Recent Post


 


moja

Responsive Advertisement

Na Veronica Mrema - Dar es Salaam

Mfuko maalum ulioundwa kwa teknolojia ya kisasa sawa sawa na ile ya kondomu uitwao kitaalamu 'SILOBAG' umesaidia kupunguza vifo vya watoto wanaozaliwa na tatizo la tumbo wazi/utumbo nje kwa 38%.

Idadi hiyo ni ya watoto wenye tatizo hilo wanaopatiwa matibabu ndani ya Hospitali ya Taifa Muhimbili {MNH}, Kabla ya hapo kwa 95% hadi 100% walifariki dunia.

Yamebainishwa hayo leo na Dkt. Hedwiga Swai kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili, wakati wa Siku ya Kimataifa ya Uelimishaji kuhusu Watoto wanaozaliwa na tumbo wazi, kwa mara ya kwanza Muhimbili imesherehekea maadhimisho hayo.

"Hili ni tatizo kubwa hasa Ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara, duniani 94% walifariki dunia lakini katika nchi za wenzetu zilizoendelea wameweza kupunguza vifo hadi 4%.

"Muhimbili tumeweza kupunguza 38% kwa teknolojia hii na tayari wataalamu wetu wa Kitengo cha upasuaji wa watoto wametoa mafunzo kwa madaktari wa Mwanza, Mbeya wakitumia kifaa hicho maalum ambacho kwa sasa tunakipata kwa msaada kutoka Ujerumani," amesema.

Ameongeza "Ni kitu kimekaa kama kondomu, tunaweza kutengeneza hapa hapa nchini itapunguza gharama, Dkt. Zaitun {Bokhari, Mkuu wa Kitengo hiki}, amenieleza wanataka kukiandikia kiwanda cha salama kondom ili watengeneze mfuko huu.

"MNH imekuwa ikiunga mkono kila juhudi inayoanzishwa, mtuambie mahitaji na tutanunua wakati pia mkiendelea kuongea na salama," amesema.

Awali, Daktari Bingwa Mbobezi Mwelekezi wa Upasuaji wa Watoto, Petronila Ngiloi amesema kwa uzoefu wake wa miaka 30 sasa ameshuhudia tatizo hilo ni la miaka mingi nchini na watoto wengi walipoteza maisha.

"Unamuona mtoto mzuri lakini tatizo utumbo na wakati hadi maini changamoto ilikuwa mtu hawezi kuishi matumbo yakiwa nje lazima yarudishwe ndani.

"Lakini vifaa vilikuwa duni, wataalamu wachache mno, hatukuwa na vyumba vya maalum vya ICU kwa ajili ya watoto, ilikuwa kubahatisha ili kuokoa maisha yake.

Ameongeza "Wengine tuliweza kuwaokoa kwa kutumia nguvu sana lakini wengi walipoteza maisha, walishindwa kupumua.

"Zaidi ya 95% tuliwapoteza, sikumbuki kama wapo waliopona kama wapo ni wachache sana," amesisitiza.

Dkt. Ngiloi amesema mwaka 2000 akiwa masomoni Afrika Kusini ndiko ambako aliona mfuko huo ukitumika  kuyahifadhi na kuyarejesha {matumbo} taratibu kama wiki mbili

"Walikuwa wanapona, walikuwa na ICU maalum ya watoto na aliwekewa mashine ya kusaidia kupumua kipindi chote cha uangalizi hadi kupona.

Ameongeza "Mwaka 2000 tulianza kufanya huduma hii kwa kutumia mfuko mbadala {wa mkojo}, lakini bado ilikuwa ni changamoto.

Naye, Dkt. Zaitun amesema mfuko wa mkojo ulikuwa changamoto kwani kulikuwa na uwezekano mkubwa wa kupasuka wakati mtoto akiendelea kupata huduma na ilikuwa na kiwango kikubwa zaidi cha joto ambalo halikutakiwa.

"Tayari tumeweza kupeleka 'sample' ya mfuko huu kwa Bohari Kuu ya Dawa {MSD} pamoja na kiwanda cha Salama na wametudokeza upo uwezekano wa kutengeneza mfuko huu nchini," amesema.

Tafiti duniani zinaeleza mtoto mmoja hadi wawili katika kila watoto 100,000 huzaliwa na tatizo hilo ambalo kitaalamu huitwa Gastroschisis na Barani Afrika wengi huzaliwa nalo.

Post a Comment

saba

nane


 


sita

Responsive Advertisement