Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement


 Na Veronica Mrema 

Licha ya 'wimbi' la pili la maambukizi ya Virusi vya CORONA vinavyosababisha ugonjwa wa homa kali ya mapafu (COVID – 19), Rais Dk. John Magufuli, amesisitiza kwamba Tanzania haitajifungia ndani kama ambavyo nchi nyingine zimefanya.

Rais Magufuli (anayemwagilia maji, mti pichani) ametoa kauli hiyo leo Januari 27, 2021 Mkoani Geita, alipokuwa akizindua Shamba la Miti la Chato, ikiwa ni siku tisa tangu Januari 18, 2021 Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto iliposambaza kwa vyombo vya habari mwongozo wa uchukuaji sampuli za vipimo vya COVID – 19 katika Hospitali na Vituo Maalum.

Rais. Magufuli akizungumza amenukuliwa “Mtatishwa sana ndugu zangu Watanzania lakini simameni imara, ninajua wapo baadhi ya watanzania wameondoka ndani ya nchi na kukimbilia maeneo mengine, wamechanjwa na walipochanjwa, wamekuja huku wametuletea CORONA ambayo ni ya ajabu ajabu, simameni imara,” amebainisha Rais. Magufuli.

“Katika kipindi hiki ambako kuna magonjwa yanayojitokeza yasiyojulikana kama CORONA, nchi nyingi wananchi wake watakuwa wamejifungia ndani.

“Sisi Tanzania hatujajifungia na hatutegemei kujifungia ndani na wala sitegemei hata siku moja kutangaza kwamba tunajifungia ndani kwa sababu Mungu wetu yupo hai na ataendelea kutulinda Watanzania,” amesisitiza.

Ameongeza “Tutaendelea kuchukua tahadhari zingine za kiafya ikiwa pamoja na kujifukizia, unajifukizia huku unamuomba Mungu, unasali, unaswali huku ukiendelea na zoezi jingine la kulima mahindi, viazi ili ule vizuri ushibe CORONA ashindwe kuingia kwenye mwili wako.

Rais Magufuli amesema “Chanjo hazifai kama wazungu wangekuwa na uwezo wa kuleta chanjo hata chanjo ya ukimwi ingekuwa imeshaletwa, ya kifua kikuu kingekuwa kimeondoka, chanjo ya malaria ingekuwa imeshapatikana hata ya kansa ingekuwa imeshapatikana .

“Lazima watanzania muwe wa angalifu kwa mambo ya kuletewa letewa, msije mkafikiria mnapendwa sana, Taifa hili ni tajiri, Afrika ni tajiri kila mmoja anaitamani, tuwe waangalifu.

“Niiombe wizara ya afya isiwe inakimbilia mambo ya ma-chanjo-chanjo bila yenyewe kujiridhisha, ipo nchi fulani  walichanjwa watoto wake wa kike wenye umri wa miaka 14 wanaambiwa kwa ajili ya kuzuia kansa ya kizazi,

“Imekuja kugundulika ile chanjo ilikuwa ni ya kuzuia wasizae, kwa hiyo niiombe sana wizara ya afya, si kila chanjo ni ya maana sana kwa taifa letu, siyo kila chanjo ina faida kwetu.

“Ni lazima watanzania tuwe macho, ni lazima watanzania tuwe waangalifu, tutafanyiziwa majaribio ya ajabu ambayo yataleta madhara makubwa,” amesisitiza.

Katika mwongozo uliotolewa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, toleo la kwanza la tarehe 14, 2021 ilianisha hatua 10 zinazozingatiwa, ya kwanza ikiwa ni ya msingi ya ufuatiliaji wa mwenendo wa ugonjwa huo duniani.

Hatua ya pili iliyoainishwa ni wale wanaostahili kuchukuliwa sampuli, tatu ni mapokezi ya wateja, hatua ya nne ya kuzingatiwa ni chumba cha kuchukulia sampuli na hatua ya tano iliyosisitizwa ni uchukuaji, utunzaji na usafirishaji wa sampuli hizo.

Kwa mujibu wa mwongozo huo, hatua ya sita ni malipo ya vipimo, hatua ya saba muda wa kuchukua sampuli, hatua ya nane uhakiki wa sampuli, hatua ya tisa majibu ya vipimo na hatua ya 10 ni uhakiki wa majibu au vipimo hivyo.

Habari hiyo kwa undani inapatikana kupitia link…. https://matukionamaisha.blogspot.com/2021/01/hatua-10-muhimu-upimaji-wa-corona.html

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement