Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement

Mchunguzi wa Maabara ya TMDA - Kanda ya Ziwa, Maximilian Rwezaula akifafanua jambo kwa waandishi wa habari namna mashine ya  MP – AES (Atomic Plasma Atomic Emition) inavyofanya kazi ya kuchunguza madini tembo (heavy metals).

Na Veronica Mrema - Mwanza 

‘Milango’ ipo wazi katika Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA), Kanda ya Ziwa, kwa wadau mbalimbali wa masuala ya tafiti za madini tembo, kushirikiana na mamlaka hiyo lengo ikiwa kuendelea kulinda afya ya jamii. 

Mamlaka hiyo ‘imepanua wigo’ wa ushirikiano na wadau wa tafiti za madini tembo ndani na nje ya nchi, ikisisitiza kwamba inayo mtambo wa kisasa yenye uwezo mkubwa wa kuchunguza madini hayo kwenye sampuli mbalimbali.

Kaimu Mkurugenzi wa Maabara wa Kanda hiyo, Bugusu Nyamweri amesema hayo alipozungumza na waandishi wa habari katika mahojiano maalum.

Nyamweri amebainisha katika mfumo wa tiba kuna kiwango ambacho mwili wa binadamu unatakiwa kuwa na madini tembo na kila mmoja anacho, lakini ni kile ambacho mwili unaweza kuhimili na kwamba kiwango hicho kinapozidi huleta athari.

“Binadamu wote tuna madini tembo kiasi fulani, kwa mfano  dhahabu wote tunayo mwilini lakini ni kwa kile kiwango ambacho unahimili, kiwango cha madini hayo kikizidi mwili unapata athari mbalimbali,” amesema.

Ameongeza “Huweza kuathiri moyo, figo, mfumo wa fahamu, baadae unakuta anakuwa msahaulifu, unamwambia hiki baada ya dakika mbili kasahau, mengine yanaathiri mfumo wa ngozi kwa mfano vipodozi.

“Hivyo lengo letu (TMDA – Kanda ya Ziwa) ni kuongeza wigo katika masuala ya uchunguzi na tafiti, vifaa vipo, tunatoa wito kama kuna taasisi itahitaji kufanya tafiti eneo hilo tupo tayari,” amesisitiza.

Nyamweri ameongeza “Kwa sababu maabara hii kama sehemu ya Mamlaka, katika eneo ambalo tunaona linahitaji kuongeza wigo ni kwenye tafiti.

“Kwa mfano, ukweli kabisa Kanda ya Ziwa kunaonekana kuna kesi nyingi za saratani tunajua kule kwenye maeneo ya wachimbaji wadogo wanatumia ‘mercury’ na wakati mwingine wanashika kwa mikono, tunahitaji kushirikiana na wadau wanaofanya tafiti, walete sampuli hizo tuzichunguze,” amesema.

Meneja wa Mawasiliano na Elimu kwa Umma wa TMDA, Gaudensia Simwanza amesema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Prof. Mabula Mchembe, aliyoyatoa hivi karibuni kwa mamlaka hiyo baada ya kuitembelea maabara hiyo.

“Katibu Mkuu akitembelea maabara hii Septemba, 2020 alielekeza tushirikiane na wadau mbalimbali katika eneo hili (la uchunguzi wa madini tembo), wadau walete sampuli zao tupime, majibu yapatine mwisho wa siku tulinde afya ya jamii,” amebainisha.

Ameongeza “Tumeanza utekelezaji, tunaalika taasisi zinazofanya tafiti walete sampuli zao, mashine tunayo imenunuliwa na Serikali kwa takribani Sh. bilioni moja na wataalamu tunao, wadau waje tushirikiane.

Mchunguzi wa Maabara ya TMDA - Kanda ya Ziwa, Maximilian Rwezaula (pichani) amefafanua kwamba mashine hiyo ya MP – AES (Atomic Plasma Atomic Emition Stectroscopy) ina uwezo wa kuchunguza aina nyingi za madini tembo kwenye sampuli moja kwa wakati mmoja tofauti na mashine nyingine ambayo walikuwa nayo na kwa Tanzania ndiyo mashine pekee iliyopo.

Amesema faida nyingine ya mashine hiyo ni kwamba inatumia gesi ya Naitrojeni ambayo inakusanywa kutoka kwenye mazingira tofauti na nyingine ambazo zinatumia 'petrolium gas' kama zile zinazotumika majumbani.

"Ukiwasha mashine unalazimika usiondoke kwa zile zinazotumia 'petrolium gas' lakini kwa hii naweka sampuli, na - set muda wa uchunguzi na wakati huo huo naweza kuendelea na shughuli zingine ninazohitajika kuzifanya ndani ya maabara.

"Tunaweza kupima madini tembo kwenye maji, chakula, vipodozi na wanafunzi wanaweza kuja hapa kujifunza na kwa vyuo ambavyo wanafunzi wanahitaji kufanya tafiti wanaweza kuja hapa kufanya," amesema. 

“Yaani kwa mfano naweza kuchunguza madini tembo aina ya copper, lead na mercury kwenye sampuli moja kwa wakati mmoja, tofauti na mashine nyingine ningelazimika kupima (kuchunguza) aina moja moja,” amebainisha.

Mchunguzi wa Maabara ya TMDA - Kanda ya Ziwa, Maximilian Rwezaula (pichani) akionesha namna wanavyochukua sampuli ili kuifanyia uchunguzi kwa kutumia mashine hiyo.

Picha zote na Veronica Mrema

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement