Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement


Na Veronica Mrema – Dar es Salaam

Kila dozi ya dawa inapaswa kutumika kwa mgonjwa mmoja kulingana na ugonjwa aliokutwa nao, hata ikiwa ugonjwa wa aina hiyo hiyo utakutwa kwa mgonjwa mwengine baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kimaabara.

Wataalamu wanasisitiza kwamba ni kosa kwa mgonjwa kubakiza dawa, anapaswa kuzitumia hata ikiwa amejihisi kupata nafuu kwani kukatiza dozi huchangia mwili kujenga usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa.

Aidha, dawa hazipaswi kutumiwa kwa kupeana bila ushauri wa daktari kwani kwa kufanya hivyo ni kosa linalchangia pia kuongeza tatizo la usugu wa dawa na hata kusababisha madhara yatokanayo na dawa kwa muhusika.

Meneja Kitengo cha Udhibiti wa Majaribio ya Dawa na Ufuatiliaji wa Usalama na Ubora wa Dawa wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA), Kissa Mwamwita anasema, kipo kisa cha mwanamke mmoja ambaye alitumia dawa za mumewe na kupata madhara (majina yamehifadhiwa). 

“Wote waliugua, wakafanya uamuzi kuambata  pamoja hadi hospitalini kufanyiwa uchunguzi wa kimaabara, vipimo walivyofanyiwa vilibaini walikuwa wakiugua ugonjwa wa aina moja.

“Baada ya kupata majibu hayo, walionwa na daktari ambaye alimpatia kila mmoja dozi yake ya dawa ya kutumia kwa matibabu dhidi ya ugonjwa aliokutwa nao.

“Kila mmoja alizingatia maelekezo aliyopatiwa na daktari katika hatua za awali za kutumia dozi walizopewa,” anasema Kissa.

Anaongeza “Lakini, siku moja dawa za mwanamke ziliisha, ndipo aliamua kuchukua dawa za mumewe atumie, akiamini kwamba siku iliyofuata angekwenda hospitalini kuchukua zingine na kurejeshea,” anasema.

Anasema hilo lilikuwa kosa kubwa alilofanya kwa sababu kitaalamu dozi ya dawa za mgonjwa mmoja hazipaswi kutumiwa na mgonjwa mwingine kwa matibabu bali kila mmoja anapaswa kutumia dozi yake kama alivyoandikiwa na daktari.

Anasema mwanamke huyo alipotumia dawa za mumewe aliishia kupata madhara yatokanayo na dawa licha ya kwamba ni dawa zile zile ambazo mumewe alikuwa akizitumia pasipo madhara yoyote kumpata.

Anaongeza “Kesi ya mwanamke huyo ni miongoni mwa kesi zilizorekodiwa na mamlaka hiyo juu ya madhara yatokanayo na dawa.

“Dawa ya mtu mmoja haitakiwi kutumiwa na mtu mwingine hata kama unaumwa ugonjwa huo huo, huwezi kuchukua ya mtu mwingine kama karanga au nguo kwamba utaomba mwenzako akusaidie.

“Kimsingi, kila mtu anapaswa kutumia dozi aliyoandikiwa na daktari na lazima amalize, hutakiwi kubakiza hata ukijisikia nafuu.

“Ukiacha ndipo inasababisha usugu kwa sababu kwa mfano umetumia siku mbili badala ya tano, malizia dozi ili vile vijidudu viishe mwilini,” anasisitiza.

Meneja Kitengo cha Udhibiti wa Majaribio ya Dawa na Ufuatiliaji wa Usalama na Ubora wa Dawa wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA), Kissa Mwamwita akifafanua jambo katika mahojiano na mwandishi wa makala haya (hayupo pichani)

UHIFADHI MAJUMBANI

Dk. Alex Nkayamba ni mmoja wa Maofisa ndani ya Kitengo hicho cha Udhibiti wa Majaribio yna Usalama wa Dawa kilichopo TMDA, anasema kwa kawaida dawa zinapaswa kutumika na kuisha kwani zinapoachwa nyumbani utunzaji wake mara nyingi huwa ni tofauti na ule unaopaswa.

“Nyumbani ni tofauti na sehemu maalum za kutunzia dawa kama famasi au hospitali, dawa inapobakizwa na kuhifadhiwa nyumbani itaanza kuharibika na mtu anapokuja kuitumia tena huwa haina ule uwezo wa awali katika kukabili ugonjwa na hii huweza kuchangia usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa,” anasema.

Anaongeza “Kwa hiyo mtu anakuwa anatumia dawa aliyohifadhi nyumbani lakini pasipo kujua kwamba ipo katika kiwango cha chini, anapokuja kuitumia kwa mara nyingine inakuwa ufanisi wake umepungua matokeo yake usugu.

“Kitaalamu daktari akimpa mgonjwa dozi ya dawa fulani anafahamu kwamba baada ya kipindi kile alichomuandikia kutumia vile vijidudu vitakuwa vimekufa, lakini akitumia na kuacha pale anapohisi unafuu si kwamba wale wadudu wamekufa.

“Baada ya kipindi fulani muhusika ataanza kuugua tena upya na kwa sababu mdudu anakuwa amezoea ile dozi ya dawa aliyopewa awali inabidi, anaporudi hospitalini abadilishiwe dawa nyingine,” anasema.

ATHARI KIUCHUMI

Dk. Alex anasema hali hiyo ina athari mbalimbali za kiuchumi kuanzia ngazi ya familia na hata Taifa kwa ujumla.

“Kwa sababu dawa haikutumika ilivyopaswa, imesababisha usugu, inabidi kubadilisha dozi na kuchukua ya bei ya juu zaidi ili kupambana na ugonjwa ule ule, lakini inapofika mahala kama Taifa tunajikuta tunaagiza dawa ambazo hazitibu maana yake ni kwamba uchumi wa nchi nao unaathirika,” anasema.

Anatoa mfano kwamba zipo baadhi ya dawa ambazo zilionesha usugu katika kutibu magonjwa husika hali iliyolazimu Serikali kuchukua hatua ili kunusuru jamii.

“Kwa mfano dawa za SP ikiwamo Fansidar na Metakelfin vile vile kuna dawa ya Amodiaquine na Chloromphenicol Injection iliyokuwa ikitengenezwa na kiwanda cha Lincoline,” anabainisha.

MUHIMU KUZINGATIA

Kissa anaongeza “TMDA tunazisajili na kuhakiki ubora wake ndipo tunaziruhusu kuingia sokoni, lakini usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa husababishwa na mambo mengi ikiwamo tuliyoyabainisha.

 “Kimsingi, mtumiaji anavyopewa dawa akitumia tofauti hasa hizi za vijiua-sumu (antibiotics), kwa mfano, mgonjwa ameandikiwa vidonge viwili kila baada ya saa nane, akipunguza ina-maana kwamba vile  vijidudu havitaweza kuuliwa na ile nguvu ya dawa.

“Anavipa usugu, ikiwa pia ametumia ‘antibiotics’ ambazo hazijafikia viwango ‘substandard’ inaweza kusababisha usugu kwa sababu vile vijidudu haviwezi kufa kutokana na ile nguvu ya zile dawa.

“Kuna tabia pia ya kutumia dawa bila kufuata ushauri na maelekezo ya daktari, mtu ananunua dawa bila ushauri wa daktari, anatumia dawa ambayo haina uwezo wa kuua vile vijidudu,” anasema Kissa.

Anaongeza “Matumizi ya dawa lazima mtu aende hospitali, apimwe ili mtaalamu aweze kujua aina ya dawa anayopaswa kupatiwa kuitumia yenye uwezo wa kuua vile vijidudu, lakini watu wanajinunulia wenyewe, wanatumia kumbe dawa ile haina uwezo wa kutibu ule ugonjwa.

“Hivi vijidudu wakati mwingine huwa vinabadilika, unaweza kutumia dawa fulani ukijua miaka kadhaa iliyopita ulitumia ukapona, kumbe kijidudu cha sasa ni kikali kuliko kile cha awali kikasababisha usugu,” anasema.

TAFITI

Kissa anasema TMDA huwa inashirikiana na taaasisi mbalimbali nchini zinazofanya tafiti mbalimbali zinazolenga kuangazia uwezo wa dawa zenye usugu kwenye jamii, ikiwamo Taasisi ya NIMR.

“Tafiti zinafanyika kuangalia, je zinafaa kuendelea kutibu magonjwa yaliyokusudiwa au dawa zingine zitafutwe, zitumike kutibu hayo magonjwa ambayo awali yalitibu magonjwa fulani.

“Hivyo, zinatafutwa ambazo zina nguvu zaidi kutibu magonjwa ambayo yanaonekana hayatibu magonjwa yaliyokuwa yanatibu zamani,” anasema Kissa.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement