Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement


Na Veronica Mrema - Dar es Salaam

Upatikanaji wa taarifa sahihi za saratani ni miongoni mwa changamoto ambazo zilikuwa zinaikabili jamii nchini Tanzania, sasa imepatiwa ufumbuzi katika Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI).

Kituo maalum cha upatikanaji na utoaji wa taarifa sahihi kuhusu magonjwa ya saratani kimezinduliwa mapema hii leo ndani ya Taasisi hiyo kubwa, ya Umma inayotoa matibabu dhidi ya saratani ambayo imekuwa ikipokea wagonjwa kutoka nchi nzima.

Kituo hicho ambacho kimeanza kwa kutoa taarifa sahihi kuhusu saratani ya matiti, ni 'matunda' ya mradi ambao Ocean Road umeupata kupitia wadau wake wa Spack.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kituo hicho, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Saratani Ocean Road ambaye pia ni msimamizi wa mradi huo, Nazima Dharsee amesema andiko maalum kuomba mradi huo waliliwasilishwa katika Taasisi ya Muungano wa Kimataifa wa Kudhibiti Saratani Duniani (Union for International Cancer Control) la Geneva, Uswizi na mwaka 2019 Tanzania ilifaulu kupatiwa mradi huo.

"Saratani ya matiti inaongoza katika saratani za kina mama duniani kwa hapa Tanzania ni ya pili baada ya shingo ya kizazi na tunaona idadi ya kina mama wanaoathirika na saratani hizi inazidi kuongezeka na inaleta athari," amesema.

Ameongeza "Saratani inahusisha matibabu mbalimbali ikiwamo uchunguzi, upasuaji, dawa kemia, mionzi na nyinginezo.

"Saratani huleta athari kubwa nyingine kwa maisha ya mgonjwa na Jamii yake mbalimbali ikiwamo kisaikolojia na hata kijamii.

"Miongoni mwa mahitaji ambayo huwasumbua wagonjwa (wananchi) ni mahitaji ya taarifa iliyo sahihi na kwa muda sahihi, inayoweza kumsaidia mgonjwa kufanya maamuzi kuhusu matibabu yake na kuzingatia kukamilisha na kuyamaliza kwa wakati," amesema.

Amesema hayo ni mahitaji ambayo yanajulikana dunia nzima na katika nchi zilizoendelea vituo na huduma ya utoaji wa taarifa ni sehemu kubwa ya huduma kwa wakina mama na kwa wagonjwa wa saratani.

"Katika sehemu zetu kutokana na changamoto tofauti tofauti inakuwa vigumu kupata huduma hizo, kwa sababu huu ni mradi wa saratani ya matiti tumeanza nayo na baadae tutaongeza pia saratani nyinginezo," amesema.

Ameongeza "Timu yetu tumeiandaa vizuri kwa mafunzo yanayoendelea, ili kuweza kujibu maswali ya wananchi. 

"Pia tumeandaa vipeperushi aina saba vitakavyojibu maswali ya wateja wetu, sehemu ya tatu ya mradi tutaanzisha (call center) itakuwa ni simu ama jumbe maalum ya bure ambazo wananchi wataweza kupiga au kupata taarifa sahihi," amesema.

Ameongeza "Kitakuwa msaada mkubwa kwani tumefanikiwa kukaa na wakina mama hawa kwenye vikundi na kuwauliza...  Hitaji la taarifa ni kubwa mno kwa kina mama na wagonjwa wa saratani kwa ujumla.

"Wengi wanapoteza muda na fedha na hata kufika wakiwa wamechelewa tiba," amesisitiza Dk. ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Taaluma Ocean Road.

Akifungua kituo hicho, Mkurugenzi wa ORCI, Dk. Julius Mwaiselage ameipongeza timu hiyo iliyofanikisha kuandika andiko hilo hatimaye Tanzania kupata mradi huo.

"Saratani Ni ugonjwa unaoongezeka duniani kote hasa nchi zetu zinazoendelea kila mwaka kuna wagonjwa wapya milioni 18 na wanaofariki ni karibu mil 9.6," amesema.

Amesema zipo sababu mbalimbali zinazosababisha ugonjwa huo kuongezeka kama vile mtindo wa maisha, ikiwamo ya matiti ambayo miaka saba iliyopita ilishika namba nne leo hii inashika namba mbili.

"Ikiwa hatua hazitachukuliwa itaendelea kuathiri wanawake wengi, hivyo hatua hii ni muhimu kwani changamoto tunayoipata ni wagonjwa kuja katika hatua za juu za ugonjwa," amesema.

Ameongeza "Serikali imefanya juhudi kubwa kuimarisha huduma za uchunguzi na matibabu lakini eneo la taarifa sahihi za magonjwa ya saratani ilikuwa ni changamoto.

"Ndiyo maana tunashukuru kwa kituo hiki kuanzishwa, ni muhimu pia timu hiyo ya Spack pia kutoa elimu kupitia mitandao ya kijamii ambako kuna upotoshaji mkubwa," amehimiza Dk. Mwaiselage.

Washiriki mbalimbali wa ufunguzi huo, wakiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa ORCI, Dk. Julius Mwaiselage.

Washiriki mbalimbali wa ufunguzi huo, wakiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa ORCI, Dk. Julius Mwaiselage.

1 Maoni

  1. Nimepimwa katika kituo mojawapo Cha Afya nikaambiwa Nina tezi Dume.Toka Jana nimeishiwa matumaini ya kuishi.Doctor kwa bahati mbaya alinieleza kisiasa kuwa ni ugonjwa wa kawaida,Ila baada ya kusoma makala yenu,nimejikuta kumbe ni ugonjwa ambao unaweza kukatisha maisha ya mtu haraka.
    ✓Je,Kuna tofauti gani Kati ya saratani na Cancer?
    ✓Je,nifanye nini ili niweze kuondokana na tatizo hili?
    ✓Je,upasuaji unaweza kufanyika katika kituo chochote Cha Afya?
    ✓Je,ni madhara yapi zaidi yanaweza kujitokeza Kama huduma sahihi haziwezi kutolewa kwa mgonjwa?

    JibuFuta

Chapisha Maoni

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement