Jumapili, 31 Januari 2021

Januari 31, 2021


Na Mwandishi Maalum (ORCI) - Tanga

Watoa huduma za afya kutoka vituo mbalimbali ndani ya Mkoa wa Tanga, waliohudhuria mafunzo ya siku sita yaliyoenda sambamba na uchunguzi wa awali na matibabu ya saratani ya mlango wa kizazi, wamesema wamejifunza mengi na sasa wanakwenda kutekeleza kwa vitendo, kuisaidia jamii.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na waandishi wa habari,  wamesema ushirikiano kati ya Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga – Bombo, umekuwa ‘neema’ kwa Wana-Tanga.

Akizungumza, Ofisa Muuguzi kutoka Hospitali ya Wilaya ya Korogwe Vijijini (Makuyuni), Mahija Mhina (anayetoa elimu kwa wananchi pichani)  amesema kupitia mafunzo hayo ameweza kuelewa kwa kina kuhusu saratani hiyo hasa chanzo chake.

“Awali nilikuwa nafahamu saratani zote chanzo chake ni ulaji usiofaa, kumbe kwa saratani ya kizazi ina vyanzo tofauti kidogo, hii inatokana na maambukizi ya kirusi cha HPV (Human Papilloma Virus).

Ameongeza “Nimeweza kujua mabadiliko ya awali yanatibika na mwanamke anaweza kuepuka saratani hii kwa kujiweka mbali na vile vihatarishi vinavyoweza kuchochea kupata maambukizi kwa mfano kuepuka kushiriki ngono katika umri mdogo, kuzaa watoto wengi na vinginevyo.

Mahija Amesema kituo chao hakikuwa kikifanya huduma ya  uchunguzi wa awali mapema lakini sasa wameelewa umuhimu wake na kwamba anaporudi kituo chake cha kazi atahakikisha hilo wanalifanya.

“Tutatoa elimu kwa jamii kuwahamasisha waje mapema kwa uchunguzi wa awali, huduma hii ni bure, tutaueleza uongozi wa kijiji kwamba tutaanza kutoa huduma hii wakati wowote kuanzia sasa kituoni kwetu,” amebainisha.

Naye, Lameck Konga kutoka Kituo cha Afya Ngamiani amesema kwa upande wao wameanza muda mrefu kutoa huduma hizo za uchunguzi wa awali na tiba isipokuwa kwa wale wanaohitaji uchunguzi zaidi hulazimika kuwapa rufaa.

“Mimi ni msimamizi wa kitengo cha Ukimwi (CTC Incharge), hivyo nimekuwa nikishiriki katika masuala ya uchunguzi wa saratani baada ya kupata elimu.

“Lakini nimekuwa nikifanya kwa kiasi kulingana na uelewa niliojengewa, leo (jana), nimeongeza maarifa mapya yatakayonisaidia kuboresha huduma.

“Nimefurahi yamefanyika kwa vitendo, wakufunzi wetu wametusaidia, wameonesha ushirikiano wa kutosha, wamejaribu kuona kitu gani tunapaswa kufahamu, wametusaidia mno,” amesema.

Kwa upande wake, DK. Mgoye Marato kutoka Kituo cha Afya Ubwari (Muheza) amesema ni mara yake ya kwanza kushiriki mafunzo hayo, amejifunza Saratani hiyo katika hatua ya awali inatibika na kupona.

“Hivyo ni muhimu kufanya uchunguzi wa awali kwa kina mama ili kubaini iwapo kuna mabadiliko ya awali kwa sababu yenyewe huwa hayaoneshi dalili, dalili zinapoanza kuonekana tayari unakuta yamegeuka kuwa saratani,” amesema.

Ameongeza “Tumejifunza katika hatua za awali inatibika kwa wepesi na kupona kabisa, tumejengewa uelewa mkubwa, katika kituo chetu tulipata nafasi kuja watoa huduma wawili, hivyo tunaporudi  na mwenzangu tunakwenda kuweka mpango kazi wa kuifikia jamii.

“Kule kituo yupo pia mwenzetu mmoja ambaye alinufaika katika mafunzo ya awamu ya kwanza, maana yake nguvu katika kituo chetu imeongezeka, sasa tunakuwa watatu kwa pamoja tunakwenda kuisaidia jamii kwa kufikisha elimu, kufanya uhamasishaji waje mapema kituoni kwa uchunguzi wa awali,” amesisitiza.

Mkurugenzi wa Huduma za Kinga wa ORCI, Dk. Crispin Kahesa amesema kambi hiyo ya kampeni maalum ya uchunguzi wa awali wa saratani ya kizazi ilianza Januari 28, 2021 na kuhitimika Januari 30, 2021.

Amesema pamoja na uchunguzi wa saratani ya kizazi kambi hiyo pia imekwenda sambamba na mafunzo kwa watoa huduma za afya zaidi ya 25 kutoka vituo mbalimbali ndani ya Mkoa huo, pamoja na kufanya uchunguzi wa awali kwa saratani ya matiti na saratani ya tezidume.

Amesema 0RCI wamefanya kampeni hiyo kwa kushirikiana na Hospitali ya Bombo, kambi hiyo ni sehemu ya uteketelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan wakati wa mbio za hisani za NBC Marathon zilizofanyika Novemba 22, 2020.

“Kutokana na mbio hizo Ocean Road tulipokea ufadhili wa benki ya NBC wenye lengo la kutoa mafunzo ya uchunguzi wa awali na matibabu ya saratani ya kizazi kwa watoa huduma za afya 100 nchi nzima,” amebainisha .

0 maoni:

Chapisha Maoni