Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement


Na Veronica Mrema

Shirika la Fedha Ulimwenguni (IMF), limepanga kutumia takriban Dola za Marekani Bilioni 650 katika awamu ya pili ya mpango wa kusaidia kwa dharura uchumi wa nchi mbalimbali zinazoendelea kutokana na madhara ya janga la CORONA, Tanzania ikiwamo.

Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa (pichani) amesema hayo leo katika mkutano wake na waandishi wa habari alipokuwa akizungumza kuhusu masuala mbalimbali ya Serikali.

Amesema Rais Samia Suluhusu Hassan ameshiriki mazungumzo na mtandao wa viongozi wanawake wa Afrika ambao unaongozwa na Rais Mstaafu wa Liberia, Ellen Sirleaf.

Amesema Rais Samia pia amefanya mazungumzo na Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Gutterres.

"Rais ameagiza Wizara ya Fedha kuandaa maandiko ili nchi yetu inufaike na mpango huu," amesisitiza Msigwa.

Msigwa amesema Rais Samia  ameamua kuimarisha juhudi za kupambana na janga la Korona kwa kutoa nafasi kwanza kwa Wataalamu kuishauri Serikali juu ya namna ya kukabiliana na ugonjwa huo.

Amesema Kamati hiyo ya Wataalamu inayoongozwa na Prof. Said Aboud ilifanya tathmini ya kitaalamu na kuwasilisha mapendekezo Serikalini.

"Rais amekabidhiwa mapendekezo hayo yenye mpango kazi wa kutafuta rasilimali kwa ajili ya utekelezaji wa mpango mkakati wa Taifa wa kukabiliana na janga la CORONA.

"Mapendekezo ya mpango kazi wa uratibu wa utoaji wa chanjo ya ugonjwa huo, pia yaliwasilishwa na kamati hiyo ya wataalamu," amesema.

Ameongeza "Balozi na taasisi mbalimbali za Kimataifa hizi zimeruhusiwa kuleta chanjo kwa ajili ya raia wa nchi zao na watumishi wao.

Amesema licha ya janga hilo kuendelelea kutikisa dunia pamoja na shughuli za uzalishaji, Serikali inaendelea kuwahimiza Watanzania wote kuendelea kuchapa kazi za uzalishaji mali kwa juhudi na maarifa.

Amesisitiza wananchi wachape kazi huku wakichukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Korona, zikiwemo kunawa mikono kwa maji tiririka.

"Hali ya Uchumi wetu ni nzuri japo na sisi tumepatwa na madhara ya Korona kama ilivyo kwa nchi zingine dunia. 

"Uchumi wetu uliokuwa unakua kwa wastani wa asilimia 6.9 umeshuka kidogo hadi wastani wa asilimia 4.7," amesema.

Amesema Serikali inatarajia   uchumi  utaendelea kukua vizuri kutokana na hatua madhubuti ambazo zimechukuliwa.

"Mfumuko wa bei kwa sasa ni wastani wa asilimia 3.3 ambayo ni kiasi kizuri," amebainisha.

Ameongeza "Akiba ya fedha za kigeni ni nzuri ambazo zinatosha kununua bidhaa na huduma kwa muda wa zaidi ya miezi 4.7.

Ameongeza "Nchi yetu imechukua hatua madhubuti za kuulinda utalii kwa kuzingatia miongozo na masharti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) dhidi ya ugonjwa wa Korona kwa kuwahakikishia watalii usalama wao wakiwa hapa Tanzania katika vivutio vyetu vya utalii.

"Matarajio yetu ni kuwa watalii watazidi kuongezeka na mmeona watu maarufu duniani wanakuja," amesisitiza.

Msigwa amesema Tanzania inazidi pia kuimarisha diplomasia ya uchumi na nchi mbalimbali, ukusanyaji wa mapato, ujenzi na usimamizi wa miradi ya maendeleo ili kuendelea kunufaisha Taifa na wananchi wake.

Amesema Serikali itaendeleza ushirikiano mzuri wadau wake ikiwamo Sekta binafsi, vyombo vya habari, taasisi na mashirika ya kimataifa

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement