Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement


Na Mwandishi Maalum - Dodoma

Taasisi za benki zote nchini zimepewa siku tatu kuhakikisha zinaweka vipukusi 'sanitizers' kwenye maeneo ya ATM na 'exchanges' ili jamii Iendelee kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya CORONA (COVID - 19).

Serikali imesisitiza Tanzania ni salama lakini jamii inapaswa kuendelea kujikinga kwani bado ugonjwa huo unaikabili dunia na kuna tishio la wimbi jipya la virusi hivyo Barani Afrika.

Alihojiwa na moja  ya chombo kimoja cha habari jijini Dodoma, ni hatua gani Tanzania inaendelea kuzichukua kuhakikisha jamii inakingwa dhidi ya wimbi jipya la maambukizi ya COVID - 19, Mkurugenzi wa Idara ya Kinga wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Leonard Subi amesema hayo.

Ameongeza "Watanzania kinga ni bora kuliko tiba tusije tukasubiri kuingia kwenye mitungi ya oksijeni, tuendelee kujikinga. Hali ni shwari hata Rais Samia Suluhu Hassan anachukua tahadhari kujikinga na maambukizi akikutana na watu mbalimbali.

"Tanzania tupo salama lakini tunatakiwa kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi hayo ambayo kwa takriban mwaka na nusu sasa bado yanaikabili dunia.

"Wizara kazi yetu ni kuendelea kihimiza wananchi kujikinga dhidi ya COVID - 19, tuendelee kuchukua tahadhari, tuliona katika wimbi la kwanza 2020 wananchi waliitika wito wa kunawa mikono, kuvaa barakoa, kukaa umbali, kufanya mazoezi, lishe bora na masuala mengineyo," amesema.

Dk. Subi (picha na maktaba) ameongeza "Tunataka kusisitiza kinachotokea Afrika maambukizi yanaongezeka na baadhi ya Wakuu wa Nchi wanatoa matamko kama tulivyomsikia Rais wa Uganda na sisi Tanzania tumekuwa na mwingiliano na uhusiano mwema na nchi jirani.

"Mashuleni, vituo vya afya tuliweka vifaa kwa kunawa kwa maji safi tiririka, tunawe mikono.

"Hatua tulizopiga tusije tukarudi tulipotoka, sisi Serikali tunaendelea kufuatilia kwenye mikusanyiko, mabasi, ndege wachukue tahadhari.

Amesema Serikali imeimarisha hatua za ufuatiliaji kwenye maeneo ya mipaka, viwanja vya ndege watu wanapimwa hali zao za afya.

"Tunafahamu kuna tishio kubwa la anuwai mpya (aina mpya ya kirusi cha CORONA) duniani,  kuna cha India, Uingereza, Afrika Kusini na Brazil ambavyo vimeendelea kugharimu maisha ya watu.

"Tunashirikiana na Mamlaka za mikoa, Serikali za Mitaa kuhakikisha tunaendelea kuwafikia wananchi," amesema.

Dk. Subi pia ametoa rai kwa vyombo vya habari kuendelea kuelimisha jamii na kuihamaisha kujikinga dhidi ya maradhi hayo.

"Tunaomba vyombo vya habari mtumie muda wenu kidogo hata mara moja au mbili  kwa siku kuwakumbusha wananchi kuchukua tahadhari juu ya COVID - 19.

"Suala la mapambano dhidi ya magonjwa si la hiyari, tuna maafisa afya pia, Watanzania suala la afya ni la muhimu na la msingi kwa Maendeleo ya Taifa tukicheza tutarudi nyuma, kila mmoja atimize wajibu wake.

"Kwenye familia ndoo za kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni ziwepo, bebeni vipukusi na katika maeneo ya mikusanyiko tunashauri barakoa zivaliwe kwa kuzingatia mwongozo tuliotoa na kwenye nyumba, magari kuwe na mzunguko wa hewa, tujikinge," ametoa rai Dk. Subi.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement