Na Veronica Mrema
Mzigo wa gharama za usafiri kwa mwananchi kufuata huduma za
matibabu dhidi ya Homa ya Ini kutoka maeneo mbalimbali ya nchi hadi Hospitali
ya Taifa Muhimbili {MNH}, utapungua Tanzania.
Ahueni hiyo inatarajiwa kwani Serikali kupitia
Wizara ya Afya tayari imekamilisha mwongozo wa matibabu
ya Homa ya Ini.
Mwongozo huo utatumika kutoa maelekezo ya tiba hiyo nchi
nzima ili kumpunguzia mwananchi gharama ya kusafiri umbali mrefu kwenda kupata
tiba hiyo, Muhimbili.
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amebainisha hayo wakati
alipotoa tamko lake kwa umma leo ikiwa ni Siku ya Homa ya Ini
Duniani ambayo huadhimishwa kila mwaka julai 28.
Waziri Ummy ameeleza hatua nyingine nyingine zinazotekelezwa na Serikali kupambana na ugonjwa huo.
“Katika kuendelea
kudhibiti homa hii, Wizara pia itaendelea kusimamia Mpango Mkakati wa Taifa wa
Kudhibiti na Kutomeza Ugonjwa wa Homa ya Ini nchini wa mwaka 2018-2023.
Amesema Wizara inaendelea kuaandaa vielelezo vinavyohusu
ugonjwa huo {Viral Hepatitis}, ili kuuelimisha umma hususan namna gani maambukizi
yanaweza kuzuiwa.
Amesema Wizara inaendelea kutoa elimu ya ugonjwa huo kupitia
vyombo vya habari pia.
“Utaratibu wa kuwapatia mama wajawazito kinga ya kuzuia
maambukizi ya Homa ya Ini aina B kutoka kwa mama mjamzito kwenda kwa mtoto zipo
katika hatua za mwisho,” amesema nao unaendelea.
Ameongeza “Tunaendelea na mchakato wa kuunganisha huduma ya
homa ya Ini na mpango wa taifa wa kudhibiti UKIMWI nchini, ili iwe rahisi
kuwekea mikakati ya kudhibiti ugonjwa huu.
Amesema ripoti ya Homa ya Ini ya mwaka 2021 ya Shirika la
Afya Duniani {WHO} zinaeeleza mwaka 2019 watu 296 duniani waligundulika wanaishi
na Homa sugu ya Ini kirusi aina B.
Amesema takwimu zinaeleza zaidi ya nusu {66%} ya maambukizi
hayo yalitoka Bara la Afrika huku watu wapatao milioni 58 walikuwa wanaishi na
maambukizi ya Homa ya Ini kisuri aina C.
Ameongeza “.., na wakati huo huo kulikuwa na vifo 820,000
duniani vilivyosababishwa na Homa ya Ini kirusi aina B.
“Kwa Tanzania, takwimu kutoka Mpango wa Taifa wa Damu
Salama (NBTS) zinaonesha kuwa maambukizi ya Homa ya Ini aina ya B miongoni mwa wachangiaji
damu kwa miaka mitatu ni kama ifuatavyo mwaka 2018 (4.4%), mwaka 2019 (5.9),
mwaka 2020 (6.1%) na mwaka 2021 (5.3%).
“Aidha, kwa kipindi hicho maambukizi ya Homa ya Ini aina C
yameendelea kuwa ni ya 2.3%,” amebainisha.
Amesema Ugonjwa wa Ini aina ya A na E unaweza kuzuilika kwa
kuboresha usafi wa mazingira, utayarishaji wa vyakula katika hali ya usafi na
matumizi ya maji safi na salama.
Amesema Ugonjwa wa Homa ya Ini aina ya B, C na D inazuilika
kwa kutekeleza afua zote za kuzuia virus vya VVU/UKIMWI.
Amehimiza wananchi kuchukua tahadhari ikiwa ni pamoja na
kupata chanjo dhidi ya ugonjwa huu kwa wale ambao hawajawahi kuipata kwani
zinatolewa nchini Tanzania, akibainisha kwamba tangu mwaka 2002 watoto wamekuwa
wakipatiwa chanjo hiyo.
“Niwasisitize wadau wote katika sekta binafsi na umma
kuendelea kuona umuhimu na kutoa kipaumbele na kuwekeza katika mapambano dhidi
ya ugonjwa wa Homa ya Ini nchini na hatimaye kuweza kuutokomeza kabisa ifikapo
mwaka 2030,” ametoa rai.
Chapisha Maoni