Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement


Na Veronica Mrema – Mwanza

Ikiwa una tabia ya kutumia dawa pasipo kuimaliza, ukibakisha na kuhifadhi nyumbani kwa lengo la kuitumia pale utakapojihisi u mgonjwa tena pasipo kwenda hospitalini kuonwa na daktari, ufanyiwe vipimo na kuandikiwa dawa nyingine, unapaswa kubadilika na kuachana nayo. 

Kwa sababu, kitaalamu kila dawa inapotengenezwa kuna kiambata hai kinachowekwa ndani yake ambacho kinakusudiwa kutibu ugonjwa husika ndani ya muda uliopangwa, unaoandikiwa na daktari.

Aidha, kila dawa ina muda wa kuisha kwa matumizi yake na muda huo unapofika tamati, wataalamu wanasema wastani wa asilimia 10 ya kiambata hai kilichomo ndani yake hubadilika, mabadiliko hayo huweza kusababisha athari kubwa kwa mtumiaji.

Katika mahojiano maalum na waandishi wa habari hivi karibuni, Kaimu Mkuu wa Maabara ya Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA), Bugusu Nyamweru  (Pichani) alisema hayo alipokuwa akifafanua jinsi wanavyochunguza myeyuko wa viambata hai vya dawa ili kufanikisha tiba.

Nyamweru alikuwa akifafanua kwa waandishi hao namna wanavyotumia mashine iliyoundwa mithili ya tumbo la binadamu inavyofanya kazi ya kuchunguza namna dawa inavyoachilia kiambata hai inapoingia ndani ya mwili wa binadamu ili kuifanikisha tiba iliyokusudiwa.

Alisisitiza dawa inapaswa kutumiwa kulingana na maelekezo ya wataalamu na kumalizwa ndani ya muda uliopangwa (usibakize dawa kwa ajili ya matumizi ya baadae).

“Kiambata hai kina muda wa ‘kuishi’ ndani ya dawa, ndiyo maana kuna ‘expire date’ (muda wa kuisha kwa matumizi), unapoisha wastani wa asilimia 10 ya kiambata hai hupungua na kubaki asilimia 90.

“Ile asilimia 90 inakuwa na uwezo wa kutibu lakini tunakuwa hatujui mule ndani ile asilimia 10 ambayo imepungua imebadilika kuwa nini, labda imekuwa sumu tayari, hivyo kile kinachoharibika kinaweza kuleta madhara,” alibainisha Kaimu Mkurugenzi huyo wa Maabara ya TMDA - Kanda ya Ziwa.

Nyamweru aliongeza “Ndiyo maana hata ‘syrup’ ikishafunguliwa, haitakiwi kubaki kwa sababu inaweza kuleta madhara, tunahimiza watu wazingatie matumizi ya dawa kama walivyoelekezwa na wataalamu.

"Tunasisitiza dawa zitumike kwa usahihi kabla ya kuisha muda wake wa matumizi, ili kuepusha athari mbalimbali zinazoweza kumpata mgonjwa likiwamo tatizo la usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa.

Kwa undani zaidi, hivi karibuni hapa hapa  MATUKIO NA MAISHA BLOG tutakuchapia makala maalum itayoangazia jinsi wataalamu wa TMDA – Kanda ya Ziwa wanavyochunguza uwezo na ufanisi wa kiambata hai kinachopatikana ndani ya dawa.

Tutaangazia jinsi kiambata hai kinavyotoka ndani ya dawa kuingia mwilini mwa binadamu, ili kufikia lengo la kufanikisha tiba dhidi ya ugonjwa husika.

Uchunguzi ambao hufanywa na wataalamu ndani ya maabara hiyo kwa kutumia mashine maalum iliyoundwa mithili ya tumbo la binadamu (Dissolution Machine), waliyonayo. USIKOSE.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement