Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement

Baadhi ya wanawake waliojitokeza siku ya kwanza ya kampeni  ya uchunguzi wa awali na matibabu dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi leo Januari 28, 2021, katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga - Bombo, wakimsikiliza kwa makini, Muuguzi Mkuu wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Jesca Kawegere. 

Na Veronica Mrema – Tanga

Wanawake wapatao 1,000 wanatarajiwa kufanyiwa uchunguzi wa awali na matibabu dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi, wataalamu mabingwa wa saratani kutoka Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), wamepiga kambi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga (BOMBO).

Akizungumza na MATUKIO NA MAISHA BLOG, Mkurugenzi wa Huduma za Kinga wa ORCI, Dk. Crispin Kahesa amesema kambi hiyo ni sehemu ya kampeni maalum ya mafunzo, uchunguzi na matibabu ya awali dhidi ya saratani hiyo inafanyika kuanzia leo (Januari 28 2021) itafikia tamati Januari 30, 2021.

“Ni ushirikiano kati ya Ocean Road na Hospitali ya Bombo, lengo letu kwanza ni kuwapa mafunzo wahudumu wa afya katika kufanya uchunguzi wa awali saratani ya mlango wa kizazi na matibabu.

“Tunawajengea uwezo watoa huduma Mkoa wa Tanga, Halmashauri na Wilaya zote za mkoa huu, washiriki waliohudhuria mafunzo haya ni zaidi ya 25, tunawakaribisha wakazi wa Tanga kutumia fursa hii ambapo tutakuwa hapa kwa ajili ya kuwahudumia,” amebainisha Dk. Kahesa.

Ameongeza “Saratani ya kizazi inashika namba moja kwa idadi kubwa ya wagonjwa wanaohudumiwa Ocean Road, Mkoa wa Tanga ni miongoni mwa mikoa 10 ambako watu wameathirika na saratani hii, kwa hiyo program hii itasaidia kuibua wale wenye matatizo mapema, watapata matibabu mapema na hivyo tutaweza kujenga afya kwa kina mama.

Amesema ingawa walengwa wakubwa wa kampeni hiyo ni wanawake, hata hivyo wanaume hawajaachwa nyuma na kwamba wale watakaofika hospitalini hapo watapata fursa ya kufanyiwa uchunguzi wa awali wa saratani ya tezidume, wasisite kujitokeza.

Mkazi wa Tanga Mjini, Jafari Ali, amepongeza ushirikiano huo wa wataalamu wa Ocean Road na wenzao wa Mkoa wa Tanga kwa kufanya kampeni hiyo kwani imemuwezesha naye kupata fursa ya kufanya uchunguzi wa saratani ya tezidume.

“Niliona matangazo yaliyobandikwa, nikaamua kufika, nimepata vipimo wala hakuna tabu, nimechunguzwa kwa kipimo cha damu, leo tarehe 28 ni siku ya kwanza, 29 na 30 wataalamu watakuwa hapa Bombo, wanaume wenzangu wajitokeze na wanawake pia wafike kuchunguzwa saratani ya kizazi,” ametoa rai.

Mkazi wa Wilaya ya Mkinga, Asia Hussein Ngoma, amewasihi wakazi wenzake wa Tanga kuchangamkia fursa hiyo ya huduma ya uchunguzi na matibabu ya awali kwa saratani ya kizazi inayotolewa na wataalamu hao.

“Kule ninapoishi mimi ni kijijini, nilisikia matangazo redioni, nikafunga safari kuja hapa, nimeonwa na madaktari, wamenichukua vipimo vizuri, wamenihudumia vizuri, nawasihi na wenzangu waje, waonwe na wataalamu hawa wenye lugha nzuri, huduma nzuri, wahudumiwe, wafarijike,” ametoa rai.

Wananchi wakisikiliza maelekezo kwa makini.
Baadhi ya wanawake waliojitokeza siku ya kwanza ya kampeni  ya uchunguzi wa awali na matibabu dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi leo Januari 28, 2021, katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga - Bombo, wakimsikiliza kwa makini, Muuguzi Mkuu wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Jesca Kawegere, alipokuwa akieleza hatua za kujifanyia uchunguzi binafsi wa saratani ya matiti.
Wananchi wakisikiliza maelekezo kwa makini.

Wananchi wakisoma vipeperushi vya elimu kuhusu jinsi ya kutambua saratani ya mlango wa kizazi pamoja na saratani ya matiti walivyogawiwa.
Baadhi ya wataalamu wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) wanaotoa huduma katika kambi hiyo Maalum ya mafunzo, uchunguzi wa awali na matibabu dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga -Bombo, wakifuatilia jambo kwa makini.

Picha zote na Veronica Mrema.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement