao.

Rwegasira anashauri wazazi wawe chachu ya ‘kuwapa moyo’ watoto wao na kuwasaidia kujijenga kufikia malengo yao maishani.

“Binafsi kama mzazi nilikuwa natamani siku moja aje arithi kazi yangu ninayoifanya, nimekuwa napenda mtoto wangu ajue sayansi, mimi imeniwezesha kuishi maisha haya na kusaidia jamii yangu.

“Sasa najisikia furaha kwamba mwanangu anakwenda kuwa kile nilichotamani awe, atafuata nyayo zangu, ni wito alionao kutoka ndani ya moyo wake, nafarijika mno,” anasema.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement