Dodoma
Idadi ya bidhaa za dawa,
vifaa tiba na vitendanishi vinavyosajiliwa nchini imeongezeka ndani ya kipindi
cha mwaka 2021/22 katika Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania {TMDA}.
Yameelezwa hayo leo Jijini
hapa na Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Adam Fimbo alipotoa taarifa ya mafanikio ya
Taasisi hiyo katika kipindi hicho, mbele ya waandishi wa habari, amesema jumla
ya bidhaa 1,286 zimesajiliwa.
“kati yake bidhaa za dawa za binadamu na mifugo
ni 933 na vifaa tiba na vitendanishi ni 353,” amebainisha.
Fimbo ameongeza “Kwa idadi hii jumla ya
bidhaa zilizosajiliwa hadi sasa imefikia 8,831 ambapo kati yake bidhaa za dawa ni
6674 na vifaa tiba na vitendanishi ni 2,157.
“Hii inaashiria kiasi kikubwa cha dawa
zinazotumika Tanzania zimehakikiwa na hivyo ni bora, salama na fanisi kwa
matumizi ya binadamu,” amesisitiza.
Kuhusu usajili wa majengo na ukaguzi, amesema
katika kipindi hicho TMDA imesajili jumla ya
maeneo 467 yanayojihusisha na biashara za bidhaa zinazodhibitiwa kwa lengo la kuhakikisha kuwa maeneo husika
yanakidhi vigezo ili kutoathiri ubora, usalama na ufanisi wa bidhaa.
“Aidha, jumla ya maeneo 10,938 yanayojihusisha na biashara
ya dawa, chanjo, vifaa tiba na vitendanishi yalikaguliwa kwa mwaka 2021/22
ikiwa ni ongezeko la maeneo 92 yaliyokaguliwa ikilinganishwa na maeneo 10,846
yaliyokaguliwa mwaka 2020/21.
Chapisha Maoni